Lengo la somo hili ni kukusaidia kujua siri iliyoko kwenye msalaba wa Yesu Kristo na thamani yake kwetu.
1 Wakoritho 1 : 17, 18 – Maana Kristo hakunituma ili
nibatize, bali niihubiri habari njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa
Kristo usije ukabatilika. Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi,
bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.
Thamani ya kitu chochote inapimwa
kwa gharama iliyotumika kukipata hicho kitu. Kama gharama ya kitu ni ndogo basi
na thamani yake ni ndogo; na kama gharama yake ni kubwa basi hata na thamani
yake ni kubwa pia.
Kwa mfano thamani ya watoto ulionao
inaweza kutofautiana kutokana na jinsi ulivyowapata. Yule aliyepata watoto kwa
taabu ataona watoto hao wanathamani kubwa sana kuliko Yule aliyepata watoto kwa
wepesi, hivyo ikakupelekea kumpenda zaidi Yule uliyempata kwa taabu zaidi
kuliko Yule ulimpata kwa urahisi.
Pia ni sawa na thamani ya madini au
vito vya thamani. Dhahabu haiwezi ikawa sawa na shaba kwa sababu upatikanaji wa
dhahabu ni tofauti na upatikanaji wa shaba. Shaba inapatikana kwa wepesi zaidi
kuliko dhahabu.
Hivyo ndivyo ilivyo thamani ya
wokovu wetu, kwa sababu wokovu wetu haukupatikana kirahisi bali ilimbidi Yesu
Kristo aache enzi yake na utukufu wake aliokuwa nao kule mbinguni ili aje afe
kifo cha msalaba kwa ajili ya kutuokoa sisi wanadamu.
Wafilipi 2 : 5 – 8 – Hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kushikamana
nacho, bali akajifanya hana utukufu, akajinyenyekeza akawa mtii hata mauti,
naam, mauti ya msalaba.
Waebrania 12 : 2 – Ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake
aliustahimili msalaba na kuidharau aibu
-
Kwa tafsiri nyingine ni kwamba Yesu aliona kuwa
kuendelea kuwa na utukufu na heshima yake huko mbinguni hakumfai kitu chochote
wakati kazi yake huku duniani inaendelea kuharibika.
-
Kwa hiyo alithaminisha ukombozi wetu na utukufu wake
huko mbinguni akaona ni bora aache enzi na utukufu ili aje duniani kutuokoa
wanadamu tutoke kwenye mikono ya adui Shetani.
-
Haikuwa rahisi kwake lakini kwa sababu aliona thamani
kubwa ya kutuokoa basi ikambidi aje kufa msalabani kwa ajili yetu.
-
Kifo cha msalabani kilikuwa ni kifo cha aibu kubwa
sana na cha kudharaulika sana
Usiutazame msalaba kama mbao mbili
zilizounganishwa pamoja bali utazame msalaba kama ishara ya thamani ya ukombozi
wako katika Kristo Yesu.
Sio kila msalaba unaouona ni
msalaba wa Kristo, kwa sababu Yesu hakusulibiwa peke yake, kulikuwa na watu
wengine ambao hao walikuwa ni wanyang’anyi. Na wote walikuwa wamesulibiwa
msalabani
-
Kwa hiyo usitishike utakapomuona mtu amebeba au amevaa
msalaba
-
Na hata kuhubiri injili, Biblia inatuambia tuhubiri
injili ya Yesu aliyesulibiwa. Hii inamaanisha kuwa kuna watu wanaweza
wakahubiri habari za miujiza na kufanikiwa lakini vyote hivyo visitokane na
msalaba yaani wokovu.
-
Unaweza ukafanikiwa ndani ya wokovu na pia ukafanikiwa
nje ya wokovu
-
Unaweza ukapokea uponyaji ukiwa ndani ya wokovu au
ukaponywa ukiwa nje ya wokovu. Kwa hiyo uwe makini na injili unayoletewa.
Biblia inatuambia kwamba neno la
msalaba kwa wanaopotea ni upuzi bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.
-
Maana ya neno la msalaba ni; ujumbe wa msalaba, au
kilichobebwa kwenye msalaba, au thamani ya msalaba, au siri iliyoko kwenye
msalaba, au kazi iliyofanyika msalabani n.k
-
Kwa lugha nyingine ni kwamba Mungu anataka tuone
msalaba kuwa ni jambo la thamani sana kwetu japokuwa watu wengine wasiojua
thamani hiyo wanapuuzia.
NB: Sasa tambua kuwa kutokujua thamani ya jambo fulani
haibadilishi uthamani wa jambo hilo. Kama wewe ni wa thamani, na sisi hatujui
thamani yako, basi haitabadilisha thamani uliyonayo bali sisi ndio ambao
hatutafaidika na thamni hiyo uliyonayo.
-
Hivyo usipojua thamani ya msalaba haitabadilisha
thamani yake bali wewe ndio hautafaidika na thamani hiyo ya msalaba.
NB: Natamani pia ujue kuwa kazi ya Yesu hapa duniani isingekuwa
na maana yoyote kama asingepitia msalabani. Kwa sababu wako manabii waliotenda
miujiza ambayo ilikaribiana na aliyoitenda Yesu, wapo waliofufua wafu, wapo walioponya
watu, wapo waliofanya ishara kubwa na za ajabu zinazokaribiana na alizofanya
Yesu, lakini utofauti wa Yesu na hao manabii au mitume ulikuwa ni kwenye kazi
ya msalaba. Ni muhimu sana ukafahamu jambo hilo.
-
Yesu asingekufa msalabani basi tungemfananisha na
manabii au mitume wengine.
-
Kwa hiyo msalaba ndio unaomtambulisha Yesu ni nani, na
ndio unaomtofautisha Yesu na watumishi wengine.
-
Injili yetu sio ya Yesu wa kabla ya msalaba bali
injili yetu ni ya Yesu aliyesulibiwa msalabani, akafa na akafufuka.
BAADHI YA MABADILIKO YALIYOTOKEA
KATIKA ULIMWENGU WA ROHO WAKATI DHAMBI ILIPOINGIA ULIMWENGUNI
Inawezekana ukawa unajiuliza ni kwa
nini Yesu alikufa msalabani? Lakini kabla ya kuendelea mbali zaidi ni vizuri
kwanza tukaona mambo yaliyotokea pale katika bustani ya Edeni wakati Adamu na
Hawa walipomuasi Mungu kwa kutoyatii maagizo waliyopewa na Mungu. Baada ya hapo
ndipo utakapojua ni nini msalaba umekuja kufanya.
Na baadhi ya mambo hayo ni:
i.
Mwanadamu alipoteza
nafasi ya kiutawala aliyopewa na Mungu alipoumbwa
Mwanzo 3 : 9 – Mungu akamwita Adam akamwambia uko wapi?
Lile neno “uko wapi” haimaanishi
kuwa Mungu hakuwa anamuona Adamu kama mtu bali hakuwa anamuona Adamu kama
mtawala wa hii dunia. Hakumuona kwenye nafasi yake.
Kazi ya dhambi ni kuharibu uhusiano
wako na Mungu kwanza kabla ya kuleta athari za kimwili.
-
Ndio maana wale wanaofanya dhambi kwa kujifichaficha
wanadhani wako salama kumbe walishapoteza mahusiano yao na Mungu kitambo tu.
Kabla dhambi haijaingia
ulimwenguni, sisi ndio tuliokuwa wakuu wa dunia hii. Ndio maana Mungu
alimwambia Adamu na Hawa kuwa waende wakaitawale dunia, wakatawale samaki wa
baharini, ndege wa angani na kila kinachotambaa juu ya ardhi.
Mwanzo 1 : 26, 28 – Mzae mkaongezeke ili mkatawale ndege wa angani, samaki
wa baharini, na wanyama na nchi yote pia.
-
Hiyo ilikuwa ni nafasi ya kiutawala na kiumiliki
tuliyokuwa nayo juu ya ulimwengu huu.
-
Dunia haikupaswa kututawala sisi bali sisi ndio
tulipaswa tuitawale dunia.
-
Na pia tulikuwa tumepewa utiisho na mamlaka ya kuiamuru
dunia nayo ikatusikiliza.
-
Kuna mambo kwenye maisha haya tunayoishi sasa
hatukutakiwa kuhangaika kabisa kwa sababu yanahitaji uyaamuru ili yatokee
lakini kwa sababu nafasi ya kiutawala hauna basi huwezi ukayaamuru ili yatokee,
hivyo utabaki unahangaika.
Zaburi 8 : 4 – 8 – Umemtawaza juu ya kazi za
mikono yako, umevitia vitu vyote chini ya miguu yake…
Zaburi 82 : 6 – 7 – Mimi nimesema ninyi
miungu, na wana wa Aliye juu…
-
Mwanadamu ndiye aliyeumbwa awe mungu wa dunia hii na
sio shetani, lakini kwa sababu mwanadamu huyo alitenda dhambi ikapelekea kupoteza
ile nafasi ya kuwa mungu au mtawala katika hii dunia.
-
Tulivyopoteza nafasi hiyo ndipo shetani akaichukua
yeye hiyo nafasi, akawa ndiye mungu wa dunia hii.
2 Wakorintho 4 : 4 – mungu wa dunia hii ni
shetani.
ii.
Tulipoteza
uwepo wa Mungu ndani yetu ambayo tafsiri yake ni kufa/mauti
Mungu aliwaambia Adam na Hawa ya
kuwa wakila tunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya hakika watakufa. Mwa 2 : 16 - 17
-
Mauti aliyoiongelea Mungu hapa ilikuwa ni mauti ya
kiroho yaani kupoteza Uwepo wa Mungu kwenye maisha yao. Ni bora ukafa kifo cha
kimwili lakini sio kifo cha kiroho.
-
Kifo cha kimwili ni pale ambapo roho ya mtu inatengana
na mwili wake bali kifo cha kiroho ni pale ambapo mwanadamu anapoteza uwepo wa
Mungu ndani yake. Ndio maana watu ambao hawajaokoka wanaitwa wafu japo bado
wanaishi duniani.
NB: Uwepo wa Mungu ndio uzima ndani ya roho ya mtu, kama hauna
Uwepo wa Mungu ndani yako maana yake roho yako haina uzima. Hicho ndicho kifo
cha kiroho. – Yohana 17 : 3 & 1Yohana 5 : 11 - 12
Huwezi ukamjua Mungu usiyemtumikia,
na Mungu unayemtumikia ndiye unayemjua. Maana yake kuna kuwa na ushirika kati yako
na Mungu.
-
Dhambi inakutenga mbali na uwepo wa Mungu, kwa sababu
Mungu hachangamani na dhambi.
-
Kwa hiyo unatakiwa ujue kuwa unaporuhusu dhambi
kutawala maisha yako basi ujue ni tayari ulishakufa kiroho kwa kuwa uwepo wa
Mungu ulikwisha ondoka ndani yako.
1 Wakorintho 15 : 22
-
Mauti ilipata mlango wa kuingilia duniani kwa njia ya
Adamu, lakini uzima uliletwa na Yesu Kristo
2 Wakorintho 5 : 14 – 15 – Yesu alikufa
kwa ajili ya wote
Kwa sababu
Yesu Kristo ni lango, hivyo kifo chake kiliwakilisha vifo vya watu wote, ili
sisi tusife tena bali tuwe hai kwa sababu kuna aliyekufa kwa niaba yetu.
-
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Adam ambaye naye alikuwa
ni lango ndio maana alipotenda dhambi yeye tulihesabiwa wote tumetenda dhambi.
Uwepo wa
Mungu unapoondoka ndani yako unapoteza ushirika na Mungu. Kwa hiyo unakosa kuwa
na mawasiliano na Mungu.
iii.
Kuanza kwa
kipindi cha utawala wa laana juu ya maisha ya mwanadamu
Kabla ya dhambi kuingia ulimwenguni
hakukuwa na laana. Laana imekuja kama adhabu kutokana na dhambi kuingia duniani.
Mwanzo 3 : 14 – 19 – Mungu anatoa laana kwa nyoka, kwa mwanaume, kwa
mwanamke na kwa ardhi
Swali: Ulishawahi kujiuliza kwa nini ardhi ilaaniwe wakati
aliyetenda kosa ni mtu?
Jibu ni kwamba: mtu ndiye aliyewekwa kuwa mwangalizi wa kila kilichopo
duniani, kwa hiyo kosa lake linaathiri mpaka vile vilivyowekwa chini yake
ikiwemo ardhi. Hiyo ndiyo sheria iliyopo kwenye ulimwengu wa kiroho. Ndio maana
kwa wakati ule ilikuwa kama baba ndiye amefanya kosa linalompasa kuuawa basi
hafi peke yake bali hata familia yake, na mifugo yake na vitu vyake vyote
vinateketezwa, pia watu wanachukuliwa na kuuawa au wanakuwa watumwa. Mfano:
Yoshua 7 : 1 - 26
-
Tafsiri ya karibu ya laana ni kutofikia uwezo wa nguvu
zako. Yaani unazalisha kingi lakini unachopata ni kidogo.
-
Unaweza ukawa unafanya kazi ya kuajiriwa na unapata
mshahara mzuri tu lakini maisha yako hayafanani na hela unayopata. Au unaweza
ukawa unajuhudi na bidii katika kufanya biashara zako na ukafanikiwa kupata
kipato kizuri lakini fedha hizo zinaishia kutibu magonjwa, kulipa madeni, misiba
n.k na wala zisikusaidie kujenga na kuendeleza maisha yako. Hiyo inaitwa laana.
-
Kuna mambo unaweza ukayaona ni ya kawaida kwenye
maisha yako lakini kumbe unatembea chini ya laana.
Ø Nyoka
hakuumbwa ili atembee kwa tumbo na kula mavumbi ya nchi bali laana ilimfanya
awe hivyo alivyo sasa; mwanamke hakuumbwa ili azae kwa uchungu mwingi bali
laana ndio imemfanya awe hivyo; wala
mwanaume hakuumbwa ili ale kwa kuteseka kiasi hicho bali laana ndio imemfanya
awe hivyo alivyo. Kwa hiyo vyote hivyo inaonyesha jinsi laana ilivyobadilisha
mfumo wa maisha ya mtu.
Ø Ni muhimu
ukajua kutofautisha kati ya kutembea katika laana na kutembea katika mapenzi ya
Mungu. Laana sio mapenzi ya Mungu bali ni adhabu kutoka kwa Mungu iliyotokana
na kuasi kwa mwanadamu.
Ø Maisha ya
laana ni maisha ya chini ya kiwango. Mtu unaishi chini ya uwezo uliopewa na
Mungu
Yako mambo mengi ambayo yaliharibika kipindi dhambi inaingia ulimwenguni
lakini leo tumejifunza hayo machache.
KAZI YA MSALABA
Tunapoangalia kazi ya msalaba
tunapata kujua sababu zilizomfanya Bwana Yesu Kristo apite kwenye njia hii ya
msalaba kwa ajili ya kutupatia ukombozi wetu.
a.
Kuleta
ukombozi wa mwanadamu kwa kupitia damu ya thamani ya Yesu Kristo
Yesu Kristo alikufa msalabani kwa
ajili ya dhambi zetu ili tusamehewe dhambi zetu na kuwa watoto wa Mungu aliye
juu. Na ukumbuke kuwa dhambi ilikata mawasiliano kati ya Mungu na Mwanadamu,
kwa sababu mwanadamu alikuwa chini ya utawala wa shetani hivyo ilibidi
akombolewe kutoka huko kwenye ufalme wa giza.
Yohana 3 : 16, - 18 – Mungu alitupenda, akamtoa Mwana
wake wa pekee ili afe kwa ajili yetu
Isaya 53 : 5 – na kwa kupigwa kwake sisi tumepona
Waefeso 1 : 7 & Wakolosai 1 : 13 - 14 – Ukombozi
ni sawa sawa na msamaha wa dhambi
-
Kwa kupitia msalaba tumepokea msamaha wa dhambi ambao
ndio ukombozi wetu.
-
Kazi kubwa moja wapo ya Yesu Kristo kuja duniani ni
kwa ajili ya kutuokoa kutoka kwenye nguvu za giza na kutuingiza kwenye ufalme
wake.
-
Na kwa sababu tulikuwa tumemkosea Mungu ilibidi kwanza
tupokee msamaha wa dhambi zetu ndipo tubadilishwe na kuwa watoto wa Mungu.
-
Damu ya Yesu iliyomwagika pale msalabani ilitosha
kabisa kutufutia makosa yetu yote mbele za Mungu na tukawa wapya kana kwamba ni
kama hatujawahi kutenda dhambi kabisa.
Tulipotenda dhambi, katika
ulimwengu wa roho ni sawa na tuliuzwa kwa shetani, kwa hiyo ilibidi Yesu Kristo
atununue. Na kitu pekee cha thamani kilichotoshea kulipa thamani yetu ilikuwa
ni damu yake pekee ambayo ni damu ya Mungu Baba. – Ufunuo 5 : 9
-
Katika Agano la Kale walitumia damu za wanyama katika
kufunika makosa lakini hazikutosha kufuta makosa ya mwanadamu, kwa hiyo ilibidi
ipatikane damu iliyo bora zaidi ili ifute makosa ya mwanadamu.
-
Hapo ndipo utakapojua ni kwa nini ilimbidi Yesu aje
duniani katika umbo la mwanadamu na auvae mwili wa kibinadamu. Roho haina damu
kama mwili ulivyo na damu. Kwa hiyo ilibidi avae mwili wa kibinadamu lakini asichangamane
damu yake na mwanadamu. Ndio maana alizaliwa kwa uweza wa Roho mtakatifu.
Kilichotafutwa hapo ilikuwa ni tumbo la Bikira Mariam ili kumleta Yesu duniani
na sio Yusufu.
-
Hakukuwa na namna yoyote ya Yesu kutuokoa akiwa yuko
mbinguni, ilimbidi aje duniani ndipo atuokoe.
Hivyo tunapouangalia msalaba wa
Yesu Kristo tunaona ukombozi wetu pale.
b.
Kushughulikia
roho ya mauti iliyokuwa inatawala juu ya mwanadamu
Msalaba ulihusika kuleta uzima
ndani ya mtu kutoka kwenye hali ya mauti aliyokuwa nayo mtu wakati angalipo
kwenye maisha ya dhambi
Waebrania 2 : 14 – 15
Mauti ilipata nguvu juu ya
mwanadamu kwa sababu ya dhambi alizozitenda. Na ndio maana mshahara wa dhambi
ni mauti, kwa kuwa mauti ni matokeo ya dhambi. – Warumi
6 : 23
-
Na lango hili la mauti lilifunguliwa kwa Adamu, hivyo
mauti ikawapata wanadamu wote
-
Kwa sababu hiyo ilimpasa Yesu kama lango, kufa kwa
ajili na kwa niaba ya kila mtu ili kwa kupitia yeye kila mtu awe na uzima. – 1 Wathesalonike 5 : 9 - 10
-
Hivyo Yesu aliihukumu roho ya mauti kwa njia ya mauti
yake pale msalabani.
-
Yesu alitumia mauti kuhukumu mauti. Ni kama vile
ambavyo unaweza ukahukumu sadaka zilizotolewa kwa miungu kwa njia ya kuachilia
sadaka yako mbele za Mungu ili kuhukumu sadaka hizo.
Warumi 6 : 10 – Maana kwa kule kufa kwake aliifia dhambi mara moja
tu, lakini kwa kule kuishi kwake amwishia Mungu.
Kwa kupitia msalaba wa Yesu
tumerejeshewa uzima ambao ni uwepo wa Mungu ndani yetu, kwa kuwa Yesu Kristo
ndiye uzima wetu na anakaa ndani yetu.
c.
Kufuta
sheria za kimwili zilizokuwa zinatawala mioyo yetu kinyume na mapenzi ya Mungu
Kazi nyingine ya msalaba ilikuwa ni
kufuta hati ya mashitaka na sheria za kimwili ambazo zilitawala ndani ya mioyo
ya watu.
Wakolosai 2 : 13 – 16
-
Na kwa kupitia hizo sheria, watu walikuwa wakipingana
na mapenzi ya Mungu, hivyo walikuwa wanafuata mapokeo yao.
-
Kuna mambo ambayo kiuhalisia yaliletwa na torati ya
Musa lakini ilikuwa ni kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Na Yesu Kristo
alipokuja ulimwenguni aliyarekebisha hayo mambo ili tusiishi tena kwa sheria
bali kwa Neno lake.
-
Na watu walikuwa wameziweka moyoni hizo sheria na
mapokeo hayo kuliko kuweka Neno la Mungu
mioyoni mwao. Kwa hiyo ndani ya mioyo yao kulijaa torati lakini haikuwasaidia
kumfahamu Mungu kama Mungu mwenyewe alivyotaka.
Mfano: Mtume Petro alikataa kwenda kuchangamana na wamataifa kwa
sababu aliwaona ni najisi kwa kuwa hawakuwa Wayahudi (kipindi kile ilikuwa
Wayahudi hawachangamani na watu wa mataifa mengine, hata kula nao pamoja
ilikuwa hairuhusiwi). Lakini Mungu alimshurutisha aende kwao kuwahubiria habari
ya wokovu ulio ndani ya Yesu Kristo. Matendo 10 : 1 – 34 – 48.
Wako watu duniani mpaka leo
wanashindwa kumpokea Yesu Kristo katika maisha yao kwa sababu ya mapokeo ya
dini zao na sheria zilizopo kwenye torati, na nyingine ni sheria zinazotokana
na jamii walizopo.
d.
Kuleta utu mpya ndani ya kila mtu atakyempokea Kristo
ili asitumikie dhambi tena
Kazi nyingine ya msalaba ilikuwa ni
kushughulikia mabadiliko ya mtu wa ndani ili maisha yetu ya kimwili yabadilike.
Hali yetu ya kimwili inategemea sana hali yetu ya kiroho. Kama mtu wa ndani
hajabadilika na unasema umeokoka basi kiuhalisia bado hujaokoka.
Kuokoka ni kubadilika. Kubadilika
mtazamo wako, mwenendo wako, n.k. Utu wako wa ndani unafanywa upya. – Waefeso 4 : 22 - 24
Warumi 6 : 5 – 6
Yesu Kristo anapotusamehe dhambi
zetu hatuachi tu tukajiongoza wenyewe bali pia anashugulika na kubadilisha utu
wetu wa ndani ili tusiwe tena watumwa wa dhambi bali tumtumikie Yeye peke yake.
Kwa hiyo mabadiliko ya mtu wa ndani
sio jitihada zako bali ni kazi aliyoifanya Bwana Yesu pale msalabani. Kwa
maneno mengine ni kwamba kufa kwa Yesu pale msalabani sio tu kwa ajili ya
kukuokoa peke yake bali pia na kuubadilisha utu wako wa ndani.
-
Ile kwamba unakataa dhambi sio kwamba ni ujanja wako
bali ni kazi ya msalaba. Kwa hiyo usijisifu, bali mtukuze Mungu.
-
Kwa maneno mengine ni kwamba Yesu alituzaa kwa upya
pale msalabani.
-
Msalabani ndiko tulikopata tabia njema, mawazo mema,
mwenendo mpya, n.k
e.
Kututoa
kwenye vifungo vya laana
Biblia inaeleza ya kwamba Yesu alipokufa
pale msalabani alitutoa kwenye vifungo vya laana vilivyokuwa vimeachiliwa juu
ya maisha yetu kama adhabu ya kuingia kwa dhambi duniani.
Katika historia ya Wayahudi, mtu
anayetundikwa kwenye mti, jambo hilo linatafsiriwa kuwa mtu huyo ni amelaaniwa.
Kumb 21 : 22 – 23 – Aliyetundikwa kwenye mti amelaaniwa na Mungu
Wagalatia 3 : 13, 14 – Yesu akatukomboa kutoka kwenye
laana
2 Wakorintho 5 : 21 – Yeye asiyejua dhambi, alimfanya
kuwa dhambi kwa ajili yetu ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye
Hivyo na Yesu kwa sababu yeye ni
lango, (kama Adamu alivyo kuwa lango) ilimbidi afe kifo cha msalabani kwa ajili
ya kuchukua laana yetu. Maana yake ni kwamba Yeye alibeba laana zetu kwa niaba
yetu, ili baraka ya Mungu kupitia kwa Ibrahimu iwafikie mataifa yote kwa njia
ya imani.
Kwa hiyo Yesu pale msalabani
alishugulikia laana iliyokuwa juu ya kila mtu, na kwa sababu hiyo tumepokea
baraka ya Mungu kupitia kwa Ibrahimu kwa njia ya kumwamini Yesu Kristo. Hivyo
usipomwamini Yesu Kristo na kumpokea kwenye maisha yako huwezi ukaipata hiyo
baraka.
Kwa lugha nyingine ni kuwa ndani ya
msalaba wa Yesu tunapata mafanikio yetu, tunapata afya zetu, tunapata kustawi,
tunapata kuongezeka na kusinga mbele zaidi n.k
Hivyo kuna kiwango cha maisha
ambayo huwezi ukakifikia kama hautompokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha
yako kwa sababu ndani yake ndipo tunapopokea baraka ya Ibrahimu kwa njia ya
imani.
f.
Kuturejeshea
mamlaka ya kiutawala tuliyopoteza
Tulipokuwa tumemuasi Mungu,
tulipoteza nafasi ya kuwa watawala katika ulimwengu huu. Na sasa baada ya Yesu
Kristo kufa msalabani na kutuokoa, tumerejeshwa katika nafasi ya kiutawala
katika ulimwengu huu.
Yohana 1 : 12 – Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika
watoto wa Mungu.
1 Yohana 3 : 1 – Tazameni ni pendo la namna gani alilotupa Baba
kwamba tuitwe wana wa Mungu, na ndivyo tulivyo.
Ufunuo 5 : 10 – ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu
nao wanamiliki juu ya nchi
Kwa hiyo, unapookoka, moja ya jambo
linalofanyika juu yako katika ulimwengu wa roho ni kukurejeshea nafasi uliokuwa
umeipoteza hapo mwanzo ulipomuasi Mungu.
v Kwa nini Mungu anakurejeshea nafasi hiyo?
Ø Kwa sababu, Mungu ni Mfalme wa mbinguni,
hivyo anavyokuja duniani ni lazima akaribishwe na mfalme wa duniani. (mfalme wa
duniani ndio wewe. Ndio maana Yesu anaitwa mfalme wa wafalme – wafalme
wanoongelewa hapa ni watakatifu wa Bwana)
-
Mfalme anakaribishwa na mfalme mwenzake, au raisi
anakaribishwa na rais mwenzake
-
Hivyo ndivyo itifaki ilivyo katika ulimwengu wa kiroho
na wa kimwili pia.
Mathayo 16 : 19 – Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni.
-
Mwenye ufunguo ndiye mwenye mamlaka.
-
Sasa huwezi ukawa na mamlaka kama huna nafasi, hivyo
unapewa kwanza nafsi ndipo unapopewa na mamlaka.
-
Kwa mfano, Rais wa
Tanzania, kinachompa mamlaka aliyonayo sasa ni kwa sababu anayo nafasi ya
urais. Lakini akishastaafu tu kwenye hiyo nafasi basi na mamlaka yake pia
yanaishia hapo. Hatoweza tena kufanya maamuzi juu ya nchi.
-
Kwa hiyo ni wazi kabisa kuwa tulipopoteza nafasi kwa
sababu ya dhambi, tulipoteza pia na mamlaka yaliyotokana na nafasi hiyo.
Shetani anachokifanya ni kukupiga
vita ili akuondoe kwenye nafasi uliyonayo kwa sababu anajua akikuondolea nafasi
uliyonayo popote pale basi hata mamlaka pia itaondoka.
g.
Kuturejeshea
utakatifu na kutupatanisha na Mungu
Wakolosai 1 : 19 – 22
Kipindi kile dhambi ilipoingia
duniani, haikumtenga tu mwanadamu na Mungu bali ilitenga vitu vyote vilivyokuwa
chini ya huyo mwanadamu na Mungu.
-
Kwa hiyo sio tu kwamba uwepo wa Mungu uliondoka kwa
mwanadamu peke yake bali uwepo wa Mungu uliondoka hadi kwenye vitu vya huyo mtu
kama vile ardhi.
-
Hivyo, kwa njia ya msalaba, Yesu alivipatanisha vitu
vyote (ikiwa ni pamoja na mwanadamu) na nafsi yake.
-
Mwanadamu akapata kuwa mtakatifu tena kama Mungu
alivyo mtakatifu.
1 Petro 1 : 15 – 16 – Kwa maana imeandikwa, mtakuwa
watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.
Hivyo, kwa njia ya msalaba tunarejeshewa
utakatifu wa Kimungu na tunapatanishwa naye. Hii inamaana ya kwamba, mahusiano
yanarejea tena baina yetu na Mungu wetu.
Kabla ya msalaba, watu walikuwa
hawawezi kwenda mbele za Mungu moja kwa moja. Ilikuwa ni mpaka wapitie kwa
kuhani mkuu na huyo kuhani mkuu ilikuwa ni lazima atoe sadaka ya kuteketezwa
kwa ajili ya dhambi zake na dhambi za wale anaowaongoza ndipo aende mbele za
Mungu, na tena huingia mara moja kwa mwaka.
Lakini baada ya msalaba, kila mmoja
akaruhusiwa kwenda mbele za Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Damu ya Yesu imetupa
ujasiri huo wa kukaribia patakatifu pa patakatifu.
Ebrania 10 : 19 – 20 – Kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa
damu ya Yesu.
Hapo ndipo utaelewa ni kwa nini
pazia la hekalu lilipasuka wakati Yesu anasulibiwa msalabani. Hiyo ilikuwa ni
ishara kuwa sasa kila mtu anaruhusiwa kwenda mbele za Mungu bila kuwa na
kipingamizi chochote isipokuwa kwa njia ya Damu ya Yesu Kristo tu.
Mathayo 27 : 51 – Pazia la hekalu lilipasuka vipande viwili.
Kutoka 26 : 31 – 35 – historia ya pazia la hekalu lililogawanya kati ya
patakatifu, na patakatifu pa patakatifu
Kwa hiyo neema tuliyonayo sisi
tunaoishi baada ya msalaba wa Yesu Kristo ni kwamba tunao ujasiri wa kumwendea
Mungu moja kwa moja kwa damu ya Yesu Kristo. Hatuhitaji tuchinje kondoo wala
mbuzi wala mnyama yeyote wala tulipe fedha yoyote, kwa sababu Yesu tayari
alishamwaga damu yake msalabani inayoturuhusu kwenda kwa Baba
Kwa kupitia damu ya Yesu tuna uwezo
wa kuwasiliana na ulimwengu wa roho. Hicho ni kitu ambacho waganga na wachawi hawawezi
ila ni mpaka wachinje mnyama au ndege ili wapate damu itakayo waunganisha na
ulimwengu wa roho.
NB: Thamani ya Yesu inatokana na msalaba. Huwezi ukamtenganisha
Yesu na msalaba. Thamani ya jina la Yesu inatokana na utii wake wa kukubali
kufa mauti ya msalaba
Hivyo msalaba, kwa kila
anayemwamini Kristo ni ishara kubwa sana ya maisha yake mapya
No comments:
Post a Comment