MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOKWENDA MBELE ZA MUNGU

 Somo hili litakusaidia kujua mambo ya msingi ya kufanya kabla hujaamua kwenda mbele za Mungu

Zaburi 24 : 3 – 6

-          Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?

-          Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe

-          Asiyeinua nafsi yake kwa ubatili, wala hakuapa kwa hila.

-          Atapokea Baraka kwa Bwana na haki kwa Mungu wa wokovu wake

-          Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao, wakutafutao uso wako, ee Mungu wa Yakobo

Katika mistari hii tunaona kwamba kuna sifa za mtu astahiliye kwenda mbele za Mungu au kusimama patakatifu pa Mungu

Na hivyo vigezo ni kama ifuatavyo:-

1)      Mtu aliye na mikono safi

Biblia inatueleza kwamba kigezo kimojawapo cha kumwona Mungu ni kuwa na mikono safi.

Na hapa ni muhimu ukajifunza kuangalia jambo kutokea rohoni kwanza kuja mwilini.

-          Anaposema mikono safi hamaanishi usafi wa mikono kwa namna ya nje bali usafi wa mikono kwa jinsi ya rohoni.

-          Hapa Biblia inatuonyesha kwamba katika ulimwengu wa kiroho, mikono inaweza ikawa safi au michafu kulingana na kilichofanywa na hiyo mikono.

-          Kwa lugha nyingine ni kwamba ulimwengu war oho unaweka rekodi ya kila kinachofanyika duniani na hasa zaidi kinachohusisha mikono ya mtu.

-          Mikono yako ikishiriki katika kutenda uovu basi ulimwengu wa roho utajua na utaweka kumbukumbu, na hivyo hivyo ukitenda mema.

-          Na kwa sababu hiyo tunapata kutambua hali za kiroho za mikono yetu.

Hili si somo jepesi sana na wala si jipya lakini tunamuomba Mungu kwa njia ya Roho mtakatifu atusaidie akili zetu tuelewe na tupate kile alichokikusudia Mungu tukipate.

Nataka tuone baadhi ya mifano kwenye Bblia inayoonyesha hali za kiroho za mikono yetu:

Mfano 1.             1 Nyakati 22 : 8, & 1 Nyakati 28 : 3  (Mikono kujaa damu)

-          Mfalme Daudi aliambiwa na Mungu kwamba hatomjengea Mungu hekalu kwa sababu mikono yake imejaa damu kwa kuwa amekuwa mtu wa vita vingi.

Isaya 1 : 15 – Nanyi mkunjuapo mikono yenu nitaficha macho yangu nisiwaone, naam mwombapo maombi mengi sitasikia maana mikono yenu imejaa damu.

-          Biblia inatuonyesha jambo la ajabu hapa kwamba unapokwenda kwenye vita na ukamwaga damu, basi hiyo damu inabaki katika mikono yako katika ulimwengu wa kiroho.

-          Na kama hujajua namna ya kushughulika na hali hiyo basi mikono yako itabaki katika hali hiyo siku zote na itakunyima kumuona Mungu kwa kiwango kinachotakiwa. Maana yake ni kwamba Mungu kujifunua kwako kunaweza kukazuiliwa kwa sababu ya hali ya kiroho ya mikono yako ambayo imejaa damu.

-          Mungu alikataa kuwasikiliza waombaji si kwa sababu waombaji wanaomba vibaya bali ni kwa sababu wamekwenda mbele za Mungu angali mikono yao imejaa damu.

-          Pia Mungu alikataa Daudi asimjengee Nyumba (hekalu)si kwababu mahusiano kati ya Daudi na Mungu wake yalikuwa si mazuri bali ni kwa sababu Daudi alikuwa na mikono iliyojaa damu kwa sababu ya vita alivyopigana.

-          Na ukiangalia Daudi alikuwa na nia njema kabisa ya kujenga nyumba ya Mungu lakini kilichomkosesha kibali mbele za Mungu ni mikono yake yenye damu.

-          Kilichokwamisha majibu ya maombi ya hawa watu si kutokuwa na imani, wala maombi yao kuzuiliwa na mkuu wa anga, n.k bali ilikuwa ni mikono yao iliyokuwa imejaa damu ndio ilimfanya Mungu aache kuwasikiliza na kuwajibu.

Mithali 6 : 16 – 18

Katika vitu saba anavyovichukia Bwana kimojawapo ni mikono imwagayo damu isiyo na hatia.

Mfano 2.              Yeremia 44 : 8, Yeremia 25 : 14, & Zaburi 18 : 20, 24 – 26 (Mikono inaweza ikabeba adhabu au baraka)

Biblia inasema Mungu atawalipa kwa kadiri ya matendo yao na kwa kadiri ya kazi ya mikono yao. Na mahali pengine inasema, Bwana amenilipa sawasawa na usafi wa mikono yangu.

-          Kilichobebwa kwenye mikono yako kinaweza kikaathiri hali yako katika ulimwengu wa kimwili. Kwa sababu kama iliyobebwa ni adhabu basi adhabu hiyo itadhihirika mwilini na kama kilichobebwa ni Baraka basi Baraka hiyo itadhihirika mwilini.

 

Baadhi ya mambo yanayohusu mikono yako ambayo chanzo chake ni rohoni lakini yanatokea mwilini

a.       Mikono inaweza ikadhoofika au ikatiwa nguvu

Yeremia 38 : 4 – Mikono kudhoofika

Waamuzi 7 : 11 – Mikono kutiwa nguvu

NB: Kibiblia anapoongelea mikono anamaanisha utendaji kazi. Kwa hiyo utendaji kazi wako unaweza ukadhoofika au ukatiwa nguvu.

-          Mikono yako inaweza ikadhoofishwa au ikatiwa nguvu kutokana na maneno unayosikia.

-          Kwa tafsiri nyingine ni kwamba ni muhimu kuchunga na kuchuja kila unachokisikia kinachokuhusu kwa sababu kinaweza kikaathiri utendaji kazi wako.

-          Watu wengi wameacha huduma na vipaji vyao kwa sababu walisikia maneno juu ya huduma zao na yakadhoofisha huduma hizo.

-          Maneno yanaweza yasiharibu moyo wako lakini yanaweza yakadhoofidha mikono yako kiasi kwamba ukashindwa kufanya uliokusudia kufanya.

-          Wapendwa wengi tunakumbuka kulinda mioyo yetu tu kwa sababu tunalinda imani zetu lakini tunasahau kulinda na mikono yetu isidhoofishwe.

Ezra 6 : 22 – Mungu akawafurahisha kwa kumgeuza moyo mfalme wa Ashuru awaelekee ili awatie nguvu mikono yao katika kazi hiyo ya nyumba ya Mungu .

-          Kwa hiyo Mungu anaweza akaachilia mazingira yatakayotia nguvu mikono yako ili uifanye kazi yake.

 

b.      Mikono ya mtu inaweza ikataabika

Ezekiel 7 : 27 – mikono ya watu wa nchi itataabika.

Kutaabika maana yake ni kuhangaika pasipo kuzalisha matunda yaliyokusudiwa.

-          Mfano wa mtu au watu ambao mikono yao inataabika ni pale unapofanya biashara kwa juhudi na bidii kubwa tu lakini mwisho wa siku huoni faidi uliyoikusudia.

 

c.       Mikono inaweza ikawa na hila.

Isaya 25 : 11

Hila ni mashauri au makusudio au nia.

Mathayo 5 : 30 na Mathayo 18 : 8

 

2)      Mtu aliye na moyo mweupe

Kigezo kingine cha kuweza kumwona Mungu ni kuwa na moyo mweupe au moyo safi.

Kama kuna moyo mweupe au safi basi pia kuna moyo mchafu.

Mathayo 5 : 8 – heri wenye moyo safi maana hao watamuona Bwana

-          Biblia kwenye mistari hii haijaelezea habari ya kumwona Bwana baada ya kufa bali imeelezea habari ya kumuona Mungu kabla ya kufa maana yake katika ulimwengu huu wa mwili.

-          Moyo safi unakupa credit ya kumuona Mungu.

Marko 7 : 20 – 23 haya ni baadhi ya mambo ambayo yanaweza yakachafua moyo wa mtu na yakamzuia asimwone Bwana.

Mithali 6 : 16 – 19 baadhi ya vitu asivyovipenda Bwana ni pamoja na moyo uwazao mawazo mabaya.

-          Na ndio maana Biblia inatutaka tulinde sana mioyo yetu kwa sababu inaweza ikatukwamisha tusimuone Mungu.

-          Kuna mambo hatutaweza kuyapata kutoka kwa Mungu kwa sababu tu mioyo yetu haiko safi.

 

3)      Mtu asiyejiinua nafsi yake kwa ubatili.

Ubatili maana yake ni uongo.

Kujiinua nafsi yako maana yake ni kujiona bora zaidi kupita wengine. Ni kujihesabia haki.

Ezekieli 28 : 1 – 2, 6 – 8, 17 – moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako.

Luka 18 : 10 – 14 ukijikweza utashushwa na ukijishusha utakwezwa.

Kuna aina nyingi za kujiinua:

i.                     Kuna wanaojiinua kwa sababu ya uzuri au hali nzuri ya maisha waliyonayo

ii.                   Pia kuna wanaojiinua kwa sababu ya utakatifu/ uchaji walionao.

Lakini kujiinua kote huku bado Mungu anapakataa. Maana yake ni kwamba Mungu anahitaji unyenyekevu.

 

4)      Mtu asiyeapa kwa hila

Neno linatukataza kuapa kwa namna yoyote ile, ila linatutaka ndio yetu iwe Ndio na siyo yetu iwe Siyo.

Mathayo 5 : 33 – 37 Usiape kabisa.

Hesabu 30 : 2 – kiapo kinaweza kikafunga nafsi yako.

Kumb 23 : 21 – 22

 

NB:  DAMU YA YESU NDIO JIBU LA CHANGAMOTO ZOTE HIZO

Waebrania 10 : 19 – 22

-          Kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu ….

-          Damu ya Yesu pekee ndio inayotustahilisha kuingia mbele za Mungu na kumweleza Mungu haja za mioyo yetu.

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...