UTOAJI WA SADAKA YA ZAKA KAMA NGUZO MOJAWAPO YA MSINGI KATIKA KUIMARISHA UHUSIANO WAKO NA MUNGU

 Lengo la somo hili: Ni kukujengea ndani yako tabia ya kutoa zaka kwa usahihi ili kuinua kiwango chako cha kumjua Mungu na kutembea katika mapenzi yake.

Yako mambo mengi yanayoweza yakaimarisha uhusiano wako na Mungu, lakini mojawapo kati ya hayo ni utoaji wa zaka.

Kwa mfano: maombi, kusoma Neno la Mungu, kushuhudia n.k ni baadhi ya mambo yanayoimarisha mahusiano yako na Mungu. Lakini pia kuna hili jambo linaloitwa “Zaka“ ni jambo la muhimu sana katika kujenga msingi mzuri ndani yako wa kumfahamu Mungu.

Malaki 3 : 7 – 10

“Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande mkayaacha maagizo yangu wala hamkuyashika….. leteni zaka kamili ghalani ….”

Ule msatari wa 10 unasema “leteni zaka kamili ghalani…”

-          Maana yake zaka timilifu au zaka yote, na wala sio nusu au kiasi.

-          Lakini huwezi ukauelewa huu mstari vizuri kama hujaanzia kwenye msatari wa 7 ambao unaonyesha jinsi Mungu anavyohuzunika kwa kuwa wana wa Israel wamegeuka na kumwacha Bwana na wala hawafuati tena maagizo ya Bwana. Lakini wao wanamuuliza Bwana kuwa wamemuachaje? Naye anajibu kwa kuwaagiza walete zaka iliyo kamili.

-          Wale wana wa Israel walianza tabia ya kuleta zaka isiyo kamili mbele za Bwana na wakaona ni jambo la kawaida, lakini Mungu hakupendezwa na hiyo tabia, ndio maana akaamua kuwaambia wajirekebishe kwa kutengeneza kile kilichowafanya wamuache Mungu.

-          Hao watu hawakufahamu kuwa kwa tabia yao ya kutokuleta zaka iliyo kamili iliwafanya waharibu mahusiano yao na Mungu wao, bali wao waliona ni sawa tu.

-          Wao waliona ya kwamba kule kwenda kanisani na kutoa sadaka kikawaida ilitosha kuimarisha ukaribu wao na Mungu wao! Hapana!

Uhusiano wako na Mungu haujengwi tu kwa sababu unakwenda kanisani au unatoa sadaka tu kiholela holela bila kufuata kanuni za Mungu katika utoaji, bali uhusiano wako na Mungu unajengwa kwa kufuata maagizo yake na sheria zake katika kutimiza kusudi lake.

MAMBO YA MSINGI YA KUYAJUA KWANZA

a.      Maana ya zaka

Zaka ni aina mojawapo ya sadaka anayoitoa mtu kwa kutoa fungu la kumi katika mapato yake.

-          Zaka ni 10% au fungu la kumi la mapato yako

-          Mungu aliagiza mwenyewe ya kwamba tutoe zaka katika mapato yetu yote

Ziko aina nyingi ya sadaka, lakini sadaka nyingi ni za hiari bali sadaka ya zaka ni ya lazima

b.      Mahali unapotakiwa upeleke sadaka yako ya zaka

-          Mungu aliagiza zaka itolewe mahali alipoliketisha jina lake (maana yake hekaluni)

-          Hesabu 18 : 21 – 24 – zaka ni mali ya Haruni na familia yake

-          Sadaka ya zaka wanapewa makuhani, ndivyo Mungu alivyoagiza

-          Huwezi ukaibadilisha sadaka ya zaka iwe kama sadaka ya kawaida halafu uitoe kwa mtu yeyote tu. Hapana. Sadaka ya zaka inakwenda moja kwa moja kwa makuhani.

 

c.       Zaka ya zaka

-          Unapopeleka sadaka yako ya zaka kwa kuhani, naye pia anatoa zaka katika hiyo zaka aliyoipokea. Hiyo ndio inaitwa zaka ya zaka.

-          Maana yake ni fungu la kumi la fungu la kumi lililopokelewa hekaluni.

-          Kiongozi wa kanisa au mchungaji au kuhani anayepokea zaka inambidi nay eye atoe zaka katika hiyo zaka aliyoipokea.

-          Hesabu 18 : 25 – 26

-          Nehemia 10 : 38

 

d.      Mahesabu ya zaka yalivyo.

Zaka ni sadaka pekee ambayo ni lazima uipigie mahesabu. Unatakiwa upige asilimia kumi (10%) ya mapato yako

Kwa mfano:

i.                    Kama ni mtu unayepokea kipato chako kwa mwezi;

Mfano, umepata sh 100,000/= zaka yake ni sh 10,000/=

ii.                   Kama unapata kipato chako kutoka kwenye biashara

Zaka unaitoa kwenye faida unayoipata. Mfano, biashara yako unapata kipato cha sh 20,000/= kwa siku lakini faida pekee katika hicho kipato chako ni sh 10,000/= basi zaka utaitoa kwenye sh 10,000/= ambayo itakuwa ni sh 1,000/=

iii.                 Pia kama ndio umeanza kufanya biashara na umekopa mtaji wa biashara hiyo

Zaka utaitoa kwenye faida unayoipata baada ya kutoa mtaji

Mfano, mtaji wa biashara yako ni sh 500,000/=

Na unarejesha sh 50,000/= kila mwezi, lakini kipato chako kwa mwezi kinafika sh 70,000/=

Basi, utatoa kwanza mtaji ambao ndio rejesho kwenye hicho kipato cha mwezi halafu kitakachobaki ndio utatoa zaka.  70,000 – 50,000 = 20,000 hivyo utatoa zaka katika sh 20,000 ambayo ni sh 2,000/=

NB: Ukishamaliza kuulipa mkopo wote, hapo ndipo utakapokuwa unatoa zaka kwa kuipigia kwenye faida yote unayoipata kwa kila mwezi. Kama unapata sh 70,000 kwa mwezi basi utaipigia zaka katika hiyo fedha yote maana hakuna mkopo wa kutoa.

 

iv.                 Kuna zaka za mifugo na mazao au nafaka

-          Kama wewe ni mfugaji wa ng’ombe kwa mfano, wakizaa watoto (mfano watoto 10) basi unatakiwa umtoe mtoto mmoja sadaka ya zaka.

Au wewe unafuga kuku na ukapata vifaranga labda tuseme 20, basi vifaranga 2 ndio zaka, unatakiwa uipeleke kwa mchungaji.

-          Lakini pia unaweza ukawa unafuga ng’ombe au kuku au kondoo au mbuzi na ukapata labda tuseme mtoto mmoja, basi ukimuuza mtoto huyo utatakiwa upige asilimia kumi yake ili utoe zaka.

-          Vivyo hivyo na kwenye mazao

Kama wewe ni mkulima na umelima mahindi kwa mfano, halafu ukavuna magunia 10 basi gunia moja ni zaka.

 

NB: Zaka inayotokana na mazao au mifugo ni muhimu kwanza uibadilishe kuwa fedha ndipo uitoe maana hiyo ndio njia rahisi nay a uhakika katika utoaji wa zaka hiyo

-          Kumb 14 : 22 – 25

Unaweza pia ukasoma:

2 Nyakati 31 : 5 – 6

Walawi 27 : 30 – 33

Nehemia 13 : 12

 

Kwa hiyo, kulingana na Malaki 3 : 10, ukisoma kwenye tafsiri za kiingereza lile neno “leteni zaka kamili” utakuta anamaanisha “leteni zaka yote”. Mungu anataka tutoe zaka kwa utimilifu na uaminifu wote.

 

 

SABABU YA MUNGU KUAGIZA TUMTOLEE ZAKA

Ø  Mungu ameagiza watu tumtolee zaka - ili uwepo wake ukae katika kile ulichokitolea zaka.

-          Kama ni kazi basi uwepo wa Mungu ukae kwenye hiyo kazi

-          Na kama ni biashara basi uwepo wa Mungu ukae kwenye hiyo biashara

Unajua kuna tofauti ya uwepo wa Mungu kukaa ndani yako wewe uliyeokoka na uwepo wa Mungu kukaa kwenye shughuli yako unayofanya.

-          Ile kwamba umeokoka na Mungu yupo ndani yako haimaanishi kuwa pia na Uwepo wa Mungu upo kwenye biashara yako au kazi yako.

-          Na ndio maana wapendwa wengi wana hali ngumu kiuchumi kwa sababu wanadhani wakishaokoka basi na biashara zao au kazi zao tayari zinakuwa na ulinzi wa kimungu. Mambo hayakwendi hivyo.

-          Unaweza ukawa umeokoka na ulinzi wa Mungu upo juu yako lakini biashara au kazi yako haina ulinzi wa Mungu.

-          Kwa hiyo unapotoa zaka unaruhusu uwepo wa Mungu ukae katika biashara yako au kazi yako au shughuli unayoifanya.

-          Maombi yako hayatoshi kulinda biashara yako bali sadaka ya zaka inaweza na inamruhusu Mungu kumkemea yeye alaye au aharibuye.

Malaki 3 : 11 – 12

 

UMUHIMU WA KUTOA ZAKA

Kutoa sadaka ya zaka ni agizo la Mungu kwa kila mtu kutokana na kipato chake.

-          Unajua sio kwamba Mungu ameagiza watu watoe zaka kwa sababu ana shida na hela yako bali ni kwa ajili ya kukusaidia wewe unayetoa hiyo zaka ili uwepo wake ukae kwenye hicho unachomtolea zaka.

-          Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana kwa kila mkristo kujua kutoa zaka kwa ukamilifu na kwa uaminifu.

Yafuatayo ni mambo yanayotokea unapotoa zaka:

1.      Uwepo wa Mungu unaketi katika kazi au biashara au shughuli unayoifanya.

Malaki 3 : 11 - 12

Kutoka 25 : 1 – 2, 8

 

Sadaka yoyote inaleta uwepo wa Mungu mahali ambapo unapatolea sadaka.

-          Kama unatoa sadaka kwa miungu basi unaachilia uwepo wa miungu kuketi mahali hapo ulipopatolea sadaka. Na kama unatoa sadaka kwa Mungu aliye hai basi unaachilia uwepo wa Mungu ukae mahali hapo ulipotoa sadaka hiyo.

-          Kwa hiyo sadaka ya zaka, nayo pia inampa nafasi Mungu akae katika hiyo shughuli au biashara uliyoitolea zaka.

-          Na Mungu akiketi mahali basi utapata kibali, utapata ulinzi wa Kimungu, utapata uwezesho wa Kimungu, utapata kustawi, utapata ushindi n.k

Wana wa Israel waliambiwa watoe sadaka kwa moyo wa kupenda ili Mungu aketi katikati yao.

-          Sadaka inampa Mungu uhalali wa kukaa mahali

-          Na ndio maana walikuwa wanajenga madhabahu ili watoe sadaka juu ya hizo madhabahu.

-          Kazi mojawapo ya madhabahu ni kujulisha aina ya mungu anayemiliki hilo eneo ambalo limejengwa madhabahu. Na hakuna madhabahuambayo hawatoe sadka juu yake.

-          Unapotoa sadaka juu ya madhabahu maana yake ni unaonyesha uhalali wa mungu anayemiliki mahali ambapo madhabahu imejengwa. Na ndio maana huwezi ukajenga madhabahu mbili za miungu miwili tofauti katika eneo moja la sivyo eneo hilo litakuwa na vita vikali sana mpaka mungu mmoja mwenye nguvu ashinde. Na kinachoipa nguvu madhabahu ni ile sadaka inayotolewa juu ya hiyo madhabahu

Kama wewe ni mfanyabiashara, pale unapofanyia biashara kuna watu wanakwenda kutoa sadaka kwa miungu yao ili miungu hiyo iwafanikishe katika shughuli zao. Sasa kama na wewe hujajua namna ya kutoa sadaka hasa ya zaka ili Mungu wako apate kukaa katika hiyo biashara yako basi utakuwa ni mtu wa kushindwa tu siku zote.

 

2.      Unapata haki ya kupata baraka kutoka kwa Bwana

Malaki 3 : 10

“mkanijaribu kwa njia hiyo muone kama sitawafungulieni madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka”

-          Sadaka ya zaka inakupa haki au kibali cha kupata baraka za Bwana

-          Unakuwa na uhuru wa kumdai Bwana akupe baraka kwa sababu ni Mungu mwenyewe ndiye aliyesema tukamjaribu kwa njia ya kutoa zaka.

Baraka - maana yake ni kustawi, kufanikiwa, kupata kibali, kuongezeka n.k

-          Faida unayoipata kutoka kwenye kazi au biashara yako, italindwa na Mungu ili uitumie kwa maendeleo, kuongeza mtaji, kufanyia maendeleo ya familia yako.

-          Ni tofauti na Yule mtu asiyekuwa na mbaraka wa Bwana, anaweza akapata faida kubwa lakini isimsaidie huyo mtu chochote, anakuwa ni mtu wa kuandamwa na mabalaa na mikosi mbalimbali

 

3.      Zaka inaleta roho ya kumcha Mungu ndani ya mtoaji

Kumb 14 : 22 – 23

Mtu mwenye tabia ya kutoa fungu la kumi mara kwa mara ni lazima ndani yake ijengeke hofu ya Mungu.

-          Ndani yako mazoea yanaondoka na badala yake inaingia tabia ya kumcha Bwana.

-          Unajua kuna wakati mwingine unaweza ukaombea sana uamsho uje kanisani, ili watu wajifunze kumcha Bwana, halafu unashangaa Mungu anakusisitizia juu ya kutoa zaka. Kumbe anakujulisha kuwa kwa njia ya kutoa zaka tunaweza kujifunza kumcha Bwana.

-          Mungu hawezi kukuruhusu uendelee kumtolea zaka na bado ukawa hujui kumcha yeye.

Matendo 10 : 1 – 4

Upo uhusiano kati ya kutoa sadaka na kumcha Bwana. Ni vitu viwili ambavyo haviwezi vikaachana.

 

4.      Zaka inaachilia roho ya utumishi kwenye uzao wako.

Mwanzo 14 : 17 – 20 – 24

Ebrania 7 : 1 – 10

Hii ni habari ya Ibrahimu wakati ametoka kuwapiga wale wafalme watano, Biblia inasema akakutana na mfalme Melkizedeki ambaye alimpa sadaka ya fungu la kumi la vitu vyote alivyoviteka nyara.

-          Kitu cha ajabu hapa ni kwamba, utoaji huu wa zaka uliachilia roho ya utumishi kwenye kizazi chake ambapo roho hiyo ilipita mpaka kwa Lawi na uzao wake ambao walikuja kuwa makuhani.

-          Lawi alikuwa ni mtoto wa Yakobo, maana yake ni uzao wa tatu kutoka kwa ibrahimu

-          Katika kipindi cha Musa, kabila la Walawi ndili kabila pekee lililopewa kuihudumia madhabahu ya Bwana na kupokea sadaka ya fungu la kumi. Na Biblia inaweka wazi kabisa kuwa wakati Ibrahimu anatoa sadaka ile kwa Melkizedeki na Lawi pia alikuwepo hapo japo alikuwa katika viuno vya Ibrahimu.

-          Kwa tafsi nyingine ni kwamba kutoa sadaka kwa babu (Ibrahimu) kuliachilia roho ya utumishi kwa kitukuu chake (Lawi).

 

ITIFAKI YA KUTOA SADAKA

Ni lazima unapokwenda kutoa sadaka mbele za Mungu uwe na imani.

Ebrania 11 : 6 – “kila amwendeaye Bwana lazima aamini kuwa yupo …”

-          Imani ndio inayofanya fedha yako iitwe sadaka. Kwa mfano, unaweza ukawa n ash 1,000/= halafu ukaamua kumtolea Mungu sadaka y ash 500/= na wewe ubaliwe na sh 500/=. Ile 500 uliyoitoa sadaka na ile 500 uliyobakiwa nayo tofauti yake ni imani. Mia tano ya kwanza ambayo ni sadaka imebeba imani ndani yake bali mia tano ya pili ambayo sio sadaka haina imani ndani yake.

 

 

Mwanzo 28 : 20 – 22 & Mwanzo 31 : 10 – 13  (Yakobo aliweka nadhiri ya fungu la kumi)

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...