KUIFAHAMU NA KUITUMIA NAFASI YA KIKUHANI ANAYOPEWA MTU ANAPOOKOKA

 Msisitizo wa somo hili ni kuandaa wanamaombi watakao simama sawasawa katika nafasi zao za maombi.

Utangulizi:

Mtu unapookoka unapata kurejeshwa kwenye nafasi au mamlaka uliyokuwa umeipoteza hapo awali. Baadhi ya nafasi hizo ni pamoja na unakuwa mtoto wa Mungu, kuhani kwa Mungu, mtenda kazi pamoja na Mungu, raia wa ufalme wa Mungu, n.k.

Yohana 1 : 12 – Wote waliompokea  aliwapa uwezo wa kufanyika kuwa wana wa Mungu

Ufunuo 5 : 9 Ukamnunulia Mungu kwa damu yako… ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu.

Usije ukaidharau hii nafasi kwa sababu kupatikana kwake ni kutokana na damu ya Yesu.

Nafasi ya kikuhani ni nafasi ya kimaombi. Kwa hiyo kama Mungu ameturejeshea nafasi hiyo basi ni dhahiri kuwa anataka tuitumie, na kwa sababu hiyo ni ya muhimu kuifahamu ili tuitumie vizuri.

 

Sasa leo nataka tuangalie nafasi ya kikuhani ndani ya watu wa Mungu.

-          Kuhani ni nafasi anayopewa mtu anapookoka, ili aende mbele za Mungu kwa ajili ya kuomba juu ya nafsi yake na kwa ajili ya wengine. Waebrania 5 : 1 - 4

-          Ni nafasi tuliyorejeshewa kwa njia ya Damu ya Yesu iliyomwagika pale msalabani. Ufunuo 5 : 9

-          Pale msalabani si tu kwamba tulikombolewa kutoka kwenye hali ya utumwa wa dhambi bali pia tulirejeshewa nafasi tulizokuwa tumepoteza tangu mwanadamu alipomwasi Mungu.

-          Na kupotea kwa hizo nafasi ndani ya mwanadamu mbele za Mungu zilikwamisha kwa kiwango kikubwa mahusiano baina ya Mungu na mwanadamu.

-          Ukumbuke kuwa pale tu mwanadamu alipomwasi Mungu automatically mwanadamu alipoteza nafasi zote alizokuwa nazo mbele za Mungu (ndio maana Mungu alimuuliza Adamu “uko wapi” [Mwanzo 3 : 9] sio kwamba alikuwa hamuoni Adamu bali hakumuona kwenye nafasi aliyokuwa amemweka).

Nafasi ndio inayokupa hadhi (heshima) pale unapoitumia.

-          Maneno utakayoongea ukiwa na nafasi ya urais hayana hadhi sawa na ukiyaongea maneno yale yale ukiwa nje na nafasi hiyo ya urais.

-          Kinachompa nguvu rais si yeye kama mtu bali ni cheo cha urais alichonacho kwa wakati ule. Muda ukiisha wa yeye kuwa rais anabaki kuwa ni mtu yule yule lakini hana tena nafasi ya urais, kwa hiyo nguvu inayotokana na nafasi ya urais pia inaondoka. Kwa mfano: rais mstaafu Kikwete akiongea sasa juu ya nchi, maneno yake hayana nguvu sawa na kipindi kile alipokuwa ni raisi wa nchi, sio kwa sababu tumemdharau bali ni kwa sababu hayuko tena katika kiti cha urais.

-          Sio watu wengi wanafuatilia pale rais mpya anapoapishwa halafu unaona mlinzi wa rais anahama kutoka kwa rais anayemaliza muda wake na anakwenda kwa rais aliyeingia madarakani. Hii inaonyesha kuwa mamlaka yamehama kutoka kwa rais aliyemaliza kuja kwa rais mpya.

-          Kinacholeta heshima na uzito wa maneno si mtu bali ni cheo au nafasi.

-          Kwa hiyo ukiwa unajua kuitumia vizuri nafasi yako ya kikuhani basi utaona mambo makubwa Mungu atakayotenda kwa kupitia maombi yako.

Historia fupi ya nafsi ya kikuhani juu ya taifa la Israeli.

-          Kipindi cha torati ya Musa kulikuwa na utaratibu wa kwamba ni lazima Kuhani mkuu tu ndiye mwenye ruhusa ya kuingia patakatifu kwa ajili ya kupeleka dhambi zake mwenyewe na dhambi za taifa zima. Na ilikuwa ni desturi ya jambo hilo kufanyika kila mwaka mara moja tu. Kutoka 26 : 31 – 33 na Waebrania 9 : 25.

-          Kipindi cha neema hasa kuanzia pale kusulubishwa kwa Yesu msalabani kulileta mabadiliko ya utaratibu wa kupaingia patakatifu pa patakatifu. Wakati yesu anasulubiwa kulitokea kupasuka kwa pazia la hekalu, hii ilikuwa ni kuashiria kwamba sasa kila mtu anayofursa na nafasi ya kwenye mbele za Mungu moja kwa moja kwa njia ya damu ya Yesu. Luka 23 : 45 na Waebrania 10 : 19 – 22

Kwa hiyo ni haki ya kila mtu aliyeokoka kwenda mbele za Mungu kama kuhani na kuomba chochote.

NB: Unapokwenda mbele za Mungu kama Mwana utasikilizwa kama Mwana, na utakapokwenda mbele za Mungu kama kuhani utasikilizwa kama kuhani. Ebrania 5 : 7 - 8

-          Mwana ni mrithi wa yote lakini Kuhani ni mpole na mtiifu.

-          Mwana ni mtawala bali kuhani ni muombaji, mnyenyekevu anayejua kushuka na kutii.

-          Ni muhimu ukajua unakwenda kwa nafasi gani mbele za Mungu. Kwa sababu ile nafasi ndio inayotoa uzito wa hayo maombi unayoomba mbele za Mungu.

Hebu fikiria kwa mfano; raisi wa nchi Fulani anapokuja hapa nchini kwetu atapokelewa na mwenyeji wake ambaye ni raisi wa nchi yetu, na hivyo hivyo akija Waziri wa nchi nyingine hapa ni lazima atapokelewa na waziri wa hapa nchini kwetu. Kinachosababisha hali hiyo ni hadhi ya nafasi walizo nazo.

-          Nguvu za sauti zao zipo kwenye nafasi zao

-          Yesu alipoomba juu ya kifo chake na namna ya kuwakomboa wanadamu, hakwenda mbele za Mungu Baba kama Mwana bali alikwenda kama Kuhani mkuu na ndio maana alibeba dhambi zetu pale msalabani.

-          Pale kwenye kitabu cha Waebrania 5 anaposema ”akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu, na ingawa ni Mwana alijifunza kutii kwa mateso”= hii inaonyesha kwamba nafasi aliyokwenda nayo Yesu mbele za Mungu si Mwana bali Kuhani mkuu. Nafasi ya Kikuhani inakupa uhalali wa kubeba dhambi za wengine na kuzipeleka mbele za Mungu.

 

Lakini pia ndani ya hii nafasi ya kikuhani kuna jambo jingine la kufahamu ambalo ni la msingi sana.

ü  Ufunuo 5 : 10Ukawafanya kuwa ufalme na makuhani

-          Hapa Yesu Kristo alifanya nafasi ya ufalme kama “taifa” na nafasi ya makuhani kama “ waombaji”

 

ü  1 Petro 2 : 9Ukuhani wa kifalme

-          Nchi zinazoongozwa na wafalme, hao wafalme neno lao ndio sheria, maana yake wanatoa maamuzi kwa maneno yao.

-          Kwa hiyo ukuhani wa kifalme ni waombaji wanaoweza kutoa maamuzi kwa njia ya maneno wanayotamka wanapoomba.

-          Hivyo neno la mwanamaombi huyo ndio linakuwa na maamuzi ya mwisho (final say) juu ya mahali pale unapopaombea.

-          Ukiamua paharibike basi pataharibika na ukiamua parekebishwe basi patarekebishwa. Mfano : Ibrahimu alipopata nafasi ya kuombea miji ya Sodoma na Gomora – Mwanzo 18: 23 – 33

Wafalme wanatawala kwa maneno bali makuhani wanatawala kwa maombi.

 

ü  Kutoka 19 : 5 – 6Ufalme wa makuhani

-          Tafsiri yake ni kwamba Mungu aliamua ajitengenezee taifa ambao watakuwa ni waombaji. Ndio maana kila mtu anayeokoka automatically anakuwa ni kuhani katika ufalme wa Mungu.

Kwa hiyo fahamu kuwa nafasi ya ukuhani ni nafasi ambayo ilikuwepo kwenye mpango wa Mungu wa kumwokoa mwanadamu kwa kupitia damu ya Yesu hivyo ina thamani kubwa sana kama tutajua namna ya kuitumia ipasavyo.

Maombi ni sawa na chakula cha kiroho kwa mtu yeyote aliyeokoka, hayaepukiki.

-          Ukitaka kuwa na mahusiano mazuri na Mungu wako ni lazima uwe na tabia ya maombi maishani mwako.

-          Maombi yanajenga mahusiano mazuri kati yako na Mungu.

-          Maombi ni mojawapo ya njia anayotumia Mungu kuzungumza na watu wake na pia ni njia anayotumia mtu kuwasiliana na Mungu wake.

-          Lakini pia maombi ni njia mojawapo ya kutawala katika ulimwengu wa roho (Ufunuo 5 : 10 – “nao wanamiliki juu ya nchi”).

 

Kuna aina mbali mbali za waombaji ambao Mungu amewaweka hapa duniani.

1.       Waombaji walinzi

Isaya 62 : 6 – 7 – tazama nimeweka walinzi juu ya kuta zako ee Yerusalemu hawatanyamaza usiku wala mchana…

Hawa ni waombaji wenye kazi ya kulinda kusudi la Mungu juu ya mahali Fulani wanapopaombea.

-          Wamesimama kama walinzi. Wao ndio wanaoruhusu jambo Fulani lipite au lisipite katika ulimwengu wa roho.

-          Daniel 4 : 17 – hukumu hii imekuja kwa agizo la walinzi na amri hii kwa neno la watakatifu…

-          kwa hiyo waombaji wa aina hii wanao uwezo wa kutoa maamuzi juu ya maeneo yao wanayoyaombea.

 

2.       Waombaji watengenezaji

Ezekiel 22 : 30 – nami nikatafuta mtu miongoni mwao atakayelitengeneza boma na kusimama mahali palipobomoka

-          Hawa ni waombaji ambao wapo kwa ajili ya kurejesha mahusiano yaliyoharibika kati ya Mungu na watu wa mahali Fulani. Mfano nabii Eliya alijenga madhabahu ya Bwana iliyovunjika 1 Wafalme 18 : 30. Kipindi hiki cha nabii Eliya kulikuwa hakuna mahusiano mazuri kati ya Mungu na taifa la Israeli kwa sababu Israeli walikuwa wanamtumikia mungu Baali. Hivyo Eliya alikuja kwa ajili ya kurejesha mahusiano yaliyopotea.

 

3.       Waombaji wazalishaji

Wagalatia 4 : 19 – Vitoto vyangu navionea utungu mpaka Kristo aumbike tena ndani yao.

-          Pia hawa ni wanamaombi wenye mzigo wa kuwaombea watu ambao ni wachanga kiroho ili wakue kiroho wasitetereke na kurudi nyuma.

-          Hii inamaana kuwa sio kwamba tunaishia kuwaombea watu waokoke halafu tunawaacha bali tunatakiwa pia tuwaombee mpaka wakue kiroho waweze kujisimamia wenyewe.

-          Unapokwenda kumhubiria mtu aokoke kumbuka kuwa unawajibu pia wa kumuombea ili akue kiroho.

-          Mtume Paulo aliwahubiria watu wakaokoka lakini baada ya muda wale watu wakarudi nyuma, ikambidi aanze tena kuwaombea mpaka Kristo aumbike tena ndani yao.

 

KWA NINI TUNATAKIWA KUOMBA?

a.       Mwanamaombi ndiye mtu mwenye maamuzi ya mwisho juu ya hali ya kimwili na ya kiroho ya mahali anapotakiwa kupaombea.

Mathayo 16 : 19; 18 : 18 – 20

-          Mbingu zinakusikiliza wewe unaomba nini.

-          Unapoombea taifa lako au kanisa lako au familia yako, ni wewe ndiye unayeamua nini kifanyike juu ya mahali hapo unapopaombea.

-          Utakachokiomba ndicho kitakachofanyika

-          Kumbuka: Muombaji anatawala kwa njia ya neno lake (maombi anayoomba) kama vile ilivyo kwa mfalme anavyotawala kwa njia neno lake. Neno la mfalme ni sheria.

b.      Nguvu za kutengeneza majibu juu ya maswali au matatizo au mazingira magumu tunayokutana nayo hapa duniani ipo ndani yetu.

Waefeso 3 : 20

-          Unapoomba ndipo unaachilia nguvu za kutengeneza majibu ya hayo mambo unayopitia.

-          Tafsiri yake ni kwamba usipoomba basi utaendelea kupata shida mwenyewe wakati uwezo wa kutoka kwenye hiyo shida upo ndani yako.

c.       Maombi yanatusaidia kutokuingia majaribuni

Mathayo 26 : 41- kesheni mwombe msije mkaingia majaribuni

-          Kuna mazingira magumu ambayo hatupaswi tukutane nayo kwenye maisha yetu.

-          Hayo mazingira tutayaepuka kwa njia moja tu ambayo ni maombi, kwa sabau kwenye maombi ndipo utajulishwa na Roho mtakatifu wapi uende na wapi usiende, au nini ufanye na nini usifanye. Mathayo 2 : 12, 13

d.      Pia maombi yanatusaidia kupata neema ya kushinda majaribu

Waebrania 4 : 16 – na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri…, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

-          Tafsiri yake ni kwamba kuna neema ya kumsaidia mtu wa Mungu anapopita kwenye magumu aweze kutunza uchaji wa Mungu ndani yake bila kumtenda Mungu dhambi

-          Watu wengi wanapopita kwenye shida Fulani kwenye maisha yao huwa wanapoa kiroho kunakosababishwa na kushuka kwa kiwango chao cha kumwamini na kumtegemea Mungu

-          Sasa kazi mojawapo ya maombi ni kuhakikisha kiwango chako cha kumtegemea Mungu kinazidi kuongezeka hata kama unapita kwenye magumu.

e.       Maombi ni njia mojawapo anayoitumia Mungu kuwasiliana na watu wake.

Isaya 41 : 21- leteni maneno yenu…, toeni hoja zenu zenye nguvu…

Isaya 43 : 26 – unikumbushe na tuhojiane.

-          Unapoona mahali pameandikwa hoja au tuhojiane, tafsiri yake ni kwamba kuna kuwa na mazungumzo baina ya pande mbili. Na kila upande unatoa hoja zake.

-          Hayo ndiyo mawasiliano yanayotokea baina ya pande mbili.

-          Kwa hiyo Mungu anaweza akakusemesha wew pale unapokuwa katika hali ya maombi, lakini pia wewe unaweza ukamsemesha Mungu unapokuwa katika maombi.

-          Ukumbuke kuwa mawasiliano yanatengeneza mahusiano. Mawasiliano yakiwa mazuri basi na mahusiano yatakuwa mazuri, bali mawasiliano yakiwa mabaya na mahusiano pia yatakuwa mabaya.

NB: Mungu akusaidie kusimama vizuri kwenye zamu yako ya maombi kwa kuwa usipoomba wewe hakuna mwingine atakayeomba kwenye nafasi yako.

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...