MASOMO MATANO YA KUJIFUNZA YANAYOTOKANA NA HABARI YA MWANA MPOTEVU

 Luka 15 : 11 – 32

Hii ni habari inayoonyesha baba mmoja aliyekuwa na watoto wawili wa kiume, na mdogo aliamua kuchukua sehemu ya mali inayomwangukia kama urithi wake kutoka kwa babaye.

-          Na kweli tunaona baada ya muda mfupi alichukua mali yake na kuondoka.

Sasa kwenye hii habari kuna mambo kadha ya kujifunza, na hayo mambo nimeamua kuyaita kama masomo kwa sababu yamechanua kwa upana wake.

-          Ni masomo ndani ya somo.

-          Unaweza ukayaelezea kama masomo kamili yanayojitegemea moja moja.

MASOMO YALIYOJITOKEZA NI KAMA IFUATAVYO:

1.      Kustawi kwako kimaisha kunategemea kufuata maelekezo ya Kimungu na maonyo yake

Luka 15 : 13 - … akatapanya mali huko kwa maisha ya uasherati

Mithali 29 : 3 – apendaye hekima humfurahisha babaye bali ashikamanaye na makahaba hutapanya mali

Hekima ni kuwa na ufahamu na ujuzi wa namna ya kuishi ikupasavyo kuishi

-          Pia hekima ni kuwa na ujuzi na ufahamu wa namna ya kufanya jambo Fulani .

-          Hekima inakupa muongozo wa namna jambo fulani linavyotakiwa kufanyika

Mhubiri 7 : 12 – hekima ni ulinzi kama vile fedha ilivyo ulinzi

-          Kuna mambo duniani ambayo huwezi ukayatekeleza na ukafanikiwa kama huna hekima ndani yako.

-          Unaweza ukawa na elimu ya darasani nzuri tu lakini ukawa huna hekima kwa hiyo ukafeli kimaisha .

-          Matumizi sahihi ya fedha au mali uliyonayo hayahitaji sana kwamba ni lazima uwe na elimu ya darasani baliunahitaji kuwa na hekima ya kukusaidia kutumia vizuri mali zako.

-          Biblia inasema asiye na hekima atajishikamanisha na makahaba, na kwa hiyo atatapanya mali

-          Ndio maana watu wengi ambao wana elimu hawajui namna ya kutumia vipato vyao ili kuwafanikisha, kwa sababu kinachokufanikisha si elimu uliyonayo bali nihekima uliyo nayo.

-          Elimu inaweza ikakusaidia kupata fedha bali hekima itakusaidia kujua namna ya kutumia hizo fedha ili ufanikiwe.

-          Kwa hiyo watu wengi wana fedha au wanapata fedha lakini hawana mafanikio. Matumizi sahihi ya fedha yako hayahitaji elimu yako bali yanahitaji hekima.

-          Ukiwa na hekima , hiyo hekima itakulinda kwa sababu hekima ni ulinzi

Biblia inaposema hekima ni ulinzi maana yake ni kwamba hekima itakusaidia kufanya maamuzi sahihi ili usichague kufanya jambo litakalokuangamiza kama vile kujishikamanisha na makahaba.

Yohana 15 : 4, 5, 7

-          Tukiwa nje ya Yesu hatutaweza kufanya jambo lolote tukafanikiwa.

-          Ukikaa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu utapokea maelekezo ya kukufanikisha kimaisha.

Yakobo 3 : 17 – Hekima itokayo juu kwanza ni safi…

Kwa hiyo maisha ya Yule mwana mpotevu yaliharibika si kwa sababu alikuwa maskini bali kwa sababu alikosa hekima.

NB: Na ndio maana unatakiwa umuombe Mungu hekima kwanza ili milango ya fedha inapofunguliwa mbele yako, fedha hizo zisikuangamize.

Kuna watu ambao Mungu hawezi kuwaruhusu wakafanikiwa kwa kuwatajirisha kwa sababu anajua kwamba wakipata fedha tu watapotea na kukengeuka.

 

2.      Ufahamu juu ya kuweka akiba

Akiba ni mali au amana ya sasa inayohifadhiwa kwa ajili ya matumizi ya baadaye (hasa zaidi wakati wa uhitaji)

Luka 15 : 14 – alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia katika nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji.

NB: Kabla hatujaendelea, nataka ufahamu aina mbili za njaa zinazoongelewa hapa:

a.       Njaa iliyokuwa imeingia katika nchi nzima ambayo chanzo chake ni mabadiliko ya hali ya hewa ikasababisha mavuno kukosekana na kupelekea kukosekana kwa chakula ndani ya nchi. Watu wote wanakutana na hiyo njaa

b.       Njaa inayompata mtu baada ya kutumia feha zake zote vibaya kwa sababu hakuweka akiba wala hakufanya maendeleo yoyote kipindi anazo fedha. Hii ni njaa ndani ya njaa

-          Wakati watu wanalia njaa kwenye nchi kwa sababu kuna ukame, wewe unalia njaa kwa sababu hata kama chakula kingekuwepo usingekuwa na fedha ya kununulia chakula.

Mojawapo ya changamoto na uzembe wanaokutana nao wapendwa ni swala la kukosa kuwa na tabia ya kuweka akiba.

-          Mtu mwenye tabia ya kuweka akiba ni mtu anayeiona kesho yake wakati hiyo kesho haijafika.

-          Akiba ni jambo la kiroho kabla halijawa jambo la kiuchumi.

-          Ukitaka kufanikiwa kimaisha basi kati ya mambo ya msingi ya kuzingatia na kufahamu ni namna ya kuweka na kutumia akiba.

Akiba ina muda wake wa kuweka na ina muda wake wa kutumia.

-          Unaweza ukapatia muda wa kuweka akiba lakini ukakosea muda wa kuitumia hiyo akiba.

-          Ndani yako ukiwa na tabia ya kuweka akiba ni lazima tabia ya uvumilivu ijengeke ndani mwako. Kwa sababu kuna wakati utataka kuitumia lakini utajua kuwa matumizi hayo si sahihi kwa wakati huo, hivyo uvumilivu na subira vinahitajika ndani mwako.

-          Akiba ili iwe akiba ni lazima ikusaidie baadae wakati wa uhitaji. Kama akiba haikusaidii baadae basi hiyo si akiba.

Mfano: Yusufu alipoweka akiba ya chakula katika taifa la Misri

Mwanzo 41 : 33 – 36

-          Nchi nzima ya Misri kulikwa hakuna mtu mwenye ufahamu wa kuweka akiba.

-          Akiba ilisaidia nchi ya Misri na nchi za jirani zisiharibiwe kwa njaa

-          Yusufu alikuwa anakusanya sehemu ya tano ya mavuno yaliyovunwa nchi nzima na wananchi wenyewe kila mwaka kwa miaka saba lakini wananchi wenyewe hawakuwa wanaweka akiba.

-          Wananchi walijua kuzalisha chakula lakini hawakujua namna ya kuweka akiba ya chakula.

-          Chakula kile kile alichokikusanya Yusufu wakati wa miaka ya shibe ndicho chakula kile kile alichokuja kuwauzia wananchi kwenye miaka ya njaa. Wananchi walijua namna ya kulima na kuvuna chakula lakini hawakujua namna ya kuweka akiba.

Mithali 6 : 6 – 8 – Ewe mvivu mwendee chungu, zitafakari njia zake ukapate hekima, maana yeye hujiwekea akiba ya chakula wakati wa mavuno.

-          Wanyama au wadudu wanafahamu umuhimu wa kuweka akiba lakini wanadamu wenye akili hawajui kuweka akiba.

NB: Fahamu kuwa swala la luweka akiba ni kanuni mojawapo ya mafanikio basi uwe na uhakika kwamba Shetani atakupiga vita sana kwamba usiweke akiba.

                                Kuna:     -Akiba ya fedha/ mali

                                                -Akiba ya chakula

                                                -Akiba ya maombi

                                                -Akiba ya wema/ kusaidia

 

3.      Kutubu ni kubadilka mtazamo

Toba maana yake ni kubadilika mtazamo. To repent – to change your mindset

Mtu anaposema anatubu juu ya maisha yake ya dhambi aliyokuwa akiishi- maana yake anamua kubadilisha mtazamo wake juu ya maisha yake na kugeuka.

Toba inaanzia kwanza kwenye akili yako.

-          Kama ulikuwa ni mwizi, ukaamua kutubu, maana yake unaanza kubadilisha mtazamo wako wa kutotaka tena kuiba.

-          Ule mtazamo wako wa kutaka kutoendelea kuiba tena ndio tunaita kutubu.

Luka 15 : 17 – alipozingatia moyoni mwake

-          Maana yake alipoamua kubadilika, alitafakari namna ya kurejea kwa baba yake.

-          Alipiga gharama ya maisha anayoishi na maisha ya watumishi wa baba yake wanavyoishi akagundua kuwa anaishi chini ya kiwango lakini akajua kuwa kuna nafasi ipo ya yeye kurejea hata kama atarejea kama mtumishi na si mwana.

Kutubu ni matokeo ya kujutia dhambi ulizofanya au kujutia mfumo wa maisha uliyokuwa ukiishi na kuamua kubadilika uishi tofauti na ulivyokuwa ukiishi awali.

-          Kule kujutia kunakufanya ubadilishe mtazamo wako wa maisha na kuamua kugeuka ili uishi kama vile apendavyo Mungu

Pia kutubu kunakupa kuhesabu gharama ya maisha unayoyaendea.

-          Unapiga gharama ya kwamba zamani nilikuwa ninatumia ujanja ujanja kupata mali au fedha iliyokuwa si halali kwa ajili ya kujikimu lakini sasa ninaokoka kwa hiyo mali ya dhuluma ninaachana nayo,

-          Au ulikuwa ni mtu unayependa kutembea na watu zaidi ya uliyenaye kwenye ndoa lakini unapookoka unaanza kubaki na mmoja tu.

-          Kama ulikuwa ni mtu wa kujipatia mali za haraka haraka unaamua kufanya kazi halali ili ujipatie riziki yako iliyo halali.

Kwa hiyo unapiga gharama ya maisha ili uamue kweli kubadilika. Na unapotubu unajua kabisa kwamba maisha yako bila kuwa na Yesu Kristo kama kiongozi wako hutoweza kufika mbinguni.

Watu wengi wanapokosea na kutenda dhambi huwa hawataki kurudi kuungama dhambi zao na kuomba rehema kwa Mungu bali wengi wanaona aibu

Mithali 28 : 13 – afichaye dhambi zake hatafanikiwa, bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema

-          Mwana mpotevu alipozingatia moyoni mwake aliamua kurudi kwa baba yake na kutubu.

-          Hakuona aibu kwamba ataonekanaje wala hakujali watumishi wa baba yake watamdharau au la bali alinia kurudi na kumuomba msamaha baba yake ili maisha yake yawe salama.

 

4.      Msamaha wa Mungu unakurejesha katika nafasi uliyoipoteza mbele za Mungu.

Fahamu hili, kwamba dhambi inakutoa kwenye nafasi bali msamaha unakurejesha kwenye nafasi.

Luka 15 : 20 – 24 – (22) lakini baba aliwaambia watumwa wake lileteni upesi vazi lililo bora mkamvike, mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni.

i.                    Vazi linawakilisha utambulisho na heshima

Esta 6 : 10 – 11

Kipindi cha zamani hata cha sasa kuna mavazi ambayo ukiyaona utajua tu huyu mtu anacheo kipi. Kwa mfano jeshini, wanajeshi wanatambuana kwa mavazi yao yenye vyeo.

Kwa hiyo mwana mpotevu alivalishwa vazi bora ili atambulike kama mwana na si mtumwa.

ii.                   Pete inawakilisha mamlaka

Mwanzo 41 : 41 – 43

Esta 3 : 10

Esta 8 : 2, 8

Mwana mpotevu alirejeshewa mamlaka aliyokuwa amepoteza wakati alipoondoka katika nyumba hiyo.

iii.                 Viatu vinawakilisha utayari wa kurejea na kuanza maisha mapya. Ndani

Efeso 6 : 15

Amani inaleta utayari

Hivyo mwana mpotevu alipopata amani moyoni mwake kwa sababu ya msamaha kutoka kwa baba yake ndipo akapata utayari wa kuanza maisha hayo kwa upya tena.

NB: Jambo la muhimu la kufahamu hapa ni kwamba msamaha wa Mungu kwenye maisha yetu hautokani na sisi kuomba msamaha bali unatokana na upendo wake Mungu kwetu sisi.

Isaya 43 : 25 – Mimi ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe

-          Hausamehewi kwa sababu umeomba msamaha bali unasamehewa kwa sababu Mungu anakupenda na hataki uangamie.

-          Mungu alitupenda kabla hatujaomba msamaha – Yohana 3 : 16

-          Ndio maana Biblia inasema tunaokolewa kwa neema, maana yake si kwa jitihada zetu wala juhudi zetu bali ni kwa pendo la Mungu mwenyewe. Efeso 2 : 8 – 9

 

5.      Haki ya kuwa mrithi

Kila anayeokoka anafanyika kuwa mrithi kwa Mungu, kwa sababu tumepewa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu, kwa hiyo kama tumefanyika kuwa wana basi tu warithi

Wagalatia 4 : 1 - 7

Anapoongelea mrithi kuwa mtoto haongelei swala la umri bali swala la ukomavu wa akili unaoonyesha kwamba mrithi anauwezo wa kusimamia na kutekeleza majukumu yake.

Katika Israel, walikuwa wanautaratibu wakuhakikisha kijana ni mpaka afikishe miaka 30 ndipo ajulikane kwamba ni kijana mtu mzima anayeweza hata kupewa majukumu ya familia.

-          Chini ya miaka 30 bado ulihesabiwa kama mtoto. Uko chini ya uangalizi wa wazazi.

-          Kwa hiyo hata kama wewe ni mtoto ambaye ni mrithi halali kwa baba yako bado ulikuwa huwezi ukakabidhiwa mali bila kuwa chini ya usaidizi wa mtu mwingine.

Kinacholeta shida si umri bali ni ukomavu wa akili za Yule anayerithi.

Luka 15 : 28 – 31, 12

-          Ndio maana kilimpa shida Yule kijana mkubwa aliposikia ya kwamba mdogo wake amerudi na amefanyiwa sherehe kubwa wakati yeye hajawahi kufanyiwa shrehe yoyote kwa baba yake.

-          Kitu ambacho baba yake alikuwa anajaribu kumuonyesha ni kwamba wewe ndiye mrithi wa haya yote wala hauhitaji kukasirika bali unatakiwa kufurahi.

-          Ni swala la muda tu kwamba bado uko chini ya uangalizi wa baba lakini mali zote izo ni za kwako.

Swala la muda katika kurithi ni swala la muhimu sana kwa sababu anayerithiwa ndiye anayepanga muda wa kurithiwa na sio anayerithi.

Ukirejea katika ile Wagalatia 4 : 2 Biblia inasema ‘bali yu chini ya mawakili na watunzaji hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba’. 

-          Hapa anaongelea swala la muda sahihi wa mtoto kurithi vitu vya baba yake.

-          Mungu anajua ni muda gani sahihi wa kukupa vitu na ni muda gani si sahihi wa kukupa kwa hiyo ni vyma ukaendelea kunyenyekea chini yake mpaka muda alioukusudia yeye mwenyewe.

-          Kuna vitu unaweza ukapewa sasa na vikaharibu uhusiano wako na Mungu, badala ya hivyo vitu vikusaidie na vikufainikishe, vinakurudisha nyuma kiroho.

-          Kumbuka kila jambo lina wakati wake hivyo usitamani upate kitu chochote kabla ya wakati ulioamriwa.

 

HITIMISHO

Ni matumaini yangu kuwa somo hili litakujengea msingi mzuri na kuimarisha mahusiano yako na Mungu.

Sasa utajua kuwa hii habari ya mwana mpotevu si tu habari ya kijana kutaka mali kwa baba yake na kuondoka bali ni habari yenye masomo muhimu ya kujifunza ndani yake.

Unaweza ukawa upo kwenye nafasi ya kijana mdogo aliyechukua mali na kuondoka au ukawa kwenye nafasi ya kijana mkubwa aliyeamua kubaki kuishi kwa baba yake.

-          Kila mmoja alikwama mahali pake lakini Mungu wetu ni wa rehema nyingi ambaye hatuachi tukaangamia.

Bwana Yesu Kristo na akubariki sana.

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...