NAMNA YA KUMTWIKA YESU FADHAA ZAKO ILI AKUSAIDIE

 Lengo la somo: Ni kukusaidia uweze kwenda mbele za Mungu kwa njia ya maombi na kujielezea mwenyewe kuhusu shida uliyonayo ili Mungu aweze kukusaidia.

Somo hili limelenga zaidi kwa mtu binafsi kupata muda wa kwenda mbele za Mungu kwa ajili ya kumwambia Mungu hali yake ya kiroho ambayo imeharibiwa na mazingira au tabia yake ya kimwili na imekuwa ni vigumu sana kwa huyo mtu kuiacha hiyo tabia au kuyaepuka hayo mazingira.

1 Petro 5 : 6 – 7

“Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari ili awakweze kwa wakati wake, huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.”

Hii sentensi ni sentensi inayotujulisha juu ya upendo wa Mungu wetu kwenye maisha yetu, ya kwamba Yeye anahusika sana na maisha yetu.

-          Kwa tafsiri nyingine ni kwamba, Chochote kinachohusu maisha yangu, Mungu wangu anahusika nacho, hata kama ni jambo linalosumbua moyo wangu bado Mungu anahusika nalo.

-          Maana yake ni kwamba Mungu anataka umshirikishe mambo yako, usiyashughulikie mwenyewe mwenyewe tu bali umshirikishe ili akusaidie. Yeye ndiye anayejua namna ya kukusaidia.

Maana ya fadhaa:

-          Fadhaa ni jambo lolote au hali au tabia uliyonayo inayohusu maisha yako lakini linakuletea usumbufu au mahangaiko moyoni mwako. Unakosa kuwa na utulivu wa ndani. Moyo wako unapata shida wa namna ya kulitatua

-          Inawezekana ikawa ni tabia fulani ambayo umejaribu sana kuiacha lakini bado unaifanya, unajijua kabisa umeokoka lakini kuna hiyo tabia imekuwa ni vigumu sana kwako kuiacha; sio kwamba unaipenda bali ni kwamba umejaribu sana kuiacha lakini bado umeshindwa.

-          Fadhaa inaweza ikawa ni jambo la kimaisha ambalo limekusumbua kwa muda mrefu na umejaribu kuliombea na kuwashirikisha watumishi wa Mungu wengine wakuombee lakini bado halijaondoka au kulipatia ufumbuzi;

-          Wakati mwingine inawezekana ikawa ni hata ugonjwa fulani ambao umekuwa ukikupata mara kwa mara na umeukemea mpaka umeona ni kama tu ugonjwa wako;

 

¨      Yote hayo yanakuletea mahangaiko moyoni mwako, unapata hofu au mashaka, na hali hiyo inasababisha moyo wako kutopata utulivu

-          Ukiona jambo lolote kwenye maisha yako linakuletea mahangaiko moyoni mwako, na unakosa kuwa na utulivu wa ndani basi ujue hilo jambo linaitwa “Fadhaa”

 

Mahali pengine kwenye Biblia imeeleza kwa tafsiri nyingine iliyo nyepesi zaidi.

Mathayo 11 : 28 – 30 – “Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha, ….. , kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi”

-          Angalia yale maneno “kusumbuka” na “kulemewa” yana maana ya kwamba moyoni mwako unapata mahangaiko na unakosa kuwa na amani ya moyo na utulivu wa ndani unapotea kabisa

-          Mizigo anayoongelea hapa maana yake ni mambo yanayosumbua moyo wako.

-          Ndani mwako kunakosa utulivu, kunakuwa na mahangaiko yanayosababisha moyo wako kulemewa.

-          Mizigo haimaanishi tu dhambi peke yake, (mzigo unaweza ukawa ni dhambi au jambo lolote ambalo linakufanya uwe umelemewa moyoni mwako na linakusumbua).

 

รจ Kwa hiyo inawezekana ikawa ni aina fulani ya tabia ambayo haimpendezi Mungu lakini bado unayo japokuwa umeokoka lakini umeshindwa kuiacha. Umejitahidi ulivyoweza lakini bado umeshindwa kuiacha. Na kwa sababu umeokoka imekuwa ni vigumu hata kumwambia rafiki yako ili muombe pamoja juu ya hilo jambo kwa sababu unaona aibu labda atakuona kama haujaokoka vile.

-          Ikitokea mnashirikishana ajenda binafsi za kuombeana basi utamshirikisha mwenzio ajenda nyingine nyingine zinazohusu labda uchumi wako au matatizo ya familia yako lakini kuna mambo yako binafsi hutoweza kumshirikisha mtu mwingine.

-          Kwa mfano, wapo watu waliookoka lakini bado ni waongo, wambeya, wazinzi, wakorofi, wenye hasira mbaya, wasiosamehe kirahisi, n.k sio kwamba wanapenda kuwa na hizo tabia bali wamejaribu kuzishughulikia wenyewe na wakashindwa.

-          Na kibaya zaidi ni kwamba watu wengi wanadhani pale wanapookoka tu basi kila kitu kwenye maisha yao kinaanza kwenda vizuri bila wao kuomba kwa bidii na kwa juhudi. Hapana. Unatakiwa ujue namna ya kushughulikia tabia au mambo ambayo yapo kwenye maisha yako kwa kutumia msaada wa Mungu aliye upande wako. Kabla ya kuokoka Mungu hakuwa upande wako lakini baada ya kuokoka Mungu anakuwa upande wako.

Watu wengi wanadhani kwa sababu Mungu anawaona na anajua shida zao basi hawahitaji tena kwenda mbele za Mungu na kujielezea juu ya mambo yanayowalemea na kuwaangasha mioyo yao.

Unajua ni hali ngumu sana kwa mtu kujijua umeokoka lakini bado kuna vitabia unavyo na havimpendezi Mungu na umeshindwa kuviacha kabisa. Umekuwa ukijiombea mara kwa mara lakini havikuachilii.

Kwa kiingereza tunasema “addicted”. Yaani jambo umelizoea kulifanya sana hata kama unajua sio jema lakini unashindwa kuliacha. Mfano kuwa na hasira.

-          Hali hiyo imekuwa ikiwatesa sana watu hata wasisonge mbele kiroho, kwa sababu muda mwingi wamekuwa wakishughulikia kuombea jambo hilo hilo tu kila siku na wakati mwingine wamekata tamaa na kudhani kuwa hiyo hali ndiyo wameumbiwa wakae nayo.

 

NB: Mizigo sio tu dhambi bali hata mambo yako ya kifamilia au ndoa yako au biashara yako ambayo hayaendi vizuri na yamekuletea shida mpaka moyo wako ukalemewa. Kuna watu wanatafsiri kuwa mzigo ni dhambi peke yake, lakini si kweli. Kuna mizigo ambayo ni dhambi na kuna mizigo ambayo sio dhambi lakini inakulemea.

Kwa sababu Biblia inatuambia kwamba tunapokwenda kwa Yesu kutua mizigo inayotulemea basi na Yeye anatupa mzigo wa kwake ambao ni mwepesi.

-          Hivyo, kwa Yesu tunatua mizigo inayotulemea halafu tunapata mzigo usiotulemea.

Mungu anapokuambia “njoo” maana yake anakupa mwaliko wa kwenda mbele zake ili ueleze mambo yako upate msaada wake. Ukinyamaza hutopata msaada wake

Ukisoma kile kitabu cha Mithali 28 : 13 – Afichaye dhambi zake hatofanikiwa bali yeye aziungamaye atapata rehema.

-          Kuungama maana yake ni kueleza kile kinachokusibu. Yaani kueleza mambo yako kwa Mungu au kwa mtu kwa lengo la kupata msaada.

-          Kuna madhehebu mengine yameweka utaratibu wa kuungama dhambi au makosa yao  kwa viongozi wao wa kidini (nayo sio mbaya).

-          Lakini Biblia inatuambia Yesu ametufungulia njia bora na hakika zaidi ambayo inatupa nafasi ya kwenda mbele za Mungu na kuungama dhambi zetu. Ndio maana wakati Yesu Kristo anakufa msalabani, pazia la hekalu lilipasuka ili kuwa ishara ya kwamba sasa kila mtu anayo nafasi ya kwenda mbele za Mungu moja kwa moja kwa njia ya damu ya Yesu Kristo.

Mimi ninachotaka uone hapa ni lile neno kuungama kwa tafsiri ya kwamba unajielezea mambo yako mwenyewe kwa Mungu.

 

 

MAMBO YA MSINGI AMBAYO MUNGU ANAYAANGALIA KWAKO UNAPOKWENDA MBELE ZAKE KUTAKA MSAADA

Sasa yako mambo ya msingi sana unayopaswa kuyajua ambayo Mungu huwa anataka ayaone kwako unapoamua kwenda mbele zake kutaka msaada. Mamo yenyewe ni hayo yafuatayo:

1.     Mungu anataka aone kama unajua shida uliyonayo

Je, wewe mwenyewe unajijua kama unashida? Hapa ni swala la ufahamu wako juu ya shida uliyonayo.

Unajua kuna watu wana shida lakini hawajijui kama wana shida. Kwa hiyo ni vigumu sana kuwasaidia kwa sababu hawajijui kama wana shida.

Marko 10 : 46 – 52 – ni habari ya mtu mmoja aliyekuwa kipofu na alikuwa akiomba omba kando ya njia. Mambo ambayo yamenishangaza kwenye hii stori ni kwamba:

-          Kulikuwa na mkutano mkubwa ukimfuata Yesu (na inawezekana walikuwa wanapiga kelele kwa sababu walikuwa wanatembea, hawawezi kutembea kimya) lakini huyu kipofu aliweza kumwita Yesu mpaka Yesu akasikia na akamwitikia.

-          Lakini sasa cha ajabu ni kuwa Yesu alimuuliza kipofu Yule kuwa unataka nikufanyie nini? Unajua swali kama hilo ungeweza kufikiri kuwa Yesu alikuwa hayuko serious, wakati anamuona kabisa kuwa huyo jamaa ni kipofu, anamuuliza unataka nikufanyie nini. Unaweza ukajiuliza ni kwa nini Yesu amuulize swali hilo wakati anamuona kabisa kuwa ni kipofu?

¨      Jibu ni kwamba, Yesu alitaka aone kuwa Yule kipofu anajua shida aliyonayo au la. Kwa sababu uweza wa kumponya alikuwa nao lakini kwanza alitaka ajue kwamba huyu kipofu anajua shida aliyonayo au vipi.

-          Huyu kipofu alikuwa anajua shida yake ndio maana alijibu kuwa anataka apate kuona. Na ujue ya kwamba huyu kipofu hakusubiri afike kwenye eneo la mkutano bali pale pale njiani alitaka Yesu amponye.

-          Na pia haikumaanisha kuwa hakuwa na shida nyingine bali hiyo ndiyo aliyoipeleka kwa Mungu na akapata msaada.

Wako watu wengi sana ambao hawajui kama wana shida na ndio maana hawapati muda mwingi wa kujiombea. Na hata kama wakijiombea huwa wanaombea mambo ya kawaida tu lakini mambo yale ya ndani yanayowasumbua mioyo yao huwa hawayaombei.

-          Na kinachowafanya wasiombe ni ile dhana kwamba Yesu anatujua shida zetu kwa hiyo wanadhani Yesu atazishughulikia mwenyewe bila wao kumwambia.

-          Bwana Yesu hashughulikii jambo usilomwambia, japo yapo ambayo anatufanyia hata kama hatumwombi kwa sababu yeye ni Baba yetu, na sisi ni watoto wake.

-          Kuna watoto wakubwa na wadogo. Watoto wadogo watafanyiwa vitu na baba yao hata kama hawajamuomba lakini kwa watoto wakubwa hawafanyiwi mpaka wamuombe baba yao. Ndivyo ilivyo kwa Mungu.

Kile kitabu cha Isaya 43 : 26 – Biblia inasema “Unikumbushe na tuhojiane, eleza mambo yako upate kupewa haki yako.”

-          Ni muhimu ukajua kuwa kuna swala la kujielezea mbele za Mungu.

-          Ni kweli anajua shida zako lakini anataka uendelee kumkumbusha, maana yake anataka aone hilo jambo unahitaji msaada wake kwa kiwango gani.

-          Unavyomkumbusha mara kwa mara ndivyo anavyoona kuwa unajijua kwamba una shida na unahitaji msaada.

Wafilipi 4 : 6 – “… haja zenu na zijulikana na Mungu”

-          Mungu anataka haja zetu zijulikana mbele zake. Sasa hiyo haimaanishi kuwa hazijui bali anataka aone kuwa unajijua kuwa una shida fulani?

 

2.     Mungu anataka aone kuwa unahitaji msaada wake juu ya shida uliyonayo.

Kuna watu wanashida lakini hawahitaji msaada wa kutoka kwenye shida walizonazo.

Luka 9 : 11 – “… akawaponya wale wenye haja ya kuponywa”

-          Watu waliomfuata Yesu walikuwa ni makutano mengi, kila mtu alikuwa ana shida yake. Na Yesu alikuwa anazo nguvu za kuwaponya wote na kutatua shida ya kila mtu lakini waliofanikiwa kupata uponyaji kutoka kwa Yesu walikuwa ni wale waliokuwa na haja ya kuponywa tu.

-          Maana yake ni kwamba, kuna watu tutakutana nao kanisani siku zote na atakuja na shida yake na ataondoka na shida yake pia. Kwa nini? Kwa sababu tu, hana haja ya kuponywa.

-          Na inawezekana kule kutokuwa na haja ya kuponywa kunatokana na kutojijua kama una shida ndio maana huna haja ya kuponywa.

-          Unajua mpaka Biblia imeandika hivyo kuwa waliponywa wale wenye haja ya kuponywa, inamaanisha kuwa Mungu anataka tuone msisitizo alionao tunapokwenda mbele zake.

-          Makutano walikuwa wengi na wenye shida walikuwa ni wengi lakini walioponywa walikuwa ni wachache.

Shetani anaweza akakuruhusu kwenda kanisani na ukasikiliza Neno la Mungu vizuri lakini asikuruhusu upate uponyaji kutoka kwa Mungu. Kwa sababu anakufunga ufahamu wako usijijue kuwa una shida, na ya kwamba unataka kutoka kwenye hiyo shida.

Ushawahi kuona mtu anakunywa pombe au anavuta sigara na anajua madhara yake lakini haitaji kuacha? Unadhani ni kwa nini? Ni kwa sababu shetani amefunga ufahamu wake huyo mtu asijijue kuwa yuko kwenye shida, na hivyo hawezi akataka msaada wa kutoka kwenye hiyo shida.

Kwa mfano, wana wa Israeli walitembea jangwani miaka 40. Sasa kuna watu waliozaliwa kule Misri kwenye nchi ya utumwa kwa hiyo wanajua kuwa utumwa ndio maisha yao ya kawaida, na kuna wengine waliozaliwa jangwani hawajui utumwa ukoje na hawajui Nchi ya Kanani ikoje, kwa hiyo wanadhani maisha ya kuhamahama ndio maisha yao ya kawaida.

-          Mtu wa namna hiyo ambaye haoni kama kwenye maisha yake kuna shida fulani hawezi akahitaji msaada wa kutoka kwenye hiyo shida, kwa sababu haioni.

-          Ndio maana ni muhimu sana kwanza ujijue kuwa upo kwenye shida fulani ndipo utake msaada wa kutoka kwenye hiyo shida.

Mfano mwingine ni kwamba, inawezekana wewe umeokoka lakini una shida ya kusamehe wengine.

-          Sasa kama hujajua kuwa kutokusamehe kunaharibu moyo wako na maisha yako ya kiroho, basi hutohitaji msaada wa Mungu wa kukusaidia kukuondolea hiyo tabia ya kutokusamehe.

Mfano wa mwanamke Msamaria - Yohana 4 : 4, - 11 – 18, - 42

Hizi ni habari za mwanamke msamaria ambaye alikutana na Yesu kisimani.

-          Ule mstari wa 14 unaonyesha kuwa Yesu alikuwa anajua shida aliyokuwa nayo Yule mwanamke msamaria ndio maana alikuwa amemwambia juu ya suluhisho la shida yake kwamba ni maji ya uzima kutoka wa Yesu

-          Yule mwanamke alikuwa na shida ya tamaa au tabia ya zinaa ndio maana alipomuomba Yesu ampe hayo maji ya uzima, ndipo Yesu alipomwambia akamlete mume wake. Yesu alikuwa anajua kuwa huyu mama hana mume wa kweli.

-          Kwa tafsiri nyingine ni kwamba Yesu alikuwa anataka aone kuwa huyu mama kama anajijua shida aliyonayo au hajijui. Cha ajabu ni kwamba Yule mwanamke alikuwa anajijua shida yake, lakini hakuwa anahitaji msaada kwa wakati ule, ndio maana alikuwa mwepesi wa kubadilisha topiki yake ya swala la wanaume aliokuwa nao na akamuuliza Yesu juu ya swala la mahali pa kuabudu (mstari wa 19 na 20).

-          Tunaona kabisa kwamba huyu mama alikuja kuwa mwinjilisti mzuri wa kuwaleta watu waje kusikiliza mahubiri ya Yesu lakini yeye hatujaona mahali popote kama alikuja kuponywa shida yake.

-          Ukisoma vizuri kwa makini ule mstari wa 4 unasema kuwa Yesu alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria, na pia utaona kuwa maongezi ya Yesu na Yule mwanamke yameelezwa kwa kirefu kuliko kile alichokifundisha Yesu kwa watu wa Samaria. Hapo utajua kuwa kulikuwa na upako mahususi kwa ajili ya Yule mwanamke msamaria ili aponywe shida yake lakini mwanamke Yule hakuwa na haja ya kuponywa.

Kuna watu ambao wako makanisani na wanajijua kabisa kuwa wana shida mbalimbali lakini hawana haja ya kuponywa. Na usidhani kwamba Mungu atakulazimisha akuponye, Wala!! Hakulazimishi. Mungu anachokifanya ni kukupa mwaliko uende kwake ili  akutue mizigo yako inayokulemea ili upate kupumzika. Lakini ukikataa kwenda hatokulazimisha bali atakuacha uendelee kuteseka na mizigo yako. Unaendelea kuteseka wakati msaada wa kukusaidia usiteseke unao.

 

3.     Mungu anataka aione imani uliyonayo kwake ya kupata msaada juu ya shida uliyonayo.

Imani huwa inatangulia kabla ya maombi yako au moyo wako. Unapokwenda mbele za Mungu kuomba jambo lolote, kinachotangulia kuonekana mbele za Mungu sio maombi yako wala moyo wako bali ni imani iliyoambatana na hayo maombi yako.

Biblia inasema katika Waebrania 11 : 6 – Pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu.

 

Baadhi ya mifano:

Marko 2 : 1 – 5Alipoiona imani yao

Luka 5 : 17 – 20 - … Uweza wa Bwana ulikuwapo pale ili apate kuponya… alipoiona imani yao

-          Walikuwapo watu wengi wanamsikiliza Yesu mahali pale na Biblia inatuambia kuwa kulikuwapo na uweza wa Mungu mahali pale ili apate kuponya lakini hakukuwa na mtu mwenye imani iliyovuta huo upako wa uponyaji mpaka walipokuja wale waliombeba Yule mtu kwenye godoro ndio waliokuwa na imani ya kuvuta ule upako wa uponyaji.

-          Na cha ajabu ni kwamba baada ya Yesu kumponya Yule mtu akaondoka zake, maana yake hadi mahubiri yakaisha (mstari wa 27).

-          Hatujaambiwa ni kitu gani alichokifundisha mahali pale bali tunaelezwa jinsi Yule mwenye kupooza alivyoponywa.

Hapa tunapata kujua jambo lingine kuwa unaweza ukajijua shida uliyonayo na pia ukawa na haja ya kuponywa shida uliyonayo lakini ukawa huna imani ya kukusaidia kuvuta upako wa uponyaji ndani ya Yesu ili kukusaidia.

NB: Imani imebeba address yako (anuani yako), ndio maana unaweza ukai-connect kwa Mungu ili kuvuta nguvu za Mungu zije zikusaidie kwenye shida uliyo nayo.

-          Ndio maana Yule mwanamke aliyekuwa anatokwa na damu muda  wa miaka 12 (Luka 8 : 43 - 48) alipogusa tu pindo la Yesu akapokea uponyaji wake, lakini ukiangalia wako watu wengi waliomgusa Yesu kwa wakati ule na hawakupokea uponyaji wowote.

-          Yule mama alimgusa Yesu kwa imani lakini wale watu wengine hawakumgusa kwa imani.

-          Imani ilibeba address ya Yule mama ndio maana ilipeleka nguvu za Mungu za uponyaji moja kwa moja kwa Yule mama na sio kwa mtu mwingine.

-          Upako unafuata address iliyoko kwenye imani

-          Address (anuani) ni njia au maelekezo ya wapi na kwa nani upako uende.

-          Upako hautoki tu kiholela-holela bali unatoka kwa address ambayo ipo ndani ya imani.

Kwa hiyo imani ni kitu cha muhimu sana unapokwenda mbele za Mungu. Usipokuwa nayo basi huwezi ukapokea kutoka kwa Mungu.

Ukirudi kusoma vizuri kwenye hiyo mifano hapo juu utagundua kuwa kila mtu aliyekwenda kwa Yesu kutaka msaada wowote, kitu cha kwanza Yesu alichokiona ilikuwa ni imani yake, ndio maana alisema alipoiona imani yake, alipoiona imani yao, alipoiona imani yake ….!

-          Imani ndio inayotangulia kwanza kabisa mbele yako kabla ya maombi yako au moyo wako, kwa hiyo kama Yesu hatoiona imani yako basi si rahisi kukujibu maombi yako.

Lakini pia kuna watu wana imani lakini isiyo ya kutaka msaada kutoka kwa Mungu, wana imani ya kupata msaada kutoka kwa waganga wa kienyeji, kupata msaada kutoka kwa watu wenye uwezo, wengine wanategemea fedha au mali zao n.k.

-          Hawa watu unakuta wanajijua kuwa wana shida fulani na pia wanajua kabisa kuwa wanahitaji msaada wa kutoka kwenye hiyo shida lakini imani walionayo si kwa Mungu bali mahali pengine.

NB: Unachotakiwa kufanya ni kwamba nenda mbele za Mungu moja kwa moja halafu mweleze shida yako:

-          Mwambie Mungu kuwa mimi ni kweli nimeokoka lakini bado ni muongo, ili akusaidie uache uongo.

-          Mwambie Mungu kuwa ni kweli nimeokoka lakini bado nina tama ya zinaa, ili akate kiu yako ya tama

-          Mwambie Mungu ni kweli nimeokoka lakini bado ni mmbeya ili akuondolee tabia ya umbeya n.k.

-          Usiogope, nenda mbele za Mungu jielezee shida yako, jiweke wazi kwa Mungu juu ya jambo lolote linalokusumbua, naye atakusaidia

Kumbuka kwamba sio kwamba hajui shida yako bali anataka aone uhitaji ulionao wa msaada wake kwenye maisha yako.

Jambo la muhimu kuwa nalo makini ni kwamba moyo wako unawindwa na adui shetani ili akuletee uharibifu.

-          Usipojua namna ya kuulinda moyo wako itakuwa ni vigumu sana kujikinga na mashambulizi ya adui.

-          Biblia inasema Linda sana moyo wako kuliko yote uyalindayo – Mithali 4 : 23

-          Lakini pia zipo silaha mbalimbali za Kimungu tulizopewa ambazo ni za kujilinda dhidi ya mashambulizi ya adui. Ni vyema ukazitambua kuzivaa na kuzitumia silaha hizo.

 

NEEMA YA BWANA YESU KRISTO NA UPENDO WA MUNGU UKUFUNIKE UTAKAPOSOMA SOMO HILI, UPATE KUONGEZEKA NA KUKUA ZAIDI KATIKA KUMFAHAMU MUNGU WETU.

AMEN.

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...