MAMBO YALIYOJITOKEZA KATIKA HABARI YA WAPELELEZI WA WANA WA ISRAELI


Hesabu 13 : 1 – 2, 25, 27 – 33; 14 : 1 – 11

Safari ya Wana wa Israeli ilikuwa ni safari ya kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine, ilikuwa ni safari ya kutoka hali Fulani ya maisha (hali ya umasikini na utumwa) na kwenda kwenye hali nyingine nzuri zaidi ya maisha (hali ya utajiri na heshima na uhuru).

Japo bado unaweza ukaitafsiri safari ya wana wa Israeli kama safari kwenda mbinguni kwa sababu ina mambo yanayofanana na yanayotusaidia kwenye safari yetu ya kwenda mbinguni.

Kila hatua waliyokuwa wanaipitia kwenye safari ile ilikuwa ina umuhimu mkubwa sana mbele za Mungu na kwenye maisha yao kwa sababu ilikuwa inaamua waendelee na safari au wasiendelee.

Kuna mambo waliyokuwa wanayafanya amabayo yaliwakwamisha katika safari yao kiasi kwamba waliweza kukaa eneo moja kwa muda mrefu kama adhabu.

-          Na hivyo ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu jinsi ambavyo kuna mambo tunaweza kuyafanya lakini yakapelekea kukwama tusivuke au tusiendelee mbele, na kuna mambo mengine yanaweza yakatufanya tusonge mbele.

Katika hii mistari tuliyoisoma inaeleza habari ya wapelelezi walivyokwenda na kurudi kuipeleleza nchi yao ya ahadi. Lakini cha ajabu ni kwamba taarifa waliyoileta haikuwa nzuri kwao

Sasa haya mambo manne ni mambo ambayo huwa pia yanatokea sana kwenye maisha yetu ya kila siku na pengine yanatukwamisha kutokuendelea mbele

 

MAMBO YALIYOJITOKEZA HAPO:

1.       Taarifa iliyoletwa na wapelelezi ilikuwa ni moja lakini tafsiri ya hiyo taarifa zilikuwa tofauti

Wale watu waliokwenda kuipeleleza nchi walikuwa ni watu 12, kumi kati yao walitafsiri kuwa ile ni nchi ambayo ina watu walio hodari kuliko Waisraeli hivyo hawataweza kupigana nao na kuwashinda.

-          Na kwa sababu hiyo wakatafsiri kuwa ni nchi inayowala watu wake.

-          Ni kweli kwamba ile nchi ilikuwa na watu warefu walioitwa majitu (Wanefili au wana wa Anaki), ni kweli ile nchi ilikuwa na maboma makubwa na maadui zao walikuwa wanakaa kwenye milima amabapo si rahisi sana kuwashinda kwenye vita.

-          Lakini kati yao wapo watu wawili waliotafsiri kuwa hata kama hao watu wana nguvu kuwashinda wao bado Israeli wanaweza kuwashinda.

-          Na hii ndio changamoto watu wengi tuliyonayo pale ambapo tunakabiliana na mazingira magumu huwa tunawahi kutafsiri kushindwa, tunaona ukubwa wa tatizo kabla ya kuona mpenyo wa Kimungu wa kutusaidia kuvuka hapo.

-          Kwenye safari ya maisha yapo mambo mengi tunakutana nayo na tunashindwa kuyavuka kutokana na vile tunavyoyatafsiri.

-          Ukishindwa kutafsiri jambo matokeo yake ni kufanya sawasawa na vile ulivyotafsiri.

-          Kama ulitasiri kuwa mazingira ya kufanya biashara kwamba ni magumu hutapata faida basi ni kweli hutoifanya hiyo biashara lakini ukitafsiri kuwa mazingira ni magumu lakini bado utapata faida basi utafanikiwa.

-          Na ndio maana tunatakiwa tuwe makini na kila habari tunayoletewa, kwa sababu shida haiku kwenye habari unayoletewa bali iko kwenye tafsiri ya hiyo habari.

-          Isaya 53 : 1 – Nani aliyesadiki habari tuliyoileta, mkono wa Bwana amefunuliwa nani?. Hii maana yake ni kwamba mkono wa Bwana anafunuliwa Yule aliyeamini habari za Bwana alizoletewa.

-          Ni muhimu sana kupima kila jambo kwa jicho la rohoni ilikuona kilichobebwa katika kila habari unayoletewa.

-          Katikati ya mazingira magumu wakina Kalebu na Yoshua waliona ushindi wakati wale wengine wote kumi waliona kushindwa. Katikati ya giza nene wao waliona nuru ikiwazukia.

NB: Chukulia mfanao unataka kuanzisha biashara, kigezo kimojawapo ni lazima upate taarifa za kutosha juu ya hiyo biashara kama itakupa faida au la, pia kama soko lake linapatikana kwenye mazingira unayotaka uianzishe, na mambo mengine ya muhimu. Lakini unapokea taarifa kwamba biashara katika eneo hilo ni ngumu hutopata faida lakini ndani yako Mungu ndiye aliyekuambia kwamba nenda kaanzishe biashara eneo hilo. Unachotakiwa ni kumwamini Mungu na sio mazingira unayoyaona.

 

2.       Tafsiri ya jinsi walivyojiona nafsi zao mbele ya adui zao.

Hawa watu kumi wanasema walijiona nafsi zao kama mapanzi na ndivyo wao walivyowaona wao hivyo.

-          Hapa Biblia inatuonyesha kuwa watu hawa walijiona kwa kujilinganisha na mapanzi, wakaenda mbali zaidi kwa kufiri na wale watu waliwaona hivyo.

-          Swali la kujiuliza ni kuwa, nani aliwaambia kuwa watu wale wanawaona wao kuwa kama mapanzi?

-          Kujiona kama mapanzi mbele ya wale watu ni sawa na kujilinganisha uwezo wao kana kwamba panzi anapigana na mtu.

-          Walijiona kama si kitu kabisa, kana kwamba hawana uwezo wowote.

-          Biblia inasema kuwa ajionavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo (Mithali 23 : 7). Maana yake ni kuwa ukijiona wewe ni hodari na shujaa basi utakuwa ni shujaa kweli bali ukijona wewe ni mnyonge na mdhaifu basi utakuwa ni mnyonge na mdhaifu kweli.

-          Kumbuka kuwa nguvu ya utendaji inatoka ndani mwako, inategemea tu kile kiwango unachoamua kukiachilia ili kifanye kazi.

-          Na katika jambo hili la watu wanavyojiona nafsini mwao kumesababisha wakwame maeneo mengi sana bila ya kujua nini cha kufanya.

-          Inawezekana kwamba muda mwingi umekuwa ni mtu wa kusema mimi siwezi tu mimi siwezi tu kwenye kila kitu, na kweli umekuwa huwezi. Na hii si kwa sababu huna uwezo bali ni kwa sababu umejijengea fikra hizo kwamba huwezi.

-          Na jambo baya zaidi ni kwamba macho yanapoona jambo yanapeleka taarifa kwenye ubongo wako na ubongo wako unatoa tafsiri. Sasa kama ubongo wako utatoa tafsiri kwamba jambo Fulani huwezi basi mwili wako wote unapokea amri kwamba jambo Fulani huwezi, hivyo inapelekea kushindwa kufanya mambo mengi tu ambayo kimsingi yapo chini ya uwezo wako lakini akili yako imekataa kuwa huwezi kuyafanya.

-          Mfano mmojawapo ni kwamba wanafunzi wengi wanafeli kwenye masomo yao si kwa sababu hawana akili bali ni kwa sababu wanajiona kuwa hawawezi kufaulu mitihani yao wakijilinganisha na wanafunzi wengine wenye akili kupita wao.

 

3.       Jinsi hofu ilivyoshinda imani yao kinyume na Mungu wao (maana yake hofu iliondoa imani ndani yao)

Kumbuka imani ni kuwa na uhakika wa kile unachokitarajia hivyo hofu inaondoa huo uhakika na kwa sababu hiyo Hofu ni adui mkubwa wa imani.

-          Ndani mwako ukiwa na hofu basi imani inapungua au inakufa kabisa, unakuwa huna imani tena.

-          Wale wana wa Israeli waliposikia habari ile waliingiwa na hofu kubwa sana kiasi kwamba si tu ilishusha imano yao kwa Mungu wao bali pia kilifisha kabisa imani yao kwa Mungu. Ikapelekea waamue kurudi Misri.

-          Hofu iliingia ndani mwao kwa sababu waliona tatizo ni kubwa kuliko Mungu wao anaeweza kuwaokoa na tatizo

-           

4.        Kutokutambua kuwa Ahadi za Bwana ni hakika na kweli

Mungu aliwaahidi kuwa atawatoa kwenye nyumba ya utumwa na kuwapeleka kwenye nchi ijaayo maziwa na asali, na kweli nchi ya Kaanani ilikuwa ni nchi ijaayao maziwa na asali.

-          Wapelelezi wote walithibitisha jambo hilo

-          Nataka tufahamu kwamba Mungu akiahidi anatekeleza kwa sababu Mungu si mwanadamu hata aseme uongo – Hesabu 23 : 19/ 1 Samweli 15 : 29/ Tito 1 : 2

-          Mungu hawezi kusema uongo na wala hana kigeugeu maana yake ni kwamba akisema amesema.

-          Zaburi 138 : 2 – Mungu ameikuza ahadi yake kuliko jina lake.

-          Inapofika mahali unatilia mashaka ahadi za Mungu maana yake unawaza kwamba anaweza akasema uongo.

Ahadi inaleta tumaini au subira. Na ndani ya tumaini kuna uvumilivu. Na uvumilivu unaleta utulivu rohoni. Kwa hiyo hata kama kuna mazingira magumu yoyote utakayopitia bado hayataweza kuondoa ule utulivu ndani yako kwa sababu una uhakika na ahadi za Mungu kwamba ni kweli zitatimia.

Lakini pia tufahamu kuwa ahadi za Mungu zina kanuni zake (terms and conditions).

-          Fahamu ya kwamba ili Mungu attimize ahadi yake huwa anafuatilia vigezo vya hiyo ahadi aliyokuahidia.

Mifano,

-          Mtu akinitumikia Baba atamheshimu – Yohana 12 : 26

-           Utakaposikiliza sauti ya Bwana na kufuata maagizo yake basi utabarikiwa – Kumb 28 : 1 -14

 

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...