FAIDA ZA KUSIKILIZA NA KUFUATA MAELEKEZO ANAYOKUPA MUNGU UNAPOOMBA

 Msisitizo wa somo hili ni kujua umuhimu wa kusikiliza na kufuata maelekezo ya Mungu anayokupa Yeye kulingana na hali uliyo nayo.

Biblia inatupa uhakika kwamba tunaoomba chochote kwa mapenzi ya Mungu yeye anajibu. Na pia hakuna lisilowezekana kwake.

Sasa mistari inayotuongoza kwenye hili somo ni Zaburi 32: 8 nayo inasema “Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, nitakushauri jicho langu likikutazama.”

Biblia inatuonyesha kuwa Mungu anaweza akakufundisha na pia anaweza akakuonyesha nini cha kufanya. Sio tu hayo bali pia anaweza akakushauri.

Somo hili linalenga kukuonysha namna ambavyo Mungu huwa anajibu maombi ya watu katika namna tofauti tofauti. Mungu anaweza akakujibu maombi yako sawasawa na vile ulivyomuomba au akakujibu kwa kukupa maelekezo yatakayokusaidia upate kile unachokiomba.

Unajua waombaji wengi wamekosa kuwa na nafasi ya kumsikiliza Mungu anasema nini wanapoomba, au wanapoombea jambo Fulani. Mungu anapenda kuzungumza na watu wake. Hii ni tabia ya kawaida ya Mungu anapojidhihirisha kama Baba kwa watoto wake. Na anataka sio tu wewe uwe unamuomba yeye tu bale na Yeye pia upate nafasi ya kumsikiliza asemapo.

Lakini pia tukumbuke kuwa Mungu huwa anatumia njia tofauti tofauti katika kuzungumza na watu wake. Hii ni kutokana na hadhi ya mausiano baina ya Mungu na mtu binafsi. Kuna wakati Mungu anaweza akaongea nawe kupitia ndoto, maono, neno la maarifa, sauti ya wazi, kupitia mtumishi wake au moja kwa moja kupitia Neno lake unapolisoma.

NB: Ni lazima tukumbuke kuwaa katika kila hali na chochote tunachopitia kuna Neno la Mungu katika hali hiyo.

Yohana 1: 1 – 3 – Vyote vilifanyika kwa huyo, wala pasipo Yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika.

-          Hii inamaanisha kuwa hakuna hali utakayopitia halafu Mungu asiseme na wewe.

-          Ni vile tu kwamba Mungu anasema na wewe lakini huelewi au hujui namna ya kumsikiliza.

Kwa hiyo ni hasara kubwa sana kutosikiliza sauti ya Mungu hata kama unatumia Muda mwingi kuomba kwa sababu Mungu anaweza akakujibu na wewe usitambue kuwa amekujibu. (Prayer is a kind of two ways communication). Tunapoomba mbele za Mungu ni lazima pia tupate nafasi ya kumsikiliza anaposema nasi juu ya yale tunayomuomba.

 

 

 

FAIDA ZA KUSIKILIZA NA KUFUATA MAELEKEZO YA MUNGU

1.      Mungu ataamuru Baraka yake ikujilie au ikufuate.

Kumb 28: 1, 2

Mbaraka wa Mungu ni Zaidi ya mafanikio ya mwanadamu. Unaweza ukafanikiwa kwenye biashara yako kwa mfano lakini usiwe na mbaraka wa Bwana juu ya hiyo biashara.

Kwa nini?

Kwa sababu biashara inaweza ikakupa faida nyingi lakini isikusaidie kukutoa kimaisha. Na ndio maana watu wengi wanafanya kazi za kuajiriw lakini maisha yao ni magumu sana kana kwamba hawana kazi lakini wana kazi. Unaweza ukajiuliza hivi hizo pesa na mishahara yao wanapeleka wapi? Lakini ukweli ni kwamba kazi zao au biashara zao hazina mbaraka wa Mungu ambao ungewafanikisha kimaisha.

Kwenye mbaraka wa Mungu kun ulinzi wa Mungu, Amani ya Mungu, utoshelevu wa Kimungu, uzidisho wa Kimungu na kibali cha Mungu.

 

2.      Unapata uhakika wa ushindi

Waamuzi 7: 1-2, - 7, - 9 –

Gidioni aliandaa jeshi kubwa sana kwa ajili ya kupigana na Wamidiani lakini Mungu alimwambia apunguze jeshi hilo hadi kufikia wat5u 300, na kuna maelekezo alimpa ya nini cha kufanya.

-Mungu akikuahidi kuwa atakupigania ni kweli kwamba atakupigania. Unachotakiwa ni kusikiliza sauti ya Mungu inayokupa maelekezo au mbinu utakayotumia kumshinda adui.

Unaweza ukawa unajua mbinu nyingi sana za kumshinda adui lakini Mungu anataka umsikilize yeye kwa sababu Mungu yeye ni Bwana wa vita, anajua ni mbinu ipi uitumie saa hiyo unapigana kwenye vita yako au kwenye hali yako.

NB: Ni muhimu sana kusikiliza maelekezo ya Mungu anayokupa hata kama ndani mwako unajua kuwa unafahamu namna ya kutoka kwenye shida uliyo nayo.

Haiingii akilini jeshi la watu 300 kupambana na jeshi lenye watu kama mchanga wa ufukweni halafu wategemee kushinda. Ni lazima Mungu mwenyewe ahusike. Njia za Mungu si sawa na njia za mwanadamu, na mawazo ya Mungu si sawa na mawazo ya mwanadamu.

Kwa nini Mungu anataka umsikilize kwanza? Ni kwa sababu anafanya mambo yake yote kwa utukufu wake- yaani anafanya hayo ili ajitwalie utukufu. Kwa hiyo ukifanya chochote ili ujitukuze mwenyewe, utainua vita na Mungu mwenyewe ambayo hakuna anayeweza kukusaidia. (Mungu hampi yeyote utukufu wake).

Pia unaweza ukasoma habari za kuanguka kwa ukuta wa mji wa Yeriko katika Yoshua 6: 1 – 16

 

 

3.      Unapata kufahamu chanzo au asili ya tatizo unaloliombea.

2 Samweli 21: 1 – 2 – 14

Hapa tunaona habari ya Mfalme Daudi katika kipindi chake kulitukia njaa ambayo ilidumu kwa muda wa miaka mitatu, na Biblia inasema ilikuwa mwaka kwa mwaka. Ndipo Daudi akautafuta uso Bwana na Bwana akamjibu.

Biblia haijaweka wazi mfalme Daudi aliomba maombi ya namna gani lakini tunaona kile alichomjibu Bwana. Bwana alimjibu “ni kwa sababu ya Sauli alivyowaua Wagibeoni”.

-          Lile neno “ni kwa sababu ya” linaonyesha kuwa Daudi aliomba kujua chanzo cha ile njaa. Ni sawa na kwamba aliomba “kwa nini njaa imekuja juu ya nchi yake”.

-          Jibu la Munngu kwa Daudi halikuondoa njaa iliyokuwa juu ya nchi bali lilimpa kujua chanzo cha njaa ile au sababu ya kuwepo kwa njaa ile.

-          Kulikuwa hakuna namna yoyote ile ya ile njaa kuondoka isipokuwa kushughulikia chanzo chake.

Wakati mwingine unaweza ukawa unaombea jambo Fulani lakini Mungu akakusemesha kitu tofauti na jambo unaloliombea. Halafu unashangaa.

-          Kumbe Mungu anakuonyesha chanzo cha tatizo lako na halitaondoka mpaka umeshughulika na chanzo hicho.

-          Tusikimbilie tu kukemea tukidhani kila tatizo tunalopitia limesababishwa na Shetani kumbe mengine ni adhabu kutokana na kosa lililofanyika huko nyuma.

Kipindi kile cha Daudi hakukuwa na damu ya Yesu ndio maana iliwabidi walipize kisasi ili kuondoa chanzo cha tatizo la njaa ile lakini sisi tunayo damu ya Yesu inayonena mema kuliko damu za watu, wanyama na hata ndege.

Hebu fikiria Daudi kaka mwaka wa kwanza anaona njaa haiondoki, mwaka wa pili bado tu, unafika mwaka wa tatu ndio anaamua kuutafuta uso wa Bwana.

-          Maana yake ameacha kuomba kwamba Mungu aiondoe njaa bali anaomba kujua chanzo cha njaa ni nini.

-          Usifikiri Biblia inaposema mwaka kwa mwaka kwamba Daudi alikuwa haombi, alikuwa anaomba. Lakini alipoona hakuna mabadiliko yoyote ilibidi abadilishe prayer point.

-          Mwaka wa kwanza Daudi anaomba lakini hatuoni Mungu akijibu chochote na mwaka wa pili vivyo hivyo, lakini mwaka wa tatu Mungu anajibu.

NB: Hebu kaa utafakari ni kitu gani ambacho Mungu amekuwa akikuonyesha au akikusemesha lakini huelewi wala hujui?

-          Kwa sababu wengi wamekwama mahali na hawajasogea mbele kwa muda mrefu wakidhani kuwa Mungu hajawajibu maombi yao kumbe ni wao hawajamsikiliza Mungu kwa makini ili kupata maelekezo ya kufanyia kazi.

Ukishindwa kusikiliza sauti ya Mungu inayosema nawe ndani yako utashindwa kuvuka mahali pa kubwa sana katika viwango vya kumjua Mungu kwenye maisha yako.

 

 

HASARA ZA KUTOISIKILIZA SAUTI YA MUNGU

1.       Kukosa kibali mbele za Mungu.

1 Samweli 15: 1 – 9, 10 -22 – 23

Kumb: utii ni bora kuliko dhabihu.

2.       Kukosa mbaraka wa Mungu

Kumb 28: 15 –

Laana ni kutofikia uwezo wa nguvu zako.

 

NAWEZAJE KUISIKIA SAUTI YA MUNGU?

1.       Jenga na kudumisha mahusiano mazuri na Roho mtakatifu

1Wakorinto 2:10 inasema ‘Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu… vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu’

2.       Ongeza ufahamu wa viashiria (signal) vya mawasiliano kati yako na Mungu

Biblia katika 1Samweli 3:9 inasema   ‘… Enenda, kalale, itakauwa AKIKUITA, utasema, Nena, BWANA; kwa kuwa mtumishi wako anasikia…’ Jambo ninalotaka ulijue hapa ni kwamba Mungu ana njia nyingi za KUITA, naam anaweza kukuita kwa sauti itokayo kinywani pake au KWA NJIA KUKULETEA ALAMA/VIASHIRIA VYENYE KUKUFANYA UJUE MUNGU ANANIITA. Kama ilivyo kwa jinsi ya kibinadamu anayekuita si lazima aongee, anaweza kutumia alama za mikono au hata maandishi nk, kukuita. Katika kukuita kwa njia ya viashiria/alama Mungu anaweza kuleta nguvu/msisimuko/ubaridi/maumivu fulani kwenye sehemu ya mwili wako au huzuni moyoni mwako kama ishara/kiashiria cha uwepo wake juu yako na hivyo KUTAFUTA/KUTAKA USIKIVU WAKO ILI ASEME NAWE. Hivyo ni lazima uwe na ufahamu na utafute kujua kuhusu alama/namna ya kwako ambayo Mungu hutumia kutafuta usikivu wako.

3.       Ni lazima ujue kutofautisha sauti ya Mungu na sauti nyingine

Hili ni muhimu sana kwako kulielewa ili usije ukaipuuza sauti ya Mungu kwa kudhani ni mawazo yako au ni ya Shetani au usije ukatekeleza jambo ukiamini kwamba Mungu amesema nawe kumbe Shetani ndiye alisema nawe. Katika             1 Samweli 3:7 imeandikwa ‘Basi Samweli alikuwa hamjui BWANA bado, na neno la BWANA lilikuwa bado halijafunuliwa kwake’. Andiko hili linatuonyesha makosa aliyofanya kijana Samweli katika kuielewa sauti ya Mungu akiichanganya na babu yake Kuhani Eli. Ni muhimu ukaelewa kwamba Mungu anaweza kusema na wewe hata kama uko katikati ya mkutano wa watu wenye kelele nyingi sana. Hii ni kwa sababu Mungu hatumii mdomo kusema nasi bali anatumia moyo wako kuzungumza. Moyo ndio kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya mtu na Mungu.

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...