UWEZA WA DAMU YA YESU KATIKA KUFUTA HATI YA MASHITAKA YA MTU MBELE ZA MUNGU

 Lengo la somo hili ni kukusaidia kujua na kuzitumia sheria mbalimbali za ulimwengu wa kiroho.

Mashitaka ni neno la kisheria, lenye maana ya kutuhumiwa kufanya kosa Fulani.

Hati ni maelezo halali au kopi yanayoelezea makosa aliyofanya mtu, na huwa yanatumiwa kama ushahidi kwenye baraza la maamuzi (mahakama). Lengo likiwa ni kukuondolea uhalali wa kupokea haki zako unazostahili kuzipata kutoka kwa Mungu.

Kumbuka, kila aliyeokoka ana “package” yake kutoka kwa Mungu. Ile tu kwamba ameokoka kunampa Mungu uhalali wa kukuhudumia kwa ukaribu zaidi.

-          Sasa hati ya mashtaka inaondoa huo uhalali wa wewe kupokea haki zako kutoka kwa Bwana.

Wakolosai 2 : 14  - 15

“akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushtaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu, akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani”

-          Biblia inaelezea kitu kinachoitwa hati ya mashtaka kwamba ina uadui kwetu kwa sababu lengo ni kukuzuia usipate unachostahili kukipata kutoka kwa Mungu ambaye ni Baba yako.

-          Kinachofuta hati ya mashtaka si msalaba bali ni damu ya Yesu iliyomwagika msalabani. Wakolosai 1 : 20

MAMBO MATATU YA MUHIMU YA KUFAHAMU KWANZA

A.     Kuna sheria zinazotawala katika ulimwengu wa kiroho

Kuna sheria zinazotawala katika ulimwengu wa roho ambazo ni lazima mtu wa rohoni uzifahamu. Hizo sheria zinafanya kazi katika ulimwengu wa roho na aliyeziweka ni Mungu mwenyewe.

Sheria ni taratibu na kanuni zilizowekwa mahali Fulani au katika mazingira Fulani ili kutoa muongozo wa mwenendo wa mahali husika, ikiwemo kuonyesha haki na wajibu wa kila anayehusika na mazingira hayo au mahali hapo.

-          Ni Mungu mwenyewe kaziweka hizo sheria lakini pia yeye mwenyewe anazifuata hawezi kuzivunja.

-          Kuna mambo ambayo itakuwa ni vigumu kuyapata hata kama umeokoka kwa sababu ni lazima ufuate sheria za kiroho kuyapata.

Zipo sheria nyingi katika ulimwengu wa kiroho zinazofanya kazi lakini mojawapo ni kwamba “Mungu hana ushirika na dhambi”. Isaya 59 : 1 - 2

-          Tafsiri yake ni kwamba mtu atendaye dhambi hana ushirika na Mungu, kwa hiyo hawezi akapokea chochote kutoka kwa Mungu.

Zipo sheria nyingi sana, baadhi ya hizo ni:

         i.            Sheria ya dhambi na mauti – Warumi 8 : 1 – 2 & Warumi 6 : 23

       ii.            Sheria ya uzima – Warumi 8 : 1 – 2 & Yohana 11 : 25 – 26

     iii.            Kuna sheria zinazohusu uchumi au mafanikio – Yeremia 29 : 7, 11

     iv.            Kuna sheria zinazohusu utawala wa kimaeneo kwa nguvu ya fedha. Luka 19 : 11 – 27 – kuna uhusiano uliopo kati ya kuwa na mali nyingi inayopelekea kuwa na nguvu ya utawala au ushawishi katika utawala uliopo.

       v.            Sheria ya kurithi. Waebrania 9 : 16 – 17

 

B.      Kila tendo analolitenda mwanadamu linarekodiwa katika nyaraka zilizopo katika ulimwengu wa roho

Inawezekana ikawa ni matendo mema au mabaya, yote yanarekodiwa.

-          Matendo mema yanaleta thawabu bali matendo mabaya yanaleta adhabu.

-          Baadhi ya maeneo yanakotunzwa kumbukumbu za matendo ya watu ni kama vile:

i.                     Aridhi/nchi na mbingu – Yeremia 22 : 29 – 30 & Kumb 30 : 19

Katika ulimwengu wa kiroho ardhi ina uwezo wa kutunza kumbukumbu, inasikia n.k

ii.                   Vitabu vya mbinguni – Ufunuo 20 : 12

Kwa hiyo, kila tendo afanyalo mwanadamu linaandikwa mahali.

-          Matokeo ya makosa uliyoyafanya yakaandikwa kwenye kumbukumbu za kiroho huwa yanaweza yakakupata wewe tu au hata uzao wako baada yako.

-          Makosa au dhambi zilizotendwa na mtu halafu adhabu yake ikapita mpaka kwa watoto wake huwa yanaitwa “uovu”. Uovu ni dhambi ambayo hujafanya wewe lakini kwako imepita kama adhabu.

-          Hivyo Mungu anaweza akapatiliza uovu wa baba kwa watoto wake hata kizazi cha tatu na cha nne. Na pia anaweza akaachilia rehema zake vizazi baada ya vizazi. Kutoka 20 : 5 - 6

 

C.      Katika ulimwengu wa kiroho kuna mahakama.

Mahakama ni eneo ambalo hukumu mbalimbali zinatolewa kulingana na sheria zilizopo.

-          Kuna kuwa na upande wa mshitakiwa na upande wa mshitaki, na kuna kuwa na hakimu.

-          Mungu ndiye anayesimama kama Hakimu, Zaburi 7 : 11 & Zaburi 9 : 8. Mtu anasimama upande wa mshitakiwa na Shetani anasimama kama mshitaki. 1 Petro 5 : 8 & Ufu 12 : 10

-          Shetani huwa anachukua hati iliyoandikwa makosa yako halafu anakwenda kukushitaki mbele za Mungu.

-          Lengo la Shetani kukushitaki mbele za Mungu ni ili akuondolee uhalali wakupokea haki zako kutoka kwa Mungu.

-          Mashitaka yanaweza kukuondolea uhalali huo wa kupokea haki zako. Haki ni chochote unachostahili kukipata kutoka kwa Mungu. Inawezekana ikawa ni afya njema, maisha ya mafanikio, elimu bora, mafanikio katika biashara au kazi, utumishi mwema n.k.

-          Mungu anaposimama kama hakimu huwa hayupo upande wako bali huwa anasikiliza hoja zenye nguvu ili atoe maamuzi (atoe hukumu). Isaya 41 : 21 & Isaya 43 : 26

NB: Sasa tambua kwamba, ili Shetani aweze kukuzuia usifanikiwe katika mambo yako huwa anaangalia sheria inayompa uhalali wa kukutesa ndipo anakutesa. Huwa anatafuta kama kuna kosa au uovu uliopo kwenye maisha yako ili kwa kupitia kosa hilo ndipo akutese. Lakini pia hata kama akikosa huwa anaweza kukutengenezea mazingira ya kumkosea Mungu ili yeye apate kitu cha kukushitakia mbele za Mungu.

-          Lengo lake ni kukuangusha tu.

Shetani akipata uhalali mahali, huwezi kumuondoa usipoondoa kwanza ule uhalali wa yeye kukaa hapo.

Mfano: Marko 5 : 1 – 17

-          Ulishawahi kuona Yesu anakemea pepo halafu pepo linakataa kutoka?

-          Yesu alikemea pepo litoke wakati lile pepo limepata uhalali wa kukaa katika lile eneo ndio maana pepo likamwambia Yesu nakuapisha kwa Mungu usinitese, na pia lilimwambia kuwa asiwapeleke mbali na mipaka ya nchi ile. Kwa sababu wanaikalia ile nchi kihalali. Na wale watu hawakumkaribisha Yesu bali walimsihi aondoke mipakani mwao.

-          Hii inaonyesha kuwa kuna mambo hawa watu wa ule mji waliyafanya yakawapa yale mapepo kibali na uhalali wa kukaa kwenye eneo lao hivyo hawawezi kutoka kama huo uhalali haujaondolewa.

-          Vivyo hivyo na hata wenye familia yako kama mapepo yanakaa kihalali basi huwezi kuyakemea mpaka ufute kwanza huo uhalali walionao ndipo uwakemee watoke.

-          Watu wengi huwa tunakimbilia kuyakemea mapepo yatoke ndani ya mtu bila kujua hayo mapepo yameingiaje. Ni vizuri ukajua kwanza mlango walio ingilia ndipo utajua namna ya kuomba.

NB: Kwa hiyo, unapokwenda mbele za Mungu ambaye ndiye hakimu, kujitetea kwako ndiko kutakupa haki yako.

-          Lakini huwezi ukajitetea mwenyewe bila kuwa na msaada wa Yesu kwa sababu Yesu ndiye anayesimama kama wakili na mwombezi wetu kwenye mahakama ya kiroho. Waebrania 7 : 24 - 25

-          Yesu anachofanya huwa ni anakuja na ushahidi wa damu yake ambayo imemwagika msalabani ikafuta hati inayotushitaki katika jambo lolote lile.

-          Kwa lugha nyingine ni kwamba Yesu anasema hati aliyonayo shetani ni hati “fake” bali ile hati “orijino” ilishafutwa msalabani kwa damu ya Yesu.

-          Wewe mwenyewe huwezi ukajitetea ukamshinda shetani kwa sababu yeye shetani anajua sheria za ulimwengu wa kiroho zaidi ya unavyojua na huwa anatumia udhaifu wa kutokujua sheria ili kukutesa. lakini pia shetani huwa anatumia hila au udanganyifu kukutesa maana yake anaweza akakutesa kwa kutumia hati feki.

-          Yesu pekee ndiye wakili mwaminifu na ndiye anayetuombea kwa sababu ya upendo wake kwetu hataki mtu yeyote ateswe na nguvu za giza. Yeye ndiye aliye kufa msalabani kwa ajili yetu kwa hiyo ana upendo wa kweli na watu wake.

Damu ya Yesu pekee ndiyo inayoweza kufuta uhalali wa shetani kutawala maisha yako. Ina uwezo wa kufuta mashitaka yote ambayo shetani anayapeleka kwa Mungu juu yako. Ina uwezo wa kufuta kumbukumbu zote zilizoandikwa kukuhusu wewe ambazo zimebeba adhabu katika ulimwengu wa roho.

Damu ya Yesu ilipomwagika pale msalabani ilifanya kazi nyingi sana sio tu kutuosha dhambi zetu bali pia kufuta hati zinazotushitaki. Kwa hiyo usiangalie upande mmoja tu wa kazi ya Damu ya Yesu bali uiangalie kwa mapana yake ndipo utaona kazi zilizofanywa kwa damu ya Yesu.

Kumbuka kwamba, Mungu anasimama kama hakimu, kwa hiyo mtu usipojua namna ya kuitumia damu ya Yesu ili kufuta mashitaka juu yako basi ujue utaendelea kuonewa na nguvu za giza sana.

-          Biblia inasema “eleza mambo yako upate kupewa haki yako” Isaya 43 : 26

-          Maana yake usipoeleza mambo yako na usipojua namna ya kujitetea basi hutopata haki yako.

Katika mahakama za kawaida hapa duniani, si kila anayehukumiwa ni mtenda kosa bali kuna ambao walishindwa kujitetea ikapelekea kukosa haki zao.

-          Ushahidi wa anayekushitaki unaweza ukakushinda kujitetea kwako wewe unayeshitakiwa, hivyo ikapelekea kukosa haki uliyostahili kuipata.

 

Namna ya kushughulikia kuondoa umiliki halali wa shetani juu ya kile unachokiombea katika maisha yako.

i.                     Omba toba kwa Mungu juu ya nafsi yako.

ii.                   Omba toba juu ya kosa lililompa shetani nafasi ya kuja na kumiliki kwenye maisha yako kihalali.

iii.                 Halafu tumia damu ya Yesu kufuta uhalali huo wa shetani wa kukumiliki

iv.                 Vunja na haribu kazi zote za shetani zilizopitia kwenye mlango huo aliopitia kuingia kwenye maisha yako.

v.                   Mkaribishe Roho mtakatifu ayatawale maisha yako. Luka 11 : 24 – 27

NB: Mlango anaopitia shetani kuingia kwenye maisha yako unaweza ukawa ni maneno ya kinywa chako, matendo yako (dhambi) au maovu (dhambi zilizotendwa na wazazi wako au vizazi kabla yako).

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...