KUKUZA KIPAWA CHA UONGOZI NDANI YAKO

 Msisitizo: Somo hili litakusaidia kujua mambo yatakayokuza na kuchochea kipawa cha uongozi ndani yako.

Katika somo hili tutalenga zaidi juu ya mtazamo (altitude) alionao mtu unavyoweza kumsaidia au kumuondolea kipawa cha uongozi ndani yake.

 

Ipo tofauti kati ya mtu anayeongoza na mtu anayeongozwa.

-          Kinachowatofautisha ni mtazamo (altitude)

-          Mtazamo ndio unaofichua viongozi katikati ya kundi

-          Kiongozi anaona jambo kwa namna ya tofauti na wale wanaoongozwa wanavyoliona jambo hilo

 

TUANGALIE JAMBO HILI LA MTAZAMO WA UONGOZI KWA KUPITIA MIFANO YA HAWA VIUMBE WAWILI:

1.     Mfano 1: Ndege Tai (Eagle)

Tai ni ndege mfalme katika ndege wote wanaoruka na wasioruka. Na ana sifa tofauti sana ukilinganisha na ndege wengine. Sifa hizo ndio zinazompa upekee wa kujifunza kitu cha uongozi ndani yake.

Kuna mambo ambayo ndege karibuni wote wanafanana kama vile kupaa hewani, kutaga mayai, kujenga viota n.k lakini pia kuna sifa walizonazo hawa ndege ambazo zinawafanya wawe na utofauti kutoka jamii moja ya ndege na jamii nyingine.

 

Baadhi ya sifa za tai zinazoonyesha sifa za uongozi ndani yake

a.      Tai ni ndege anayeruka juu zaidi kuliko ndege wote

Tai anaruka juu zaidi kwa sababu hataki kuchangamana na ndege wengine ambao sio level yake (viwango vyake)

-          Tai ni ndege ambaye yuko makini katika kuchagua aina ya company au marafiki

-          Tai anaporuka juu hategemei kukutana na ndege mwingine isipokuwa tai mwenzake. Tafsiri yake ni kwamba tai hawezi akachangamana na marafiki wasiomsaidia (wasiokuwa level zake)

Vivyo hivyo kiongozi ni lazima na ni muhimu kuwa makini sana katika kuchagua aina ya marafiki au watu wake wa karibu.

NB: Kuna aina ya marafiki au watu ambao hutatakiwa kabisa kuwa nao kama watu wako wa karibu, kwa sababu wanaweza kuharibu kile kilichopo ndani yako

 

1 Korintho 15 : 33 – msidanganyike, mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.

-          Mazungumzo mabaya yanaweza yakaletwa na washauri au marafiki ulionao kwenye maisha yako.  

-          Kuna viongozi wameshindwa kufanya mambo makubwa, sio kwa sababu wao ni viongozi wabaya bali ni kwa sababu wana marafiki wasiowasaidia

-          Wanasaikologia wanasema – ukitaka kujua tabia ya mtu basi angalia aina ya marafiki wanaomzunguka huyo mtu utagundua tabia yake

-          Viongozi wengi wana marafiki ambao ni watu waliokata tamaa, wenye mtazamo wa kushindwa, wasioona mbali

-          Hao marafiki wa aina hiyo wana mchango mkubwa sana katika kuharibu mtazamo wa uongozi  ndani yako.

-          Ndio maana tai huwa ana tabia ya kuruka juu sana ambapo atakutana tu na tai wenzake – maana yake atakutana na wenye mtazamo unaofanana na wa kwake.

 

b.      Tai ni ndege anayependa dhoruba au tufani (storm)

Huyu ndege huwa anapenda sana dhoruba kwa sababu humsaidia kwenda kwa kasi zaidi hewani

-          Tai anapokutana na dhoruba angani ndio muda anaojiachia vizuri katika mwendo huo wa upepo wa dhoruba, na huo upepo humsaidia aruke juu zaidi

-          Kwa hiyo hutumia dhoruba kwenda mbali zaidi angani. Ni tofauti na wanyama au ndege wengine ambao huwa wanaogopa wanapokutana na dhoruba lakini tai huifurahia dhoruba hiyo.

Kiongozi unatakiwa usiogope changamoto unazokutana nazo bali uzitumie changamoto hizo kama ngazi ya mafanikio yako

-          Watu wengi waliofanikiwa si kwamba hawakukutana na changamoto bali waliziona changamoto walizopitia kama ngazi ya kuelekea kwenye mafanikio yao.

-          Kiongozi unapokutana na changamoto yoyote, mtazamo unaotakiwa kuwa nao ni lazima uwe ni tofauti na wale wanaoongozwa wanapokutana na changamoto ya namna hiyo.

-          Mtazamo wa anayeongozwa ukifanana na mtazamo wa anayeongoza basi sifa ya uongozi inapotea.

1 Samweli 17 : 8 – 11, 16, 23 – 24, 31 – 37

-          Daudi alipokutana na Goliathi hakutishika na urefu aliokuwa nao, wala ushujaa wa vita aliokuwa nao, bali mtazamo wake juu ya ushindi katika magumu ndio uliomsaidia kupigana na Goliathi.

-          Unajua Biblia imeeleza jinsi Goliathi alivyokuwa mrefu, silaha za vita alizokuwa nazo, ujuzi na ushujaa wa kivita aliokuwa nao na idadi kubwa ya wanajeshi waliokuwa pamoja naye; lakini vyoote hivyo havikumtisha Daudi asiweze kupigana naye.

-          Daudi hakuwa na uzoefu wa kupigana vita wala kutumia silaha za vita, kwa kifupi hakuwa na sifa yoyote ya kwenda vitani na hasa kupigana na mtu hodari kama Goliathi lakini imani aliyokuwa nayo juu ya mtazamo wake ndivyo vilivyomsaidia kupigana.

-          Daudi alijiona anaweza akashinda ile vita hata kama hana vigezo vya kupigana katika vita hiyo.

-          Kwa wana wa Israel, vile vita vilkuwa ni tatizo kubwa sana kiasi kwamba walikaa karibia siku arobaini  usiku na mchana bila kwenda vitani wakimuogopa Yule Goliathi, lakini kwa Daudi vile vita vilikuwa ni fursa (mstari wa 26).

 

Kiongozi ni lazima ujue kubadilisha changamoto kuwa fursa (Leaders must know how to see challenges into opportunities)

Watu wengi wanakwama hata kuendelea na uongozi walionao mahali Fulani kutokana na changamoto wanazopitia.

-          Mungu hakumpitisha Daudi ili akutane na simba au dubu ili auawe bali wamuimarishe mtazamo wake wa uongozi ndani yake ndio maana hata alipokutana na Goliathi hakupata shida kwa sababu alikwisha pitishwa kwenye shule ya kuimarisha msimamo wake wa kuona changamoto kuwa fursa kwake.

-          Na hapo ndipo utakapojua kuwa wakati mwingine Mungu anaweza akaruhusu magumu yakujie kwenye maisha yako kwa ajili ya kukutengeneza uwe kiongozi mzuri baadae.

-          Ukipitia changamoto sasa, haimanishi kuwa hautapitia changamoto baadae bali utapitia tu changamoto zingine. Hivyo changamoto za sasa zinatakiwa zikuimarishe na zikusaidie kupambana na kukabiliana na changamoto utakazopitia baadae.

 

 

c.       Tai ni ndege mwenye msimamo katika mtazamo alionao (focus)

Hapa tunongelea swala la msimamo katika mtazamo ulionao juu ya jambo Fulani.

-          Tai huwa anatabia ya kwenda juu sana angani na kwa sababu hiyo huwa anauwezo wa kuona vitu vingi sana vilivyo chini ardhini. Na mara nyingi huwa anayaona mawindo yake akiwa huko angani na kupelekea kuyakimbiza kwa kasi zaidi bila kuyumbishwa na chochote na anahakikisha ni mpaka anayakamata.

-          Tai anapokusudia kuwinda kitu Fulani huwa haruhusu kitu chochote kimpotezee lengo alilonalo juu ya kuwinda anachowinda.

-          Na ndio maana huwa anashuka kwa kasi kubwa ili mawazo yake na macho yake yasitazame kitu kingine bali yatazame mawindo yake tu.

Na kiongozi unatakiwa kuwa na msimamo katika mtazamo ulionao juu ya mambo unayoyashughulikia kama kiongozi.

-          Kwa sababu unaweza ukaletea wazo na Roho Mtakatifu ndani yako kwamba ufanye hiki na kile lakini wale ulionao wakaona labda ni vigumu kwa jambo hilo kutekelezeka, hivyo wakataka kukushauri vinginevyo. Unachopaswa kufanya ni kusimamia msimamo wako (na hili ni kama una uhakika kwamba wazo hilo au jambo hilo ni kusudi la Bwana)

Kutoka 14 : 10 -14, 15 – 16

-          Hizi ni habari za Musa na wana wa Israel wakati wametoka nchi ya Misri kuelekea Kaanani, walipofika kando ya bahari ya Shamu hawakujua nini cha kufanya. Mbele yao kulikuwa na bahari, kulia na kushoto kwao kulikuwa na milima, na nyuma yao kulikuwa na jeshi la Farao ; kwa hiyo wakaogopa sana  kiasi cha kukata tamaa na kutaka kurudi Misri.

-          Musa ndiye aliyekuwa kiongozi na wana wa Israel walikuwa wanamlilia yeye juu ya shida yao waliyokuwa nayo. Walimwambia kuwa wanataka kurudi Misri maana yake waende kinyume na agizo la Mungu alilopewa Musa. Kama Musa asingisimama imara katika msimamo wake basi wasingesonga mbele.

Kiongozi unatakiwa ujifunze kusimamia kile unachokiona kwa sababu kile unachokiona ndicho Bwana anachotaka ukifanye.

-          Kiongozi ni mtu jasiri ambaye ana uwezo wa kusimamia anachokiamini.

 

 

 

 

2.     Mfano 2: Simba

Simba ni mfalme katika jamii ya wanyama wa msituni na porini.

-          Lakini tukiangalia uhalisia ni kwamba simba sio mnyama mrefu kuliko wanyama wengine, na wala sio mzito au mnene kuliko wanyama wengine na pia sio mnyama mwenye akili zaidi kuliko wanyama wengine lakini ndio “king of the jungle”- mfalme wa porini.

-          Ile kwamba anakosa sifa za kuwa si mrefu kuliko wote, si mzito kuliko wote, au sio smart kuliko wote hamzuii yeye kuwa mfalme wa porini.

-          Kuwa kiongozi sio swala la kuwazidi watu sifa za kimwili (urefu, unene, ujanja, ujuzi, elimu n.k) bali ni swala la mtazamo (altitude)

-          Kwa mantiki hiyo ni kwamba simba ame-cancel visingizio vyote (execuses) vya mtu kuwa kiongozi. Kwa hiyo mtu hawi kiongozi kwa sababu ya sura ya nje bali kwa mtazamo alionao.

-          Mtazamo unaweza ukakufanya uwe kiongozi au la.

 

¨      Hebu tuangalie mfano huu:

Simba anapotokea porini akimuona tembo, haogopi ukubwa wa tembo, wala haogopi  nguvu za tembo bali kinachokuja akilini mwake ni kwamba huyu tembo ni chakula.

-          Lakini pia temo naye anapomuona simba porini haijalishi kwamba ana umbo dogo kuliko yeye, au hana nguvu kama yeye bali kinachokuja akilini mwake ni kwamba hapa naweza kuliwa

 

Ø  Kinacho watofautisha hawa wanyama wawili ni mitazamo yao.

-          Mtazamo ulionao unaweza ukakufanya ujione ni mdogo sana hata kama kiuhalisia si mdogo

Hesabu 13 : 1 -2, 25, 27 – 33

-          Waliotumwa kuipeleleza nchi ya Kaanani walikuwa ni viongozi wa kila kabila.

-          Viongozi wawili (Yoshua na Kalebu) kati yao ndio waliokuwa na mtazamo tofauti na wenzao. Ni kweli wote walikuwa ni viongozi lakini walikuwa na mitazamo tofauti.

Mtazamo unatokana na kile unachokiamini (your altitude is produced from your belief. You can’t have altitude beyond your belief)

-          Kile unachokiamini ndicho kinatengeneza mtazamo ndani mwako. Kama unaamini katika kushindwa huwezi ukawa na mtazamo wa kushinda.

-          Na unakuta wakati mwingine mtu unakuwa ni wa kusema tu siwezi kufanya hiki, au siwezi jambo fulani, siwezi siwezi siwezi… hali hiyo itakupelekea kutokuwa na mtazamo wa kuweza hata siku moja.

 

NB: Jeshi la kondoo linaloongozwa na simba linaweza likawashinda jeshi la simba linaloongozwa na kondoo.

-          Tofauti ya haya majeshi mawili ni viongozi wao ambao hiyo tofauti imetokana na mitazamo yao.

Kwa mfano katika mechi ya mpira wa miguu, timu inayofungwa mara nyingi hawalaumiwi wachezaji bali analaumiwa kocha.

Kwa nini?

-          Kwa sababu wachezaji wanacheza mpira kwa akili za kocha wao. Na ndio maana timu inapofungwa huwa hawawafukuzi wachezaji bali wanamfukuza kocha.

Kiongozi anaweza akafanya kundi likafanya vizuri au vibaya.

Na ni muhimu sana kujua kwamba kiongozi unatakiwa uone mbali zaidi ya unaowaongoza wanavyoona.

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...