Ni muhimu sana ukijua ya kwamba upo uhusiano kati sadaka
uliyoikusudia kuitoa mbele za Mungu na imani yako kwa Mungu huyo unayemtolea
hiyo sadaka.
Sadaka ni kama kibebeo mfano bakuli, kama ukipeleka sadaka
yako ambayo ni kibebeo mbele za Mungu halafu haina imani ni sawa na umepeleka
kibebeo kitupu.
Kwa sababu Mungu anaangalia kwanza imani kabla ya kuangalia
sadaka uliyoitoa.
Waebrania
11 : 4
“Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko
Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu akazishuhudia sadaka zake, na
kwa hiyo ijapokuwa amekufa angali akinena”
Angalia yale maneno “kwa imani”, halafu tuangalie mambo
yafuatayo:
i.
Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo- Ebrania 11 : 1
Kama Habili alitoa sadaka kwa imani basi kuna kitu alikuwa
anakitarajia akipate kutoka kwa Bwana wakati anatoa sadaka yake.
ii.
Chanzo cha imani ni kusikia neno la Kristo – Warumi 10 : 17
Na kama chanzo cha imani ni kusikia neno la Kristo, basi ujue
pia Habili kuna namna alisikia sauti ya Mungu ndani yake ikimuagiza atoe
sadaka.
Biblia haijatuambia walipata wapi agizo la kutoa sadaka
wakati ule, lakini wakati ule tunaona wote wawili wanakwenda kumtolea Mungu sadaka
zao. Na mmoja anapata kibali yeye na sadaka yake bali mwingine hapati kibali
yeye na sadaka yake
Mwanzo 4 :
3 – 7
Sadaka ya Habili ilikuwa imebeba imani ndani yake ndio maana
ilipofika mbele za Mungu aliifurahia lakini sadaka ya Kaini haikuwa imebeba imani
ndani yake. Kumbuka kuwa pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu. – Ebrania 11 : 6
Kwa hiyo tofauti ya sadaka iliyotolewa na Habili na Kaini
ilikuwa kwenye imani.
-
Na ni hatari sana kutoa sadaka bila imani, kwa sababu
imani ndio inayokupa kibali kwa Mungu na sio sadaka.
-
Watu wengi wanadhani watakubaliwa na Mungu kwa sababu
wanatoa sana sadaka. Na kwa sababu hiyo wanatoa kwa mazoea na kwa kufuata
mkumbo tu.
-
Sadaka yoyote haitolewi kwa mazoea wala kwa mkumbo
bali sadaka inatolewa kwa imani.
Imani ndio inayounganisha sadaka yako na moyo wako mbele za
Mungu.
-
Mungu akiingalia sadaka iliyobeba imani ndani ake
anauona moyo wako, kwa sababu ndani ya imani kuna tarajio, na hilo tarajio ndio
haja ya moyo wako.
Unapotoa sadaka mbele za Mungu pasipokuwa na imani ni sawa na
hauamini kuwa Yeye yupo na pia hauamini kuwa anaweza akaleta matokeo ya sadaka
uliyotoa, ndio maana anakuwa haifurahii hiyo sadaka. Kumbuka pasipo imani
haiwezekani kumpendeza Mungu na kila amwendeaye Mungu ni lazima aamini kuwa
yeye yupo.
Ukiangalia
ule mstari wa Mwanzo 4 : 3 – 7 unaona ya kuwa Kaini alikosa
kibali kutoka kwa Bwana sio kwa sababu ya kutokutoa sadaka bali ni kwa sababu
alitoa sadaka pasipokuwa na imani.
-
Ule mstari wa 7
unasema “kama ukitenda vyema hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko…”
-
Tafsiri yake ni kwamba Mungu alikuwa anamwambia Kaini
kuwa jambo lolote linalofanyika pasipo imani halimpendezi Mungu maana yake
linakuwa ni dhambi.- Warumi 14 : 23b
-
Hii inaonyesha kuwa Kaini hakutenda vyema bali
alitenda dhambi kwa kutoa sadaka bila imani ndio maana Mungu akamwambia kuwa
kama ukitenda vyema hutapata kibali?
-
Macho ya Mungu kabla hayajaitazama adaka uliyoitoa
yanatazama kwanza kilichobebwa ndani ya hiyo sadaka. Kwa hiyo kama sadaka yako
haina imani basi Mungu anakuhesabia kuwa hujafanya jambo jema. Maana yake
hapendezewi na hiyo sadaka yako. Hivyo hawezi akaikubali.
Sadaka pasipo kuwa na imani ni sawa na kuandika barua
isiyokuwa na address kwa hiyo haijulikani inakwenda kwa Mungu yupi, hivyo usitegemee
kupata majibu.
Sadaka inaweza ikabadili mfumo wa maisha yako (maisha yako
yanaweza yakawa mazuri au yakawa mabaya).
-
Unaweza
ukapokea baraka au laana unapotoa sadaka
Ø Wapo
waliotoa sadaka wakakataliwa na kupata laana:
Mfano 1: Mfalme
Sauli
1 Samweli
15 : 22 – 23
-
Sauli aliambiwa na Mungu akawaangamize Waamaleki wote
na mali zao lakini yeye alikwenda akaua watu na akabakisha mifugo iliyonona ili
aje aitoe sadaka kwa Mungu.
-
Mungu akaikataa sadaka yake kwa sababu hakuitii sauti
yake iliyomwagiza.
Mfano 2: Anania na
Safira
Matendo 5 :
1 – 11
-
Huyu mtu na mkewe walipatana wakauza kiwanja chao ili
waje walete fedha hiyo kama sadaka kwa Mungu, lakini walizuia kwa siri baadhi
ya kiasi cha fedha katika ile thamani waliyoiuza na wakadanganya kuwa wamekiuza
kwa fedha pungufu.
-
Mungu aliamua kuwaua mbele ya kapu la sadaka kwa
sababu walikuwa ni waongo; waliamua kuitii sauti ya Shetani iliyowashawishi
wazuie kwa siri kiasi fulani cha fedha badala ya kuitii sauti Mungu
iliyowaagiza wakauze kiwanja na kuileta thamani yote ya fedha mbele za Mungu
-
Kumbuka unaweza ukawa na imani lakini isiyo ya Kristo.
Imani ya Kristo huwa inakuja na Neno la Kristo ndani yake, na imani ya shetani
huwa inakuja na neno la shetani ndani yake. Ndio maana mtume Petro aliwaambia
ni kwa nini shetani amewajaza kumwambia uongo Roho Mtakatifu.
Ø Pia wapo
waliobarikiwa baada ya kutoa sadaka
Mfano 1: Ibrahimu
Mwanzo 22 :
1 – 12 – 14
-
Ibrahimu alipoambiwa amtoe mwanawe kuwa sadaka kwa
Mungu, wala hakumzuia bali alikubali kumtoa.
-
Ndipo Mungu alipoahidi kumbariki Ibrahimu na kumfanya
kuwa baraka kwa mataifa yote.
-
Ibrahimu aliamua kuitii sauti ya Mungu bila kujali
mazingira aliyokuwa nayo, kwa sababu Isaka ndiye mtoto wa pekee wa ahadi
aliyekuwa naye. Kwa kawaida ilikuwa ni vigumu lakini alitii.
Mfano 2: Mfalme
Sulemani
2 Nyakati 1
: 6 – 13 & 1 Wafalme 3 : 4 – 5
-
Mfalme Sulemani alipopakwa mafuta kuwa mfalme aliamua
kumtolea Mungu sadaka.
-
Hiyo sadaka ilimfanya Mungu ashuke azungumze naye
kwenye ndoto ili ampe haja ya moyo wake.
-
Hatukuambiwa kuwa alitoa sadaka ya shukrani au alitoa
sadaka ya namna gani lakini tunajua kuwa Mungu alijibu.
Hii inaonyesha yakuwa tunapotoa sadaka yoyote Mungu huwa
anaifuatilia. Hivyo kila sadaka unayoitoa huwa ina matokeo yake. – 1
Wakorintho 9 : 6
NB: Hii inatupa kuwa makini sana tunapotoa sadaka mbele za
Mungu tusije tukajitwalia laana badala ya baraka.
KAZI YA IMANI NDANI YAKO UNAPOTOA
SADAKA
Ni vizuri kwanza ukajua kuwa kuna aina mbalimbali za sadaka
ambazo mtu anaweza akazitoa mbele za Mungu
-
Unaweza ukatoa sadaka ya fedha, au mali, au hali, au
ukatoa nguvu zako, au ukatoa mwili wako kutumika na ikahesabika kuwa ni sadaka
mbele za Mungu, au pia unaweza ukatoa sadaka ya ukarimu n.k
Warumi 12 :
1
-
Sadaka yoyote ile ni lazima ibebe imani ndani yake
ndipo itakapompendeza Mungu
a.
Unapata
kuwa na amani juu ya kazi uliyopewa na Mungu uifanye hata kama mazingira
uliyopo hayakuruhusu ufanye hivyo
Kuna wakati Mungu anaweza akakusemesha utoe sadaka ambayo
kiuhalisia ni vigumu sana kuitoa kutokana na mazingira uliyopo, lakini imani
ndani yako inawahi kukamata moyo wako ili uwe na amani juu ya hicho
ulichoamriwa na Mungu ukifanye.
Waebrania
11 : 31
Yoshua 2 :
1 – 8 – 10
Biblia inasema kuwa Rahabu Yule kahaba aliwasaidia wale
wapelelezi wa Israeli kwa imani. Hii ni kwamba kuna namna ambayo Mungu
alizungumza na Rahabu juu ya kuwahifadhi wale wapelelezi hata kama kwa uhalisia
walikuwa ni maadui zao. Ile sauti ya Mungu ndani ya moyo wa Rahabu ikatengeneza
imani. Nayo imani ikaachilia amani ndani ya moyo wa Rahabu ili asiogope kuwakaribisha
wale wapelelezi.
-
Usidhani ilikuwa ni kitu chepesi kwa Rahabu
kuwakaribisha na kuwahifadhi wale wapelelezi, haikuwa kitu kirahisi. Ndio maana
ilibidi Mungu aachilie amani ndani yake ili kazi aliyopewa ifanyike.
-
Rahabu alikuwa anajua kabisa kuwa hawa watu wanakuja
kuangamiza mji wao wote lakini bado alipata amani ya kuwapokea na kuwahifadhi
wasiuawe na majeshi ya mji wa Yeriko.
-
Imani huwa inaachilia amani ndani ya mtu – Warumi 5 : 1
-
Hivyo hakuna amani pasipo kuwa na Imani.
-
Sadaka aliyoitoa Rahabu ilikuwa ni sadaka ya utu au
ufadhili.
Na kwa sababu hiyo, Rahabu kwa njia ya imani amepata heshima
kubwa kuliko hata wale wapelelezi
-
Biblia inatambua jina la Rahabu lakini majina ya wale
wapelelzi hatujajulishwa.
-
Pia Rahabu anatajwa kwenye ukoo wa Yesu kitu ambacho
si kila mtu alipata kuwa na heshima hiyo.
b.
Imani
inampa Mungu nafasi ya kushughulikia maisha yako ya baadae au msimu mpya kwenye
maisha yako.
Kuna watu ambao huwa wanasikia ndani yao msukumo wa kutoa
sadaka kila wanapokaribia kuingia katika msimu mpya kwenye maisha yao.
-
Sasa usidhani tu kuwa ni jambo la kawaida bali ni
sauti ya Mungu inazungumza ndani yako kwa sababu Mungu anataka ashughulikie
hali au mazingira unayoyaendea kwenye hatua nyingine ya maisha yako.
Mfano 1: Waebrania
11 : 7 & Mwanzo 8 : 15 – 21
Hizi ni habari za Nuhu wakati anatoka kwenye safina baada ya
maji kupungua juu ya nchi wakati wa Gharika.
-
Biblia haijatuonyesha kama kuna sehemu Mungu
alimwambia Nuhu amtolee sadaka bali Nuhu mwenyewe alijua umuhimu wa Mungu
kuhusika kwenye msimu mpya wa maisha yao kwa sababu dunia nzima walikuwa
wamebaki watu nane tu, pamoja na hao wanyama na ndege waliokuwa nao kwenye
safina.
-
Kumbuka kuwa baada ya gharika, kila kitu juu ya uso wa
dunia yote kiliharibika. Lakini sadaka aliyoitoa Nuhu ilifanya mambo yafuatayo:
i.
Ilimfanya Mungu aahidi kutoipiga tena dunia kwa maji,
ii.
Pia alirejesha majira na vipindi vya hali ya hewa
vilivyoharibiwa na maji.
Kwa hiyo kwa kupitia sadaka aliyoitoa Nuhu, Mungu
alishughulikia maisha ya wale watu nane baada ya kutoka kwenye safina.
Mfano 2: habari za
Mfalme Sulemani alitoa sadaka mbele za Mungu ili Mungu ashughulike na msimu
mpya kwenye maisha yake ya yeye kuwa mfalme wa Israel
1 Wafalme 3
: 4 – 5
c.
Imani
inaleta ushirika kati ya mtoa sadaka na Mungu anayetolewa hiyo sadaka
Unapotoa sadaka kwa Mungu wako ni ishara mojawapo ya kuwa
kuna ushirika kati yako na Mungu wako.
-
Kwa sababu sadaka inajulisha ni Mungu yupi
unayemtumikia
-
Kama unatambika basi utatoa sadaka kwa mizimu
unayoitambikia lakini kama unamtumikia Yehova Mungu wa kweli aliye hai basi
utatoa sadaka kwake.
-
Sasa kinachokuunganisha wewe na Mungu unayemtolea hiyo
sadaka sio sadaka bali ni imani. Kwa sababu ili utoe sadaka kwa Mungu aliye
hai, ni lazima kuwa ulisikia na kuitii sauti ya Kristo ndani yako ikajenga
imani ya Kristo moyoni mwako ndio maana ukaenda kumtolea Mungu sadaka; lakini
kama ulisikia sauti ya shetani ndani yako ikajenga imani ya kishetani moyoni
mwako basi utakwenda kutoa sadaka kwa miungu na mizimu.
-
Imani ndio inayokusukuma ni wapi pa kuipeleka sadaka
yako.
Na ni muhimu kukumbuka ya kuwa mahali ilipo hazina yako ndipo
na moyo wako utakapokuwepo. Mathayo 6 :
21
-
Imani huwa inakamata usikivu wa mtu ili kutii sauti ya
Mungu anayemtumikia.
-
Kama huwa unatoa sadaka kwa miungu basi hiyo miungu
inakamata moyo wako ili usisikie sauti nyingine bali sauti ya hiyo miungu tu.
No comments:
Post a Comment