SIFA ZA MTU ANAYEMFUATA YESU KRISTO

 DARASA LA WANAOUKULIA WOKOVU

19/03/2023

Mungu ameweka vigezo na masharti juu ya kila anayetaka kumfuata Yesu Kristo

-          Ili uwe mwanafunzi waYesu Kristo ni lazima ufuate vigezo na msharti aliyoyaweka

 

1.      Kujikana mwenyewe na kujitwika msalaba wako

Luka 9 : 23 – 26

Mathayo 10 : 34 – 39

Luka 14 : 25 – 33

 

Mistari hiyo hapo juu inaelezea sifa ya mtu atakaye kumfuata Kristo ya kwamba ni lazima ajikane mwenyewe na aubebe msalaba wake ndipo amfuate Yesu.

-          Kujikana mwenyewe ni kufanya maamuzi ya kuachana na yake mambo ambayo yatakuzuia ushindwe kumfuata Yesu kwa uaminifu.

-          Yanaweza yakawa ni mambo mabaya au yakawa ni mambo yanayoweza yakachukua nafasi ya Mungu ndani ya moyo wako.

-          Mungu anapoona kuna jambo ambalo linaweza likachukua nafasi yake ndani ya moyo wako basi huwa anakuambia mapema kwamba uachane na jambo hilo.

-          Ndio maana kwenye hiyo mistari hapo juu inaonyesha wazi kwamba Yule asiyemchukia baba yake aua mama yake au mke wake au familia yake basi huyo hastahili kuwa mfuasi wa Yesu. Maana yake ni kwamba watu hao unaweza ukawaweka moyoni nao ukawasikiliza wao sana kuliko kumsikiliza Mungu.

-          Mfano: Mungu anaweza akakuagiza uende ukahubiri mahali fulani, lakini mzazi wako akakukataza usiende kuhubiri kutokana na hatari anayohisi inaweza ikatokea juu yako utakapokwenda. Hivyo ikapelekea wewe kumsikiliza sana mzazi wako badala ya kumsikiliza Mungu aliyekutuma kazi hiyo.

Si watu wengi sana wanajua kwamba watu wako wa karibu wanaweza wakakuzuia usiwe mkamilifu mbele za Bwana. Ndio maana anasema katika ile Mathayo 10 : 36 – na adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake.

-          Hapa anaongelea adui ambao wanamkwamisha mtu kuwa mwanafunzi mwaminifu wa Yesu Kristo.

-          Anachomaanisha hapa si kwamba ukawachukie watu wa familia yako kwa sababu wao ni wabaya bali anakupa taadhari ya kwamba watu wanaoweza kukukwamisha wewe usiwe mwanafunzi wa Yesu kwa ukaribu kabisa ni watu wa nyumbani mwako.

-          Familia yako au ndugu zako hawatakiwi kuchukua nafasi ya Mungu ndani ya moyo wako.

-          Mungu anachotaka ni kwamba akiwa anasema na wewe uwe unasikia na kutii, badala ya kuwa unasikia na sauti ya ndugu zako wakikuamulia kuifuata sauti ya Mungu au uipuuzie.

-          Huo ndio unaitwa msalaba wako, kwa maana hutokuwa unapata ushirikiano mzuri na watu wa familia yako au ndugu zako kwa sababu wataona kila wanachokushauri kinyume na yale maagizo ya Mungu huwa hawafanikiwi.

Msalaba tafsiri yake ni mateso au adha au shida. Hivyo kujitwika msalaba wako maana yake ni kukubali kuyabeba mateso yatakayotokea wakati wewe ni mwanafunzi wa Yesu.

Baadhi ya mateso au shida hizo ni kama

-          Kuchukiwa na kukataliwa na ndugu

-          Kutengwa na familia

-          Kutopata msaada kutoka kwa watu ambao ungefikiri wangekusaidia wakati wa uhitaji. n.k

Yote hayo unaweza ukayajumuisha katika sentensi moja nayo ni : kupiga gharama ya wokovu

Biblia inatuambia katika kile kitabu cha Luka 14 : 28 -32 ya kwamba mtu akitaka kujenga mnara ni sharti apige gharama kwanza kabla hajaanza kujenga ili ajue ataweza kujenga au hatoweza kukamilisha ujenzi huo.

Na vivyo hivyo katika kuwa mwanafunzi wa Yesu ni lazima upige gharama kwanza na kujua kwamba unatakiwa kuacha hata vile vitu ulivyokuwa ukivipenda hapo mwanzo ili visije vikakufanya ukashindwa kuwa mwanafunzi mwaminifu wa Yesu Kristo.

Wengi tunataka kuingia kwenye wokovu na mambo yetu ya kale (tabia za zamani) ambayo hayatufaidii kitu tena.

Biblia inaseam kuwa itamfadia nini mtu akiupata ulimwengu wote na kupa hasara ya nafsi yake? Itakufaidia nini wewe kuupata utajiri wote na mali zote halafu roho yako ikaenda kuangamizwa katika jehanamu ya moto?

Hivyo ni lazima kupiga gharama na kujua kuwa kuna mambo ya kuachana nayo hata kama kwa nje tunaona yanatusaidia na yanapendeza.

Biblia inasema katika kile kitabu cha 1 Yohana 2 : 15 – 17 “mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake”

-          Ili umpende Kristo na uwe mwanafunzi wake mzuri ni lazima usiipende dunia wala mambo ya duniani.

 

2.      Kutokupenda mali zaidi ya kumpenda Yesu Kristo.

Mtu ambaye anapenda fedha au mali zaidi ya kumpenda Yesu hafai kuwa mfuasi wa Yesu.

Mathayo 6 : 24

Mathayo 19 : 16 – 22

 

Biblia inasema mtu hawezi akatumikia mabwana wawili (Mungu na mali)

Nataka uone jambo fulani hapa: kwa nini Biblia inasema mabwana wawili ikiwa inamjumuisha mali sawasawa na “bwana”?

-          Jibu lake ni kwamba Mungu akiingia ndani yako, wewe unakuwa mtumishi wa Mungu, lakini pia na mali ikiingia moyoni mwako, unakuwa mtumishi wa hiyo mali. Kwa hiyo mali nayo inakuwa ni bwana wako.

-          Ndio maana Yesu anasema huwezi ukatumikia mabwana wawili kwa sababu wote watataka ufanye kile wanachokuambia.

-          Katika ulmwengu wa roho, fedha au mali ni kiumbe kinachoweza kukutumikisha kama utakipa nafsi moyoni mwako kikutawale.

Kwa hiyo ni lazima ujue namna ya kuepukana na tamaa za mali ili usiwe mtumwa wa mali na badala yake uwe mtumwa wa Kristo.

Mali zilimfanya yule kijana ashindwe kumfuata Yesu.

-          Ndani yake kupenda mali kulizidi kumpenda Yesu hivyo akaamua afuate mali kuliko kumfuata Yesu.

 

Ziko sifa nyingi za mtu anayetakiwa amfuate Kristo, lakini kwa leo tutajifunza hizo mbili tu.

Ubarikiwe.

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...