Msisitizo wa somo: Ni kukusaidia kuachilia ndani yako msukumo wa maombi na kuutafuta uso wa Bwana kwa bidii haliukijua ya kwamba muda wetu wa kukaa hapa duniani ni mchache sana.
Napenda kurudia jambo hili kwamba katika ulimwengu
wa roho kwa sasa kuna uharaka upo, ambao umeachiliwa kwa kila mtu aliyerohoni
ili kumsaidia kukaa vizuri na Mungu kwa kujiweka tayari kwa ajili ya kumpokea
Bwana Yesu atakapokuja kulichukua kanisa lake.
Somo hili linahusu maandalizi anayopaswa kufanya mtu
wa Mungu katika nyakati hizi za siku za mwisho.
-
Unaweza ukajua ya kuwa hizi ni siku za mwisho lakini usijue ni nini cha
kufanya katika hizi siku za mwisho.
-
Kwa hiyo somo hili litakusaidia kukuwekea msingi thabiti wa kufanya
maandalizi ili usije ukabaki wakati wa kuja kwa Yesu Kristo mara ya pili
Luka 12 : 35 –
48
Mathayo 24 :
42 – 51
Biblia inazungumza habari ya kukesha na kuwa tayari
kwa ajili ya kurudi kwa Yesu Kristo mara ya pili ulimwenguni.
Na inaeleza mambo ya msingi kabisa ambayo kama
kanisa na watu wa Mungu tunatakiwa tuyafanye wakati tupo katika kipindi hiki
cha nyakati za mwisho.
Bwana Yesu wakati anafundisha na kuelezea mambo
yatakayotokea katika nyakati za mwisho alielezea pia tabia na wajibu wa
watumishi wake wanavyopaswa kuwa katika nyakati hizo.
Lakini kabla hatujaangalia maandalizi ya kujiweka
tayari kwa ajili ya kumpokea Yesu Kristo atakapokuja mara ya pili, hebu kwanza tuangalie
maana ya maneno yafuatayo:
a. Maandalizi
Maandalizi maana yake ni matayarisho
Matayarisho ni yale mambo yanayofanyika kabla ya
jambo lililokusudiwa kutokea au kufanyika.
Kwa mfano: unapotaka kwenda kazini asubuhi baada ya
kuamka, kuna mambo ya kufanya kwanza kabla ya kuondoka: unakwenda kupiga
mswaki, halafu unaoga kisha unavaa ndipo unaondoka. Hayo yote yanaitwa
maandalizi ya kuondoka kwenda kazini.
Vivyo hivyo na sisi pia tunatakiwa tufanye
maandalizi ya kuwa tayari kipindi hiki cha siku za mwisho.
b. Nyakati za mwisho
Biblia inaposema nyakati za mwisho au siku za mwisho
maana yake ni siku tunazotarajia kurudi kwa Bwana Yesu mara ya pili ulimwenguni
kwa ajili ya kulichukua kanisa lake (yaani unyakuo)
Manabii na mitume mbalimbali walitabiri kuhusu
kurudi kwa Yesu mara ya pili na kuelezea mambo yatakayotokea katika siku hizo.
Kwa mfano: Daniel 12 : 1 – 13
Mathayo 24 : 1 –
51
Marko 13 : 1 –
37
Luka 21 : 5 – 36
1 Wathesalonike
5 : 1 – 11
2 Wathesalonike
2 : 1 – 17
2 Timotheo 3 : 1 – 9
Kitabu cha Ufunuo wa Yohana chote
Nataka ufahamu ya kuwa kurudi kwa Yesu ni hakika
wala si hadithi za kutungwa tu kama wengine wanavyodhani.
-
Na ukishajua kwamba ni jambo la uhakika basi utajiweka tayari.
Kipindi hiki cha siku za mwisho kimeambatana na
matukio mengi sana yanayopaswa kutokea ulimwenguni. Na katika hayo
yaliyotabiriwa kutokea, mengi yamekwisha kutokea yaliyobaki ni kidogo tu lakini
ili kugundua hivyo ni lazima uwe mfuatiliaji wa mambo yanayotokea duniani kwa
jicho la kiroho.
-
Ukiyaangalia kikawaida hutoona chochote bali ukiyapima kutokea rohoni
utagundua kuwa ni mambo yaliyokwisha kutabiriwa na utajua kuwa hizi ni nyakati
za mwisho.
MAMBO YA KUTILIA MKAZO
UNAPOJIANDAA KWA HABARI YA KURUDI KWA YESU
1. Kutambua majira na nyakati tulizopo
Luka 12 : 39,
& Mathayo 24 : 43
-
Kama mwenye nyumba angaliijua zamu au muda ambao mwizi atakuja,
angalikesha asingeiacha nyumba yake ivunjwe.
Bwana Yesu anasisitiza jambo la kujua majira ya
kujiliwa ili tusipate uharibifu ambao kwa kawaida tungetakiwa tusiupate. Kutokujua
kunaleta uharibifu na madhara na hasara.
Vipengele vifuatavyo ni vya muhimu kuvijua:
a. Kwa nini tunatakiwa tujifunze kujua majira yanayokuja?
i.
Kujua majira yanayokuja kunakusaidia kujiandaa kukabiliana na mambo
yaliyokusudiwa kutokea kwenye hayo majira yanayokuja.
Mfano: Askari anayejua kuwa
yuko vitani maandalizi yake ya kupigana vita sio sawa na askari ambaye hayuko
vitani. Wote ni askari lakini kinachowafanya watofautiane katika maandalizi yao
ni ufahamu walionao juu ya mazingira waliyopo. Mmoja anajua niko vitani kwa
hiyo kila wakati natakiwa kuwa tayari, na huyu mwingine anajua hayuko vitani
hivyo hafanyi maandalizi kama ya Yule aliyepo vitani.
-
Ndio maana kuna kitu kinachoitwa kambi.
-
Mwanajeshi yeyote anayekwenda kwenye uwanja wa mambano huwa anatokea
kambi na sio nyumbani.
-
Hata wachezaji mpira wanapokaribia kwenda kuchea mechi yoyote huwa
wanautaratibu wa kukaa kambini.
Ulishawahi kujiuliza ni kwa nini wanakaa kambini na
sio nyumbani? Kwani kuna ulazima gani wa kutokea kambini ndipo waende kwenye
mashindano? Kwa nini wasitokee nyumbani ndipo waende kwenye mashindano?
-
Jibu ni kwamba, nyumbani hawawezi wakafanya maandalizi sawa sawa na
wakiwa kambini.
-
Ile tu kwamba wanajua kuwa kuna mashindano yanakuja mbele yao, kunawapa
msukumo wa kujiandaa kwa ajili ya hayo mashindano.
-
Ndivyo na hivyo hivyo kanisa la Mungu tunatakiwa tujue ya kuwa nyakati
hizi ni nyakati za kujiweka tayari kwa ajili ya kunyakuliwa, hivyo hatupaswi
kuwa nyumbani bali kambini.
-
Ndio maana Biblia inasema “kesheni”
maana yake tuzidi kujiandaa kama tuko kambini na sio kama tuko nyumabni.
-
Nyumbani unalala lakini kambini hulali. Kwa hiyo anayekesha hakeshi
akiwa nyumbani bali anakesha akiwa kambini.
-
Katika ulimwengu wa roho watu wa Mungu tunatakiwa tuwe kambini na sio
nyumbani. Maana yake ni kwamba kama ni kuomba ni lazima tuongeze kiwango cha
maombi, na kama ni kusoma Neno basi tusome na kutafakari kwa bidii, pia na kama
ni kuutafuta uso wa Mungu basi tuutafute kwa bidii.
Inashangaza sana pale unapoona watu wa Mungu
wamepunguza kuomba, kusoma Neno yaani kama wako nyumbani vile badala ya kuwa
kambini. Mungu atusaidie sana.
ii.
Kujua majira na nyakati
kunakusaidia kuepuka athari ambazo zingetokea kwa sababu ya kutokujiandaa
Luka 19 : 41 – 44 – kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.
-
Kutokutambua majira kunaleta kuangamizwa.
-
Yesu aliulilia mji si kwa sababu mji ni mzuri bali aliulia mji kwa
sababu haukutambua majira ya kujiliwa kwake hivyo ukaangamizwa.
NB: Kujua tu ya kwamba hizi ni
nyakati za mwisho bila kufanya maandalizi ni sawa na kutokujua. Na watu wengi
wamekuwa wakisema tu hizi ni siku za mwisho hizi ni siku za mwisho lakini
hawajajiandaa kabisa. Hao hawajui kuhusu majira ndio maana hawajui nini cha
kufanya. Kama wangalijua majira na nyakati hizi ni nyakati za namna gani basi
wangalijua na yawapasayo kufanya.
b. Namna ya kutambua majira ya siku za mwisho (unatambuaje majira?)
Biblia imeweka wazi namna ya kutambua majira haya ya
siku za mwisho. Hebu tuangalie mistari ifuatayo: Mathayo 24 : 32 –
33,
Marko 13 : 28 – 29,
Luka 21 : 29 – 31
-
Kwa mtini jifunzeni, tawi lake linapoaanza kuchipuka basi mjue majira
ya mavuno yamekaribia, kadhalika nanyi myaonapo hayo yanapoanza kutokea basi
mjue kuwa yu karibu milangoni.
-
Bwana Yesu anatuambia kuwa tujifunze kwa mtini ambao ni lugha ya picha
akiwa anamaanisha taifa la Israel.
-
Maana yake ni kwamba tujifunze kufuatilia kile kinachotokea kule Israel
kwa sababu kupitia mambo yanayotokea Israel tutapata kujua majira na nyakati za
mwisho yanakwendaje.
v Baadhi ya mambo ambayo ni muhimu kufuatilia kuhusu taifa la Israel ni
ü Ujenzi wa hekalu la tatu
ü Mipaka ya nchi
ü Mji wa Yerusalem
ü Uongozi wa juu wa taifa
-
Israel ni saa kwa kanisa na ulimwengu wote.
-
Chochote kinachotokea katika taifa la Israel, kinatokea kwa makusudi,
kwa sababu Mungu ndiye aliyeliweka taifa hilo kuwa kama saa ya ulimwengu.
-
Unajua haitoshi tu kusema kwamba kutakuwa na vita kati ya taifa na
taifa, au njaa mahali mahali, au ukame au matetemeko ya aridhi na mambo
mengine; kwa sababu hayo yote yalishawahi kutokea huko nyuma miaka ya zamani
bali kitu anachotaka Bwana Yesu tukione hapa ni kwamba tangu kuzaliwa kwa taifa
la Israel (yaani kupata uhuru – tawi la mtini kuchipuka) kunaonyesha majira
yaliyokwisha kubadilika ulimwenguni. Si majira tena yale ya kale bali yamekuwa
ni majira ya nyakati za mwisho.
Ukiwa ni mfuatiliaji wa habari za Israel basi
haitakupa shida sana kujua namna ya kuiombea nchi hiyo, kwa sababu ni wajibu
wetu kama kanisa kuiombea nchi ya Israel kama taifa teule la Mungu.
Mungu alisema atakayeibariki Israel atabarikiwa na
atakaye ilaani Israel atalaaniwa.
-
Mwanzo 12 : 3
NB: Mtini, tawi lake
linapoanza kuchipuka halibadilishi majira yaliyopo bali linaonyesha majira
yaliyokwisha kubadilika tayari.
Ni hatari sana kwa watu wa Mungu kutokutambua majira
waliyopo.
-
Wana wa Israel wenyewe walikuwa wanaongozwa na wana wa Isakari ambao
walikuwa ni wajuzi wa nyakati na yawapasayo wana wa Israel kufanya – 1 Nyakati 12 : 32
-
Ukishajua majira uliyopo utajua pia na nini cha kufanya katika hayo
majira.
-
Haitoshi tu kusema hizi ni siku za mwisho bila kufanya maandalizi.
2. Kutumika kwa uaminifu katika utumishi wowote ulio nao
Mathayo 24 :
45 – 51 –
mtumwa mwaminifu …. awape watu chakula kwa wakati wake
Marko 13 : 33
– 34 –
bwana wa nyumba amewapa kila mtu kazi yake
Luka 12 : 37 –
38 – heri
watumwa wale ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha
Hapa Mungu anataka tujifunze juu ya Uaminifu katika
kumtumikia.
Uaminifu si jambo dogo bali ni kitu ambacho Mungu
huwa anakiangalia kwa uzito mkubwa sana kuliko hata tunavyofikiri.
Kulingana na kitabu cha Wagalatia 5 : 22, Uaminifu ni mojawapo ya tunda la Roho Mtakatifu
ambalo analiachilia anapoingia moyoni mwako.
Kwenye tafsiri nyingine katika Bibilia, uaminifu ni
sawa na kweli. Ile Zaburi 51 : 6
inasema hivi: Tazama wapendezwa na kweli iliyo moyoni.
-
Lile neno kweli maana yake uaminifu.
Ukisoma vizuri hiyo mistari utagundua kitu pale
ambacho ni hiki: mtumwa anayeongelewa hapo au wakili anayetajwa hapo hakuachwa
bila kazi bali alipewa kitu cha kufanya.
-
Na moja ya mjukumu aliyopewa ni kuhakikisha anawapa watu wa nyumbani
hapo chakula kwa wakati au anatoa posho kwa wakati
-
Lile neno “kwa wakati”
tafsiri yake ni kwamuda uliokusudiwa. Hivyo elewa kwamba kazi uliyopewa ina
muda wake wa kufanyika.
-
Na kama itaonekana hakufanya kazi kama alivyoagizwa kufanya basi
atapata adhabu ya kuwekwa kundi moja na wasioamini japokuwa alikuwa ameamini.
Kanisa la Mungu tunatakiwa tujue ya kwamba Mungu
ndiye aliyetuweka nyakati hizi, na ametuweka kwa makusudi. Na kama amekuweka
kwa makusudi basi anachokitaka ni wewe kulitimiza kusudi lake.
Watu wengi si waaminifu linapokuja swala la
utumishi.
-
Unaweza ukakuta wapendwa hawana muda wa kuomba kwa uaminifu, wala
kusoma Neno, wala kuhudhuria katika ibada za kanisani.
-
Na baadhi yetu tunadhani kuwa maombi ni kazi ya kikundi cha maombi tu
kilichopo kanisani halafu watu wengine maombi hayawahusu.
-
No! Hiyo sio sawa. Maombi ni jukumu la kila mmoja wetu.
Mungu anachotaka ni sisi kuwa waaminifu katika kutumika
mbele zake.
-
Kumbuka kwamba kila mtu anayo kazi aliyopewa kufanya hapa duniani.
Hakuna mtu asiye na kitu cha kufanya.
-
Hivyo Mungu anataka tufanye kazi kwa uaminifu wala si kwa kutegea wala
kwa ulegevu bali kwa bidii tukijua hatuna muda mwingi wa kukaa hapa duniani.
Biblia inasema mtumwa mwaminifu ni Yule ambaye
atawapa watu chakula kwa wakati wake maana yake ni kwamba mtumwa huyo atatenda
kwa busara kulingana na wakati alio nao.
Mtumwa mwaminifu ni mtu Yule anayefanya kazi ya Mungu
kama Mungu anavyotaka lakini mtumwa mbaya ni mtu Yule anayefanya kazi ya Mungu
isivyostahili (ni muongo, mlegevu, si mkweli, hawapi watu chakula kwa wakati
n.k)
Na Biblia inaweka wazi kabisa kuwa iko adhabu juu ya
Yule mtumwa asiye mwaminifu kwamba atawekewa fungu lake pamoja na watu
wasioamini. Hii inamaanisha kuwa japokuwa alikuwa ameamini lakini atawekewa
fungu lake pamoja na watu wasioamini.
Hivyo usije ukatumika kiholela au kwa ulegevu
ukidhani ya kuwa Mungu haoni!
NB: Nyakati hizi ni nyakati
ambazo kuna nguvu kubwa sana za upotevu, yaani watu watasongwa na mambo ya
duniani kuliko kawaida na ndio kipindi ambacho badala ya watu kuweka nguvu
kubwa katika kumtafuta Mungu, wataweka nguvu kubwa katika kupambana na hali zao
za maisha.
-
Kumtafuta Mungu itakuwa ni kama swala la ziada, bali watu watasumbukia
sana maisha yao.
-
Lakini Biblia imekwisha tuonya mapema ya kwamba “tafuteni kwanza ufalme
wa Mungu na haki yake ndipo hayo mengine mtazidishiwa” – Mathayo 6 : 33
-
Shetani anajua ya kuwa muda wake wa kufanya kazi ni mchache sana na
ndio maana anaachilia kila aina ya mambo mapya duniani ili kuzidi kuwateka
kifikra wanadamu wazidi kumsahau Mungu wafuate mambo yao wenyewe.
Ni maombi yangu kuwa kanisa liinuke na kusimama
katika zamu yake. Watu wa Mungu wajue kuwa muda tulionao ni mfupi sana.
-
Tusilale kama wengine walalavyo bali tukeshe tukimngojea Bwana wetu ili
tusije tukaachwa.
MUNGU
WA MBINGUNI AKUBARIKI SANA!!!
No comments:
Post a Comment