UPAKO WA ROHO MT. UNAOKUJIA JUU YAKO ILI KUKUANDAA KWA AJILI YA MAISHA YAKO YA BAADAE

 Msisitizo wa somo hili ni kuweka ndani yako kiu ya kutaka kupata msaada wa Kimungu kwa ajili ya kukufanikisha kwenye malengo uliyo nayo.

Uko upako maalumu ambao tunauita upako wa maandalizi ambao kazi yake kubwa ni kumuandaa mtu kwa ajili ya kufikia au kutimiza kusudi la Mungu alilolibeba kwenye maisha yake.

Inawezekana mtu huyo pia akaw amebeba kipawa cha uongozi ndani yake, hivyo akandaliwa kuwa kiongozi wa baadae kwenye nafasi yoyote ile kama vile uongozi wa kwenye familia, au kanisa au jamii yake au taifa.

Hivyo tambua kwamba Mungu wetu ni wa upendo ndio maana anakupa kipindi cha maandalizi ya kukabiliana na huo msimu mpya unaouendea.

 

1 Samweli 16 : 1 – 11 – 13

Kwenye hii mistari tunaona namna nabii Samweli amekwenda kwenye nyumba ya Yese na kumpaka mafuta Daudi kwa ajili ya kuonyesha kuwa Bwana amemchagua kuja kuwa mfalme wa Israel baada ya mfalme aliyekuwepo wakati huo ambaye ni mfalme Sauli.

-          Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Daudi kupakwa mafuta ili baadae aje kuwa mfalme.

Kumbuka kwamba: Daudi alipakwa mafuta mara tatu:

i.                    Mara ya kwanza: 1 Samweli 16 : 13

ii.                 Mara ya pili:         2 Samweli 2 : 4

iii.               Mara ya tatu:        2 Samweli 5 : 1 – 3

Nataka tuone jambo hapa:

Daudi alipopakwa mafuta ile mara ya pili alikuwa mfalme wa Yuda, na alipopakwa mafuta ile mara ya tatu akawa mfalme juu ya Israel wote, swali linakuja pale alipopakwa mafuta kwa mara ya kwanza ili kuwa ni kwa jili ya nini?

-          Alipopakwa mafuta ile mara ya kwanza Biblia inasema Roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile.

Kwa nini roho ya Bwana ilimjia Daudi siku ile aliyopakwa mafuta kwa mara ya kwanza?

Mithali 29 : 18a – pasipo maono watu huacha kujizuia

-          Lile tukio la Daudi kupakwa mafuta lilimjulisha yeye mwenyewe juu ya kile kitakachotokea baadaye kwenye maisha yake, ya kwamba atakuja kuwa mfalme juu ya Israel. Hayo maono yakaingia moyoni mwake.

-          Sasa ili maono hayo yatimie, ni lazima ujifunze kujizuia. (Kujizuia maana yake ni kufanya unachotakiwa kufanya na kutofanya usichotakiwa kufanya – self control. Kujizuia huko kunaendana na maono uliyobeba)

-          Ndio maana ilibidi Mungu aachilie upako juu yake wa kumsaidia kujizuia.

Na hapo tunaona kabisa ya kwamba tangu amepakwa mafuta ile kwa mara ya kwanza ilipita miaka mingi ndipo akaja kupakwa mafuta mara ya pili na ya tatu kwa ajili ya kuwa mfalme wa Israel.

-          Ukisoma vizuri Biblia utagundua kuwa pale alivyopakwa mafuta kwa mara ya kwanza hakuwa mfalme pale pale bali aliendelea kuchunga kondoo wa baba yake.

1 Samweli 17 : 15

-          Na tunaona pia kwamba roho ya Bwana iliyomjilia Daudi ndiye Yule yule roho ya Bwana iliyomwacha mfalme Sauli

-          Hapo ndipo utajua kuwa Mungu alikuwa anamwandaa Daudi kwa ajili ya uongozi au utumishi uliokuwa mbele yake.

KAZI YA UPAKO WA MAANDALIZI NDANI YA MTU

a.     Kukuandaa kifikra juu ya mabadiliko ya kimazingira ya kazi unayokwenda kukutana nayo

Daudi alikuwa ni mchunga kondoo wa baba yake, hivyo akili yake muda wote ilikuwa inawaza mambo ya kondoo. Haikuwa rahisi sana kwake kubadilika kwa haraka kimtazamo wa kuwa kiongozi juu ya watu.

Kuwa kiongozi ni swala la kubeba jukumu kubwa zaidi kuliko kuwa mchunga kondoo. Ilibidi Mungu aingilie kati kwa kuachilia upako juu yake ambao utamsaidia kubadilisha mtazamo wake.

Zaburi 78 : 70 – 72 “akamchagua Daudi mtumishi wake, akamwondoa katika mazizi ya kondoo …., akamweka ili awachunge wana wa Israel. ”

Kwa hiyo upako uliokuja juu ya Daudi ulimsaidia kubadilisha mtazamo wa kuchunga kondoo na kwenda kuchunga wana wa Israel.

-          Mungu alikuwa anajua huyu mtu anahitaji msaada wa kufanya maandalizi mapema ili aweze kusimama katika nafasi yake kwa uaminifu.

-          Mabadiliko ya nyakati au msimu kwenye maisha yako yanahitaji sana mabadiliko kwenye fikra na sio kwenye roho. Hii ni kwa sababu eneo la maamuzi ndani yako sio rohoni mwako bali ni kwenye akili yako.

-          Mchakato wa kumbadilisha Daudi kifikra ulihitaji masaada wa nguvu za Roho Mtakatifu ndio maana akapakwa mafuta mapema sana wakati mfalme aliyekuwa anatawala bado yuko madarakani.

-          Mungu anajua kabisa kuwa unahitaji msaada katika hatua hiyo ya mabadiliko ndio maana anaachilia upako huo wa maandalizi ndani yako mapema ili ukuandae kwa hatua hiyo.

Kimsingi ni kwamba pale tu Daudi alipopakwa mafuta ili kuwa mfalme basi Yule mfalme aliyekuwepo madarakani hakuwa na kazi tena. Ni sawa na kumchagua rais mwingine wakati kuna rais aliyepo madarakani.

-          Lakini Mungu aliamua Daudi aendelee kujifunza na kujijenga kifikra juu ya nafasi ya kuwa mfalme wa Israel.

-          Upako wa Roho Mt juu yake ulihakikisha Daudi anafahamu maswala ya kiuongozi ya kitaifa ambayo ni tofauti na kuchunga kondoo ndio maana ilibidi Mungu amtengenezee njia ya kwenda ikulu kwa mfalme Sauli mara kwa mara.

Vijana wengi wana imani juu ya Mungu wao kuwa anaweza akawafanikisha na kufikia katika malengo yao lakini mitazamo yao bado haijawa tayari kukabiliana na mazingira hayo.

-          Na ndio maana ni rahisi sana kwao kuachia safari njiani pale wanapokutana na changamoto ngumu wakati wakielekea kutimiza ndoto zao au maono yao.

 

b.     Kushughulikia hofu inayokukwamisha kuingia msimu mpya

Mtu anaweza akawa na hofu ya kufanya jambo fulani  jipya au hofu ya kuingia msimu mpya  hivyo ukakwama kuona mabadiliko kwenye maisha yako.

1 Samweli 17 : 1 – 2, 8 – 11, 31 – 37

Jambo la ajabu hapa ni kwamba hivi vita vya Israeli na Wafilisti vilitokea baada ya Daudi kupakwa mafuta ile mara ya kwanza.

-          Kila mtu kwenye taifa la Israel aliogopa kwenda kupigana na Goliathi hata mfalme Sauli aliogopa, hata majemedari wa vita pia waliogopa kwenda kupigana na Goliathi isipokuwa Daudi peke yake ndiye aliyekuwa na ujasiri wa kwenda kupigana.

-          Hivi vita vinatokea mara baada ya Daudi kupakwa mafuta. Na hii ni wazi kwamba hata Daudi mwenyewe angeogopa kwenda kupigana na Yule Goliathi, lakini kwa sababu upako wa RohoMtakatifu ulikuwa juu yake basi akapokea nguvu na ujasiri wa kwenda kupigana na Yule Mfilisti.

-          Hicho ndicho kilichomtofautisha Daudi na wana wa Israel wote, ya kwamba yeye peke yake hakuwa muoga wa kwenda kupigana na Goliathi.

Kile kitabu cha Matendo 1 : 8 – “mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu”

Wale mitume wa Bwana Yesu kabla hawajampokea Roho Mt walikuwa hawana ujasiri wa kwenda kuhubiri Neno la Mungu kwa watu, lakini baada ya kupokea nguvu juu yao wakapata ujasiri, hawakuogopa tena hata kama wangepitia mateso na kuuawa.

-          Kwa hiyo hata kile kipindi cha Daudi alipopakwa mafuta, alipokea nguvu za Roho Mt juu yake zilizoshughulikia hofu ndani yake ambapo hizo nguvu hazikuwepo kwa Mwisrael yeyote wa kipindi kile ndio maana bado Waisrael walikuwa na hofu ya kwenda kupigana na Goliathi lakini Daudi peke yake akawa na ujasiri.

-          Na ukumbuke pia ya kwamba Roho ya Bwana iliyomwacha mfalme Sauli ndiye Roho Yule yule aliyekuja juu ya Daudi, hivyo ujasiri ukatoka ndani ya Sauli ukaenda kwa Daudi.

Na hivi ndivyo ilivyo hata katika maisha ya vijana wengi wa sasa, wameshindwa kusonga mbele kwa sababu ya hofu iliyopo ndani yao ya kujaribu kuanza biashara, au hofu ya kuwa viongozi, hofu ya kusimamia misimamo ya mipango waliyonayo, na hata wengine wana hofu ya kuoa au kuolewa wakiogopa wenzi wao wanaweza wakawaumiza kwa kuwaacha au kuwatenda vibaya.

-          Hofu ni mojawapo ya silaha kubwa ya Shetani anayoitumia kuwapigia watumishi wa Mungu na hasa vijana ili wasifanikishe malengo waliyonayo.

-          Hofu ikiwepo ndani yako basi ujue kuwa imani haipo. Ndio maana waoga watakwenda motoni kwa sababu uoga/hofu inaitoa nje imani.

-          Wengine wameshindwa kuanzisha hata biashara kwa sababu ya kuogopa kupata hasara

-          Kwa hiyo, kuanzia sasa usiruhu hofu ikatawala ndani yako.

Upako wa Roho Mtakatifu juu yako utashughulikia kuondoa hofu hiyo ndani yako.

 

c.      Kukusaidia kuchagua aina ya marafiki au washauri watakaoendana na maono uliyobeba

1 Samweli 18 : 1 – 5

“roho ya Yonathani ikaambatana na roho ya Daudi”

-          Mungu aliamua kumtengenezea Daudi aina ya marafiki ambao wangemsaidia kufikia malengo au maono aliyokuwa nayo.

-          Tunajua ya kuwa Daudi alikuwa na marafiki wengi alipokuwa anakaa kwa baba yake lakini hatuoni wakitajwa hata mmoja, sasa haimaanishi walikuwa ni wabaya bali inawezekana walikuwa hawana cha kumsaidia kufikia kwenye malengo aliyokuwa nayo. Na ndio maana Mungu aliamua kumkutanisha na marafiki wengine watakaomsaidia kufikia hatima yake (wakina Yonathani na watu wa vita wa mfalme Sauli)

Kuna hatua kwenye maisha yako utafika ambapo Mungu hatokuruhusu uendelee kuwa na aina ya marafiki ulionao, sio kwa sababu Mungu amewachukia bali ni kwa sababu hawawezi kukusaidia kufikia maono uliyo nayo

-          Sio kila mtu utakayekutana naye anafaa kuwa rafiki yako. Wengine wataletwa na shetani kwa ajili ya kuua maono yako. Hawana mawazo ya kukusaidia bali wanakupa ushauri wa kukukandamiza ili ujione kuwa huwezi kitu.

Linapofika swala la kuchagua marafiki utakaoambatana nao sio swala la kwako kuchagua bali ni la Mungu kukusaidia kutambua aina ya marafiki wa kuwa nawe.

-          Urafiki ni jambo la kiroho kabla ya kuwa la kimwili. 1 Samweli 18: 1 - inasema “roho ya Yonathani iliambatana na roho ya Daudi”

-          Tafsiri yake ni kwamba, roho zao ziliungana kwa sababu zilipatana na kupendana.

-          Kwa hiyo urafiki wao, msingi wake haukuwa mwilini bali rohoni.

-          Na ndio maana watu wengi ni rahisi sana kuumizwa na marafiki zao, au ni rahisi sana kuwaamini marafiki zao kutokana na misingi ya urafiki wao ambao ni rohoni.

-          Hivyo ni muhimu sana kumshirikisha Mungu kwanza kabla hatujachagua marafiki kwenye maisha yetu.

Wagalatia 2 : 9 – mtume Paulo alipewa mkono wa shirika na wale mitume wakubwa.

-          Maana yake ni kwamba walimpa support kwenye huduma yake.

-          Kuna watu Mungu atakukutanisha nao ili wakupe mkono wa shirika. Japo kuna watu wengine yamkini hata watumishi wa Mungu utakutana nao lakini watakupinga, hawatakupa mkono wa shirika.

 

d.     Kukusaidia kuwa na utulivu moyoni mwako pindi utakapopita katika mazingira magumu.

Hakuna anayezoea au anayependa kupitia mazingira magumu kwenye maisha yake.  Lakini inapotokea ukapita kwenye mazingira hayo magumu kwa ajili ya kule unapoelekea basi ni wazi kabisa kuwa Mungu anahitaji uwe na utulivu moyoni mwako ili umsikilize Yeye akuongoze namna ya kuvuka kwenye hayo mazingira bila kutegemea akili zako mwenyewe.

-          Vijana wengi tunakwama njiani inapotokea tunapitia mazingira magumu kwa sababu tunadhani mazingira yote magumu tunayoyapitia yameletwa na adui shetani, kwa hiyo tunashughulika nayo zaidi kwa kutumia akili zetu pekee bila kumshirikisha Mungu kwanza.

-          Upako wa maandalizi unakusaidia kutulia na kumwacha Mungu mwenyewe akupiganie.

-          Na ndio maana mara nyingi unapopita kwenye changamoto kama hizo unajikuta unaomba halafu badala Mungu kushughulika na tatizo lako, Yeye anashughulika na hali ya moyo wako. Kwa sababu hali ya moyo wako ni ya muhimu sana kukaa sawa katika kipindi hicho cha maandalizi ili kumruhusu Mungu kukuvusha katika mazingira hayo.

 

Zaburi 77 : 1 – 13

Hayo ni maombi ya Daudi wakati ule anapitia katika hali ngumu ya kumkimbia mfalme Sauli.

-          Upako uliokuwa juu ya Daudi haukumbadilishia mazingira aliyokuwa anayapitia bali ulimbadilisha hali ya moyo wake anavyojitazama; yaani nguvu za Mungu zilimbadilisha namna anavyomuona Mungu.

NB: Inawezekana unapita mahali pagumu zaidi, na Mungu anajua kuwa unapita mahali pagumu lakini Mungu anashughulika na hali ya moyo wako na sio mazingira unayopitia kwa sababu anajua mpango alionao kwa ajili yako ni mpango wa kukufanikisha na sio wakukukwamisha. Yeremia 29 : 11

Katika kukupa utulivu moyoni mwako ni lazima upako huo wa maandalizi utashughulikia tabia ya kusamehe ndani yako.

-          Ndani ya moyo wako kama ni vigumu kumsamehe mtu aliyekukosea basi Mungu atashughulikia hali hiyo kwa sababu kutokusamehe ni kikwazo kimojawapo cha kuwakwamisha watu wasifikie malengo yao.

-          Kutokusamehe kunamfanya mtu aache “ku-focus” kwenye malengo yake na badala yake huyo mtu anaanza “ku-focus” namna ya kulipiza kisasi juu ya watu waliomkosea.

Katika kila hali unayopitia liko Neno la Bwana la kukusaidia kuvuka hapo, kwa hiyo ni muhimu sana kukawa na utulivu moyoni mwako ili uweze kusikia kile atakachokuambia Yesu ili ukifanye.

Biblia inasema Imani chanzo chake ni kusikia, kusikia Neno la Kristo, hivyo ili uwe na imani ya kushinda magumu unayopitia ni lazima ujifunze kusikia kwanza Neno la Kristo ndipo imani ijengeke ndani mwako.

 

MUNGU AKUJALIE KUWEZA KUISHI KWA KUTIMIZA KUSUDI LAKE.

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...