JIFUNZE KUWA NA HALI YA KUMPENDA MUNGU KAMA NGUZO YA MAHUSIANO YAKO NA MUNGU WAKO

 Msisitizo wa somo hili ni kujifunza kuwa na mahusiano ya ngazi ya juu kabisa na Mungu wetu katika msingi wa upendo.

Kumpenda Mungu kuna kuwa ni nguzo au msingi wa mahusiano yako na Mungu wako.

Marko 12 : 30 – “nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.”

Mungu anataka tumpende kwa kiwango cha juu sana kuliko kitu chochote.

Ndio maana kaweka amri ya kumpenda, japo ilitakiwa hii iwe ni tabia ya kawaida kwa watoto wa Mungu.

-          Somo hili litakusaidia kujua namna ya kumpenda Mungu katika kiwango anachokitaka Mungu.

-          Kiwango anachotaka Mungu tumpende si nusu wala robotatu bali ni kwa nguvu zote, akili zote, moyo wote, na roho yote.

Hapa hatuongelei swala la Mungu kumpenda mwanadamu bali tunaongelea mwanadamu kumpenda Mungu.

-          Kuna tofauti kubwa sana kati ya Mungu kumpenda mwanadamu na mwanadamu kumpenda Mungu.

-          Unaweza ukawa unamtumikia Mungu lakini ukawa humpendi huyo Mungu unayemtumikia.

-          Kumtumikia Mungu haimanishi kwamba ndiyo unampenda. Unaweza ukawa ni mtumishi wa Mungu mkubwa tu lakini ukawa humpendi Mungu unayemtumikia.

-          Vita kubwa ambayo shetani anaileta kwa watu wa Mungu si pale wanapomtumikia Mungu bali ni pale wanapoamua kumpenda Mungu wanayemtumikia. Uwe na uhakika shetani atakupiga vita ambavyo hukutegemea.

Wafilipi 3 : 8 – Nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu Bwana wangu …

-          Mtume Paulo anatuambia juu ya kumpenda kwake Yesu kulivyokuwa katika namna ambayo ilimfanya ayahesabu mambo yote kuwa hayana faida kuliko kumpata Yesu.

-          Alimpenda Yesu kwa kila kitu alichokuwa nacho; moyo wake, mwili wake, nguvu zake, akili zake, vyote vilimpenda Yesu.

Biblia inamaanisha nini inaposema “mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote na kwa nguvu zako zote”?

NB: Kupenda ni kuthamini, ni kujali, n.k

Inamaanisha:

i.                    Mshirikishe Mungu kwanza katika kila ufanyalo (kutengeneza ushirika imara na Mungu)

Mithali 19 : 21 – Mna hila nyingi moyoni mwa mtu, bali shauri la Bwana ndilo litakalo simama. (Hila maana yake ni mipango, shauri maana yake ni kusudi au mapenzi ya Mungu)

Mathayo 6 : 33 – Bali utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake …

Maana yake katika kila unachofanya ni lazima utafute kujua kama jambo hilo ni kwa ajili ya mapenzi ya Mungu na si kwa mapenzi ya kwako binafsi. Kabla hakijawa cha kwako ni lazima kiwe cha Mungu kwanza.

Uzito wa hii pointi upo kwenye neno “kwanza”. Tafsiri yake ni kwamba; kuna watu wanafanya maamuzi juu ya mambo Fulani kwenye maishi yao na wanakuja kumjulisha Mungu juu ya kile walichokwisha kukiamua na si kuomba Mungu awasaidie kufanya maamuzi.

-          Mfano: unaweza ukawa umemuona mtu ukampenda na ukataka kumuoa lakini unakuja kumuomba Mungu akusaidie umpate mtu huyo ili umuoe. Tangu ulipoanza kutafuta mwenza wako hukumshirikisha Mungu ili akusaidie umpate mtu sahihi kwa ajili yako lakini ulipomuona Fulani ndipo ukaenda kwa Mungu ukihitaji akupatie huyo.

-          Hapo hujamshirikisha Mungu kwanza bali umefanya maamuzi yako kwanza.

-          Kilichoanza si Mungu kwanza bali ni maamuzi yako kwanza.

Kwa kumshirikisha Mungu kwanza katika kila unachofanya, kunampa Mungu kuwa na nafasi ya kwanza moyoni mwako. Kuwa na ushirika na Mungu ni jambo la muhimu kupita tunavyofikiri.

ii.                   Bila msaada wa Mungu huwezi kufanya jambo lolote kama ikupasavyo kufanya.

Mithali 3 : 5 , 6 – Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote wala usizitegemee akili zako mwenyewe.

-          Maana yake ni kwamba mwanadamu ameumbwa katika Namna ambayo hawezi akafanikiwa pasipo kupata msaada wa Mungu.

-          Akili yako kuna mahali itafika itashindwa kukusaidia. Kinachotakiwa ni wewe kuwekeza akili yako yote kwa Mungu.

-          Neno “kutumaini” maana yake ni kutarajia, au kutegemea

 

iii.                 Muda au mali au mwili wako ulio nao si wako kwa ajili yako bali ni kwa ajili ya Bwana

Warumi 12 : 1,2 – Itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu ya kumpendeza Bwana …

Mithali 3 : 9 – 10 – Mheshimu Bwana kwa mali yako na kwa malimbuko yako yote …

Zaburi 24 : 1 – Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake.

-          Ni muhimu kuelewa kwamba kila kitu alichonacho mwanadamu ni mali ya Mungu. Hata mwili na pumzi uliyonayo si ya kwako bali ni ya Mungu.

-          Kwa hiyo unaweza ukavitumia vitu hivyo vyote alivyokupa Mungu kwa ajili ya Mungu.

-          Wakolosai 1 : 16 – vitu vyote viliumbwa kwa ajili yake na kwa njia yake

-          Unapotoa muda wako kwa ajili ya Mungu inaonyesha kwamba unampenda Mungu

-          Unapotoa mali zako kwa ajili ya Mungu inaonyesha kuwa unampenda Mungu n.k

 

iv.                  

 

Kwa hiyo, kumpenda Mungu ni mfumo tulioumbiwa nao ili tuwe nao, lakini kwa sababu ya dhambi kuingia ulimwenguni tukapoteza hiyo tabia ya kumpenda Mungu na badala yake tukaipenda dunia.

1 Yohana 2 : 15 - 17

-          Dhambi ilichofanya ndani ya moyo wa mtu si tu kuondoa tabia ya kupenda bali ilibadilisha kipaumbele cha kupenda. Badala ya mtu kumpenda Mungu akaanza kuipenda dunia.

-          Vita kubwa aliyonayo shetani juu ya watu a Mungu ni kuhakikisha watu wa Mungu hawampendi Mungu wao wanayemtumikia.

-          Japokuwa kwa nje tunaona wanamtumikia Mungu lakini ukweli ni kwamba hawampendi Mungu wanayemtumikia.

Mathayo 15 : 8 – 9

-          Watu hawa wanamheshimu Mungu kwa midomo yao lakini mioyo yao iko mbali na Mungu wanayemheshimu.

-          Hakuna mahali kwenye Biblia inaposema mpende Bwana Mungu wako kwa midomo yako yote bali imesema umpende Bwana Mungu kwa moyo wako wote.

-          Sasa kwenye hii mistari inaonyesha kwamba mioyo ya watu iko mbali na Mungu wao, japo kwa midomo yao wanaonekana kama wanamtumikia Mungu. Tafsiri yake ni kwamba hawampendi Mungu wao kwa mioyo yao yote japo wanamtumikia.

-          Na zaidi sana ni kwamba, kule kumpenda Mungu kuliko pungua ndani yao kunapelekea kutokumsikiliza tena na badala yake wakaanza kusikiliza sauti za wanadamu wenzao wasisikilize sauti ya Mungu.

 

 

VIASHIRIA (INDICATORS) VINAVYOONYESHA KAMA MTU ANAMPENDA MUNGU WAKE KWA KIWANGO KINACHOHITAJI

i.                    Kushika na kufuata maagizo na maelekezo anayopewa na Mungu (utii wa Neno la Mungu).

Yohana 14 : 15- mkinipenda mtazishika amri zangu.

1 Samweli 15 : 22 – kutii ni bora kuliko dhabihu

Kusikiliza maagizo ya Mungu ni kiashiria kikubwa sana cha kuonyesha kama mtu anampenda Mungu au hampendi.

-          Kwa sababu ukimpenda Mungu basi utamsikiliza na kufuata Neno lake.

-          Zaburi 119 : 11 – moyoni mwangu nimeliweka neno lako nisije nikakutenda dhambi.

-          Hajasema kwamba moyoni unaweka huduma au unaweka watu au wazazi bali amesema kuwa ameweka neno la Mungu maana yake Mungu atakapokuwa anazungumza naye basi atasikia na kutii.

-          Mfano, mtu unayempenda utamsikiliza.

 

ii.                   Ushirika na Mungu wake unazidi kuimarika (intimacy fellowship with God)

Yohana 14 : 15, 16 – 17

-          Hiki ni kiashiri kinachoonyesha kukua kwa ushirika baina yako na Mungu wako

-          Ushirika maana yake ni kuungana,au kuwa na umoja, au kuwa na mahusiano ya ndani zaidi.

-          Watu wenye ushirika mmoja wana tabia ya kuwa na mawasiliano ya karibu katika namna ambayo hadhi ya mahusiano yao ikipungua basi watajua kuwa mahusiano yao yamepungua, na yanahitaji kurekebishwa.

Kutoka 33 : 15 – Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa

-          Musa alikuwa anajua kabisa kwamba ameanza safari ya kuwatoa waisrael utumwani akiwa na mahusiano mazuri na Mungu, lakini sasa inafika mahali Mungu anaamua kumtuma malaika wake badala ya Yeye mwenyewe kwenda pamoja na Musa

-          Na hiyo ilikuwa inamaana kuwa hadhi ya mahusiano baina ya Mungu na Musa ilikuwa imeshuka.

-          Huwezi ukaanza safari na Mungu halafu umalize na malaika. Katika ulimwengu wa roho, hilo ni gap kubwa sana

 

iii.                 Kiwango cha kuwapenda watu wanaomzunguka kitaongezeka.

1 Yohana 4 : 20 – mtu akisema nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo.

-          Kumpenda Mungu ndani yako kutaachilia msukumo na tabia ya kuwapenda wengine bila kujali wanamwabudu Mungu unayemwabudu au la.

-          Kosa moja ambalo wapendwa wengi huwa tunalifanya na huwa tunadhani ni kawaida ni kuwa na uhusiano mzuri na wapendwa wenzetu tu, lakini hao wengine hata kusalimiana nao huwa hatusalimiani.

Mathayo 5 : 43 – 47 – mkiwapenda wanaowapenda ninyi tu mwapata thawabu gani, tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada?

-          Ni muhimu kujua kwamba kipimo cha kumpenda Mungu kinapimwa kwa kuangalia kiwango chako cha kuwapenda wengine. Kwa sababu huwezi kumpenda Mungu usiyemuona halafu mtu unayemuona humpendi.

-          Ndio maana Biblia inasema mpende jirani yako kama nafsi yako.

-          Na jambo la ajabu ni kwamba na Mungu ameweka hata kipimo cha msamaha kitokane na kipimo cha sisi kuwasamehe wengine. Mathayo 6 : 12, 14

NB: Kwa hiyo mtu akija akikuambia kwamba kumpenda Mungu ni kuwachukia watu wengine basi anakudanganya.

-          Ni kweli unaweza usichangamane nao katika shughuli zao lakini haimaanishi uwachukie.

-          Kwa sababu Biblia inatutaadharisha kutokushirikiana nao katika dhambi wala kuwafuata lakini tunatakiwa kuwapenda, kuwaombea na kutafuta kuwa na amani na wao.

 

iv.                 Utoaji

Kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda, mtatwaa sadaka kwake

 
Kutoka 25 : 1 - 2

Kutoka 35 : 5

-          Hakuna upendo usiokuwa na msukumo wa kutoa.

-          Kipindi kile wana wa Israel walikuwa wanasafiri na hawakua na makazi ya kudumu, na Mungu alkuwa akiwtembelea na kuondoka. Lakini alipotaka kuketi katikati yao alitoa utaratibu wa nini kifanyike ili uwepo wake uwe pamoja nao.

-          Ndipo akasema kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda, mtatwaa kwake sadaka.

-          Angalia lile neno “kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda”, kupenda nini? Kupenda uwepo wa Mungu ukae kwake.

-          Hii haikuwa sadaka ya kawaida bali ilikuwa ni sadaka ya kuuleta uwepo wa Mungu ukae katikati ya wana wa Israel.

Yohana 3 : 16 – kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwana wake wa pekee ….

-          Mungu mwenyewe anatufundisha kuwa watoaji, kwa jinsi alivyomtoa Mwana wake wa pekee.

-          Ni kanuni ya kiroho kwamba kupenda kunaendana na kutoa

-          Huwezi ukatoa kama hupendi.

-          Utoaji wa kumpenda Mungu hutoangalia kama unacho au huna. Utakuwa radhi kutoa vyote ulivyonavyo kwa sababu tu unampenda Mungu.

-          Swala la utoaji kwako halitakuwa swala gumu, maana kuna watu wanapotoa sadaka huwa wanaumia mioyo yao sana kana kwamba wanapoteza, na wengine wanatoa tu ili mradi wabarikiwe lakini si kwa sababu wanapenda kutoa.

 

Hebu tuone mifano kadhaa ya watu wanaomtumikia Mungu bila kumpenda Mungu wanayemtumikia.

Mfano 1: Mathayo 7 : 21 – 23

Si kila mtu aniambiaye Bwana Bwana atakayeingia katika ufalme wa mbinguni …

-          Hawa watu walikuwa wanamtumikia Mungu, na cha kushangaza zaidi ni kwamba hata ishara na maajabu vilitendeka kupitia mikono yao, lakini Mungu aliwaambia kuwa siwajui ninyi. Maana yake walikuwa wanamtumikia Mungu bila kuwa na ushirika na Mungu wanayemtumikia.

-          Ni sawa na kutokee wakala “fake” wa kuuza simu za kampuni Fulani ambayo inatengeneza simu halali lakini anayeziuza hizo simu halali si wakala halisi wa hiyo kampuni. Kwa hiyo simu zinazouzwa ni halali, na kampuni inayotengeneza hizo simu ni halali, lakini wakala ni “fake”. Hivyo kampuni haimtambui wakala anayeuza simu hizo japokuwa simu zinazouzwa na huyo wakala ni simu halali za hiyo kampuni.

NB: Mungu anawapenda watu wote. Lakini wale watu wanaompenda Mungu ndiyo hao ambao Mungu anawajua.

Mfano 2: 1 Samweli 15: 23

Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe …

-          Mfalme Sauli aliambiwa na Mungu kwamba nenda kawapige Waamaleki wote wala usiache hai kiumbe chochote, lakini yeye hakuua wanyama walionona, akawaleta ili kuwatoa sadaka kwa Mungu.

-          Alienda kinyume na maagizo aliyopewa na Mungu wake, akafanya aliyoyaona yeye kuwa ni mazuri. Hakujua kuwa “utii ni bora kuliko sadaka”. Kumtii Mungu ni muhimu zaidi kuliko kutoa sadaka asiyokuambia uitoe.

-          Hii inamaanisha kwamba, mfalme Sauli hakutimiza ule mstari unaosema kwamba “Mkinipenda mtazishika amri zangu”. Kwa Sauli huo mstari haukuwepo.

-          Kwa hiyo alikuwa ni mtu anayemtumikia Mungu lakini yuko mbali na Mungu wake. Hana ushirika naye, hasikilizi neno lake n.k.

 

NB: Ni maombi yangu kwako kwamba umfahamu Mungu zaidi na zaidi na zaidi ili uishi kama apendavyo yeye na si kama upendavyo wewe.

-          Ukae katika Neno lake

-          Uyafanye yale yanayompendeza

-          Na umzalie Mungu matunda kwa kila kai njema ndani yako.

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...