Msisitizo/lengo la somo: Kukusaidia utoke kwenye madhara yanayotokana na kutokusamehe.
Somo linaeleza namna ambavyo mtu
anaweza akaathirika kiroho au akadhoofika kiroho kwa sababu tu hana tabia ya kusamehe
wengine wanaomkosea.
-
Inawezekana ikawa ni wazi kabisa kwamba umeokoka na
wala dhambi zingine hazikusumbui yaani unajua kuziepuka na unazishinda, au ni
muombaji mzuri na unaendelea kumtumikia Mungu, lakini unakwama kwenye eneo la kusamehe
wanaokukosea.
-
Tabia ya kusamehe ni tabia ya Mungu, bali shetani
hawezi kusamehe
-
Hivyo kutokusamehe wengine ni tabia ambayo asili yake
ni Shetani.
-
Huwezi ukawa mtoto wa Mungu halafu ukawa si mtu wa
kusamehe wanaokukosea.
Shetani
hawezi kusamehe ndio maana anafanya
kisasi na malipizi
-
Kwa hiyo ndani yako ukiona una tabia ya kulipa kisasi
– maana yake huwezi kusamehe na ndio unajitambua wazi kuwa ndani yako hayumo
Roho wa Bwana bali roho ya Shetani
Mathayo 6 : 12
Biblia inasema hivi “utusamehe deni
zetu kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu”
-
Huu mstari ukisoma kwa makini utagundua kuwa uzito
wake upo kwenye lile neno “kama” ambapo tafsiri yake ni kwamba
“tunapoomba msamaha mbele za Mungu, tunamfanya atumie kipimo kile kile
tunachotumia sisi katika kuwasamehe wengine”
-
Kipimo ambacho unatumia wewe kuwasamehe wale ambao
wamekukosea, ndicho kipimo hicho hicho ambacho Mungu atakitumia kukusamehe wewe
makosa yako.
NB: Haijalishi huwa unaomba toba kwa muda mrefu kiasi gani, na
hata kama ukataja majina yote ya Mungu lakini kama huna tabia ya kuwasamehe
wale waliokukosea wewe, basi unakosa kigezo cha kusamehewa dhambi zako mbele za
Mungu.
-
Hii ni kanuni katika ulimwengu wa kiroho ndani ya
ufalme wa Mungu. Huwezi ukasamehewa kama wewe husamei wengine.
-
Na kitu cha ajabu ni kuwa, aliyeiweka kanuni hii ni
Mungu mwenyewe.
Ni kweli kabisa kusamehe ni kazi
sana na ni ngumu sana hasa pale aliyekukosea akiwa hata hajakuomba msamaha.
Kibinadamu ni ngumu lakini kwa Mungu yote yanawezekana.
Tulipookoka, tuliuvua utu wa kale tukavikwa utu mpya.
Waefeso 4 : 23 – 24
Biblia inasema “na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu;
mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu
wa kweli”
-
Nataka uyaangalie hayo maneno yaliyopigiwa mstari hapo
juu.
-
Utu mpya umeumbwa kwa namna ya Mungu.
-
Kwa hiyo, hapo zamani jambo la kusamehe wengine
lilikuwa ni gumu kwa sababu tulikuwa na namna ya kibinadamu (utu wa kale) ndani
yetu, lakini sasa tumeokoka hivyo tumeuvaa utu mpya ambao umeumbwa kwa namna ya
Mungu, kwa hiyo kusamehe halitakiwi kuwa swala gumu tena.
-
Shetani anachokifanya ni kukuletea tabia za utu wa
kale wakati wewe umeuvaa utu mpya.
Utu mpya ulioumbwa kwa namna ya
Mungu - maana yake utu mpya umeumbwa katika tabia ya Mungu, katika sura ya
Mungu, katika utaratibu wa Mungu.
-
Hivyo yale yote ambayo ni magumu kuwezekana kibinadamu
basi kwa Mungu yote yanawezekana. Ndivyo Luka
1 : 37 inavyosema.
-
Katika hayo yaliyokuwa hayawezekani kibinadamu na sasa
kwa Mungu yanawezekana ni pamoja na swala la kusamehe waliotukosea.
-
Mahali pengine kwenye Biblia inasema samehe saba mara sabini- maana yake
usichoke kusamehe kwa sababu hiyo ni tabia ya Mungu na sio ujinga.
-
Watu wengine wanadhani ukimsamehe aliyekukosea dunia
itakuona ni mshamba. Ni kweli unaweza ukawa mshamba kwao lakini mbele za Mungu
wewe ni wa thamani sana.
Kumbuka kuwa Biblia inatuambia tusiifuatishe
namna ya dunia hii. Kwa hiyo tusifuate dunia inasema nini bali tufuate Bwana
Yesu anasema nini.
KWA NINI TUNATAKIWA TUWE NA TABIA
YA KUWASAMEHE WATU WALIOTUKOSEA?
Kwa nini Mungu anaweka mkazo sana
sisi tuwasamehe wale waliotukosea? Kwani kuna shida gani tusipo wasamehe?
Unajua wakati mwingine unaweza
ukadhani ya kwamba Mungu ni Dikteta (unadhani ya kuwa hana huruma na wewe), kwa
sababu ni kama anakusisitiza uwasamehe wale waliokukosea wewe badala ya wao
ndio waje kwako wakunyenyekee ili uwasamehe. Lakini ukweli ni kwamba Mungu
anatupenda sana ndio maana anatuwazia mema siku zote.
Ukipita vizuri kwenye hili somo
utajua ni kwa nini ni muhimu sana wewe kuwasamehe waliokukosea hata kama
hawajarudi kukuomba wewe msamaha.
Tunatakiwa tusamehe kwa sababu
zifuatazo:
1.
Ili kupata
rehema au msamaha wetu kutoka kwa Mungu.
Mathayo 6 : 14 – 15 – kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu
wa mbinguni atawasamehe ninyi makosa yenu… msiposamehe na yeye hawasamei ninyi.
-
Anayeanza kusamehe kwanza si Mungu kwanza bali ni wewe
kwanza.
-
Mungu anaangalia akiba yako ya msamaha kwa wengine
ndipo anajua kama unastahili kupata msamaha au la.
-
Kusamehe wengine ni tiketi ya wewe kupata msamaha
kutoka kwa Mungu. Bila hiyo tiketi huwezi kupata msamaha kutoka kwa Mungu.
-
Na kama hujapata msamaha wa Mungu maana yake huwezi
pia ukashirikiana naye.
Ile “sala ya Baba yetu” inatuonyesha mambo tofauti tofauti ikiwemo
vipaumbele vya ufalme wa Mungu. Sasa katika uflme wa Mungu, tunaona sheria ya
msamaha ilivyo.
-
Sheria ikiwekwa mahali popote, pona yako si kuivunja
sheria bali ni kuifuata sheria.
-
Sasa wewe ukiwa ni mwana wa ufalme wa mbinguni ni
lazima ukatambua sheria zilizopo katika huo ufalme uliopo. Na mojawapo ya
sheria ndio hiyo ya kwamba huwezi ukasamehewa kama wewe husamei wengine.
NB: Anayeanza kusamehe si Mungu
kwanza bali ni wewe kwanza.
-
Wewe ndiye unayempa Mungu nafasi ya kukusamehe au
kutokukusamehe.
2.
Ili
tusiingie kwenye vifungo vya kiroho kwenye maisha yetu
Mathayo 18 : 21 – 35
-
Hii ni hadithi ya mtu mmoja aliyekuwa akifanya kazi
kwa bosi wake ambaye alikuwa ni mfalme, na alifanya kosa la kupoteza kiasi
kikubwa cha fedha. Bosi wake mtu huyo aliamuru huyu mtu auzwe pamoja na mke
wake na watoto wake lakini huyo mtu aliomba sana msamaha naye akasamehewa.
Shida ilikuja pale ambapo yeye sasa alipokutana na mtu mwingine aliyekuwa
anamdai dinari, aliamua kumtesa, kitu ambacho hakikuwapendeza hata watu
walioona jambo lile. Walioona wakamtaarifu Yule mfalme naye akamshika Yule mtu
na kumtesa sana.
-
Biblia inasema katika mstari wa 35 kwamba “Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni
atakavyowatenda ninyi msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake”
-
Huu mstari
ni mzito kupita tunavyoweza kuusoma.
-
Anachokieleza hapa ni kwamba, Mungu atawatendea wale
wasiosamehe wengine vile vile kama Yule mfalme alivyomtendea Yule mtumwa wake
mwovu.
Alimtendea
nini? Alimpeleka kwa watesaji.
Kwa hiyo,
Mungu naye atawesa au ataachilia mateso
(vifungo) kwenye maisha yako ambayo asili yake ni wewe kutokusamehe.
-
Maana yake hiyo ni adhabu ya Mungu kwa wale wasiokuwa
na tabia ya kuwasamehe waliowakosea.
Unajua kwamba unaweza ukawa
unapitia mahali fulani pagumu kwenye maisha yako, ukadhani ni Shetani ndiye
aliyesababisha kumbe si Shetani bali ni adhabu ya wewe kutokusamehe wengine.
Mungu anaamua kuachilia adhabu juu
yako kwa jambo ambalo kikawaida usingefikiri kama angekuadhibu.
-
Hivi ushawahi kufikiri, ni kweli kwamba huyu mtu
alikuwa ana haki ya yeye kumkamata aliyekuwa anamdai dinari (tena pengine hata
kumtesa ilikuwa ni haki yake). Lakini Yule mfalme alimwambia “Je haikukupasa
wewe kumsamehe mjoli wako kama mimi nilivyokurehemu wewe?”
-
Maana yake ni kwamba huyu mtumwa ilimpasa yeye pia kumsamehe
mjoli wake kwa sababu yeye naye alisamehewa deni lake.
NB: Sasa angalia jambo la ajabu kwenye hii mistari ifuatayo:
Mathayo 5 : 23 – 26 na Luka 12 : 58 – 59
Angalia yale maneno “patana na
mshitaki wako mapema”
-
Kwa nini Yule aliyekukosea, Biblia inamuita mshitaki
wako?
Kwa sababu,
katika ulimwengu wa roho Yule aliyekukosea ndiye anayegeuka kuwa mshitaki wako.
Anakuwa mshitaki wako kwa sababu hujamsamehe. Ile tu kwamba hujamsamehe,
inakuwa kwako ni mashitaka.
-
Kwa hiyo, Biblia inaposema patana na mshitaki wako
kwanza, hiyo ni lugha ya kiroho yenye maana ya kumsamehe.
Hivyo, ukirudi kwenye ile Mathayo 18 : 35 utaelewa kuwa Mungu anaweza
akampa mtu adhabu kwa sababu ameshitakiwa mbele zake kwa kutokuwasamehe
waliomkosea. Dhambi inakuwa ni kutokusamehe.
Maisha yako yanaweza yakawa
yamebanwa mahali, huwezi kujinasua hapo ukidhani ni Shetani ndiye aliyeyabana
kumbe uko kifungoni. Na aliyekufunga ni Mungu mwenyewe.
-
Hakuna shida ngumu kama hiyo ya kufungwa na Mungu kwa
sababu unakosa mtetezi. Hakuna wa kukuamulia.
-
Unaweza ukakemea kuanzia asubuhi mpaka jioni na bado
shida yako iko pale pale.
-
Ili kutoka kwenye hiyo shida ni mpaka utambue siri hii
iliyopo kwenye kusamehe wengine.
Sasa wewe mtu wa Mungu hutakiwi
kuona shida katika kusamehe kwa sababu kusamehe kuna kusaidia wewe usikosane na
Mungu wako.
-
Mbele za Mungu, kutokusamehe ni dhambi kama dhambi
zingine.
-
Hivyo ni muhimu ukawa makini usije ukashindwa kukua
kiroho kwa sababu tu umewaweka watu moyoni kwa kutokuwasamehe.
-
Anayekaa moyoni mwako ni Yesu na sio watu.
3.
Ili tupate
amani (raha) moyoni
Unapoacha kusamehe, kinachopata
shida sana ni moyo wako.
Ndio maana Mungu hawezi akaa bila
kutusamehe kwa sababu kinamuumiza moyoni.
Ile Isaya 43 : 25 inasema – Mimi ndimi niyafutaye makosa yenu kwa ajili
yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zenu.
-
Pale anaposema anatusamehe dhambi zetu kwa ajili yake,
inaonyesha kuwa hatusamehewi kwa sababu tumeomba tusamehe bali ni tabia ya
Mungu kutusamehe na pia hawezi kukaa bila kutusamehe.
-
Hivyo hata wewe mwanadamu ukikaa bila kusamehe ni
lazima utapata shida moyoni mwako.
Mathayo 11 : 28 – 29 – ukishatua mzigo kwa Yesu utapata raha nafsini mwako
au moyoni mwako.
-
Kutokusamehe ni kuweka mzigo moyoni mwako ambao
utaondoa amani au raha ndani yako.
-
Na ndio maana watu wengi wameokoka lakini hawana amani
au hawana furaha mioyoni mwao. Kwa sababu gani? Kwa sababu hawajui kuwasamehe
watu waliowakosea.
NB: Ukikosa amani au raha moyoni mwako utakuwa umekosa kitu
kikubwa sana na cha muhimu sana.
Kumbuka kwamba,
a.
Amani ndani
yako ndiyo inayokupa uwe na maamuzi sahihi – Wakolosai 3 : 15
-
Ndio maana watu wengine wanakuwa ni wenye hasira za
karibu na huwa hawana maamuzi sahihi kwenye mambo yao
b.
Pia, Amani
ndiyo inayobeba na kuhifadhi umoja wa Roho ndani yako – Waefeso 4 : 3
-
Ukipoteza amani ndani yako ni wazi kabisa hutokuwa na ushirika
mzuri na watu wengine, hata kama mnasali pamoja.
-
Mahusiano yako na watu wengine yanategmea kiwango cha
amani kilichopo moyoni mwako
-
Amani ikiwepo basi mahusiano yatakuwa mazuri, lakini
amani isipokuwepo na mahusiano hayatakuwa mazuri.
c.
Amani yako
inaweza ikatuonyesha kiwango cha imani yako – Warumi 5 : 1
-
Biblia inatuambia kuna uhisiano kati ya amani na
imani.
-
Amani ni matokeo ya imani ya kuhesabiwa haki, kwa hiyo
amani ikipotea inaonyesha kwamba ni wazi kuwa imani imepotea pia.
Tunamuhitaji Mungu sana katika
jambo hili maana si jepesi kibinadamu lakini kwa Mungu ni jepesi.
Mshirikishe Mungu katika shida yako
naye atakusaidia namna ya kutoka hapo.
Hata kama huwezi kusamehe kwa
sababu unaona kosa la mtu aliyekukosea ni kubwa sana, wewe nenda mbele za
Mungu, jiweke wazi mbele zake, mwambie kuwa huwezi kusamehe, lakini unahitaji
msaada wake. Utashangaa namna ambavyo ataachilia utulivu ndani yako na nguvu za
Roho Mtakatifu zitakujilia ndani yako na hapo hapo utapokea amani moyoni na
ndiyo itakusaidia kusamehe.
-
Ile ile amani ambayo inaondoka kutokana na
kutokusamehe ndiyo hiyo hiyo Yesu atairudisha kwa sababu ni yeye ameuondoa
mzigo wa kutokusamehe moyoni mwako.
Bwana Yesu anao uwezo wa kukusaidia
kusamehe. Hata kama shida ni kubwa namna gani, wewe nenda mbele zake naye
atautua mzigo wako.
No comments:
Post a Comment