Msisitizo: Ni kukusaidia kumtumikia Mungu kwa uaminifu huku ukitimiza unayopaswa kuyafanya.
UTANGULIZI:
Kuna tofauti kubwa sana kati ya kumtumikia
Mungu na kulitumia Jina la Yesu. Kuna watu wanalitumia jina la Yesu kuombea
watu, kutoa unabii, kuhubiri n.k lakini sio watumishi wa Mungu.
Somo hili linalenga kukusaidia kujua tofauti
iliyopo kati ya Yule mtu ambaye ni mtumishi wa Mungu na mwingine si mtumishi wa
Mungu lakini anatumia jina la Yesu akidhani ya kuwa anamtumikia Mungu.
Kumtumikia Mungu ni wito ambao mwanzilishi
wake ni Mungu.
-
Wito wako ndio unaokupa kujua sababu ya kuumbwa kwako.
-
Kumtumikia Mungu ni kufanya yale mapenzi ya Mungu. (maana yake kuyajua
na kuyafanya yale ambayo Mungu anataka uyafanye)
-
Kwa hiyo kama hufanyi yale anayokuagiza Bwana maana yake ni kwamba
humtumikii yeye, hata kama unatumia jina lake kwenye kazi yako au huduma
unayoifanya.
Luka 6 : 46 – Kwa nini
mnaniita Bwana Bwana lakini hamyatendi nisemayo?
-
Hii inaonyesha wazi kabisa kwamba ili uwe ni mtumishi wa Bwana
Yesu ni lazima uwe unafanya kile anachokuagiza kukifanya.
-
Kwa mfano; kuna watu
wanahuduma ya kuimba, kuhubiri au kuombea wenye shida mbali mbali kwa kutaja
jina la Yesu lakini hawafanyi yale ambayo Mungu anawaagiza kufanya.
Malaki 1 : 6 – “Mwana
humheshimu baba yake, na mtumwa humcha bwana wake, …basi kama mimi ni bwana
wenu kicho changu ki wapi”
-
Kama watumwa au watumishi hawamsikilizi bwana wao (bosi wao)
wanasemaje kuwa wanamtumikia?
-
Kwa maana kumtumikia mtu ni kufanya kile anachokuagiza ukifanye.
-
Mungu hataki ufanye kile unachokijua wewe au unachokiona kuwa ni
sahihi bali anataka ufanye kile anachokuagiza ukifanye. Hiyo ndio maana halisi
ya kuyafanya yale yampendezayo Mungu.
NB: Kumbuka kwamba unapomtumikia Mungu, yeye ndiye anayekuambia nini
cha kusema au cha kufanya unapotumika. Ni sawa na mtu anayekwenda kuhubiri
halafu hapati muda wa kumuuliza Mungu nini cha kuhubiri na badala yake
anakwenda kuhubiri kwa mazoea.
Biblia inasema hivi katika Mathayo 7 : 21 – 23
“si kila mtu aniambiaye Bwana Bwana
atakayeingia katika ufalme wa mbinguni bali ni Yule afanyaye mapenzi ya Baba
yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile Bwana hatukufanya unabii kwa
jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo? Ndipo nitawaambia dhahiri sikuwajua
ninyi kamwe”
-
Hapa Bbiblia inatuambia kuwa kuna watu wanaotumia jina la Yesu
katika kufanya huduma zao lakini Yesu mwenye jina hilo hawajui wao.
-
Wao wanadhani wanamtumikia Mungu lakini kumbe wanatumia tu jina la
Yesu katika kufanya huduma zao lakini kiukweli hawamtumikii Mungu.
NB: Kutumia jina
la Yesu bila kuwa na ushirika na Yesu huko sio kumtumikia Mungu.
-
Na kwa sababu hiyo watu wengi wanadhani ya kwamba kule kukemea mapepo kwa kutumia jina
la Yesu au kutoa unabii au kuhubiri kwa kutumia jina la Yesu ndio pekee
kumtumikia Mungu, sio kweli.
-
Mungu anachotaka hapa ni wewe kuwa na ushirika naye kwanza. Kwa
sababu kuwa na ushirika na Mungu ndio kutakusaidia wewe kumfahamu Mungu na
kuyajua mapenzi yake ili uyafanye.
-
Ushirika na Mungu unakujulisha mapenzi ya Mungu ni nini; nini
Mungu anataka wewe ufanye.
-
Kuwa na ushirika na Mungu ni jambo la muhimu sana kwa kila
mtumishi kujua kabla ya kuanza utumishi wowote ule.
-
Kwa sababu kazi ya kumtumikia Mungu si ya mtumishi wa Mungu bali
ni ya Mungu mwenyewe, yeye ndiye aliyekuagiza uifanye hiyo kazi, hivyo anajua nini
wewe unatakiwa kukifanya.
-
Wengine wandhani utumishi ni kazi yao ndio maana wanafanya vile
wanavyotaka wao na sio vile Mungu anavyotaka.
Pale Yesu aliposema “ndipo nitawaambia
dhahiri sikuwajua ninyi kamwe, ondokeni kwangu ninyi mtendao maovu”
-
Neno “sikuwajua” maana
yake sikuwa na uhusiano wowote na ninyi au sikuwa na ushirika wowote na ninyi.
-
Ni kweli mlitumia jina langu kuponya, na kutoa unabii na kufufua
wafu lakini mimi na ninyi hatujawahi kuwa wamoja, hatujawahi kufahamiana,
hatukuwa na ushirika wowote. Kwa hiyo kazi mliyoifanya nisawa na hakuna kitu.
Kwa mfano, Daktari ambaye anatibu watu katika
kituo cha afya lakini hajasajiliwa na serikali.
-
Kwa hiyo serikali haimtambui japokuwa anatibu watu
-
Hata kama atakuwa anatumia dawa za serikale kutibu watu ni kweli
watu watapona lakini yeye mwenyewe hatambuliki na serikali.
-
Pia ni hatari kwa afya za hao watu anaowatibu kwa sababu daktari
huyo anaweza asifuate miongozo ya afya katika kutibu wagonjwa inayotolewa na
serikali mara kwa mara.
Ukisoma kitabu cha Matendo 19 : 13 – 16
-
Hii ni habari ya wana saba wa mtu mmoja aliyekuwa anaitwa Skewa
ambaye alikuwa ni kuhani mkuu.
-
Vijana hao walijaribu kukemea pepo kwa kutumia Jina la Yesu lakini
pepo aliwaambia hivi Yesu tunamjua na Paulo naye tunamjua lakini ninyi ni akina
nani?
MAMBO KADHAA YANAYOTOKEA KATIKA
ULIMWENGU WA ROHO UNAPOKUWA NA USHIRIKA NA BWANA YESU
Mtumishi wa Mungu ni lazima uwe na ushirika
na Mungu unayemtumikia. Sasa yafuatayo ni mambo ambayo yanatokea pale ambapo
wewe mtumishi wa Mungu unapokuwa umetengeneza ushirika mzuri na Mungu wako.
1.
Ndani
mwako unabeba sura ya Mungu
2 Korintho 4
: 3 – 4
– Kristo ni sura ya Mungu.
Yohana 14 :
7 – 11
Yesu yu ndani ya Baba na Baba yu ndani ya Yesu, hivyo aliyemuona Yesu amemuana
Baba pia. Na aliyembeba Yesu amembeba Baba pia
Yohana 17 :
21 22
-
Unapompokea Bwana Yesu moyoni mwako, katika ulimwengu war oho
hauonekani wewe tena bali anaonekana Yesu aliye sura ya Mungu ndani yako.
-
Wewe ulishakufa, sio wewe unayeishi tena bali ni Krsto ndiye
anayeishi ndani mwako – Wagalatia 2 : 20
-
Mapepo yakikuangalia hayakuoni wewe bali yanaona sura ya Mungu
ndani yako.
-
Sura ya Mungu inaonekana ndani yako kwa sababu wewe unakuwa ndani
ya Yesu na Yesu anakuwa ndani yako.
-
Ndio maana utaelewa ni kwa nini Yule pepo aliwaambia wana wa Skewa
kwamba Yesu tunamjua na Paulo tunamjua lakini ninyi ni wakina nani?
-
Tafsiri yake ni kwamba Yule pepo alipoangalia ndani ya mioyo ya
wale wana wa Skewa hakuona sura ya Mungu ndani yao.
2.
Unabeba
heshima ile ile aliyonayo Yesu
Yohana 17 :
22 – Nami
utukufu ule ulionipa nimewapa wao …
-
Kwa lugha nyingine utukufu maana yake ni heshima au hadhi au
mamlaka.
Efeso 1: 20
– 23; 2 : 6 – Yesu ameketi juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu
na usultani, … akatufufua pamoja naye akatuketisha pamoja naye juu sana.
1 Yohana 3 :
1 – 2
– Ni pendo la namna gani alilotupa Baba kwamba tuitwe wana wa Mungu, … wala
haijadhihirika bado tutakavyo kuwa lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa,
tutafanana naye.
Katika ulimwengu wa roho, sisi tunapata kuwa
na heshima ile ile aliyonayo Yesu kwa sababu tumembeba Yesu mioyoni mwetu.
Zaburi 8 : 4
– 6
Zaburi 82 :
6 – Mimi
nimesema ndinyi miungu, na wana wa Aliye juu.
-
Biblia inaposema “tumeketishwa pamoja naye juu sana” maana yake
mahali alipoketi Yesu ndipo na sisi tumeketi hapo hapo, kwa hiyo heshima
aliyonayo Yesu ndio hiyo hiyo na sisi tuliyonayo.
NB: Kwa nini
tumepata heshima kama aliyonayo Yesu? Kwa sababu katika ulimwengu wa roho kuna
mamlaka tofauti tofauti za madaraka; kuna wafalme, wakuu wa anga, majeshi ya
pepo wabaya n.k hivyo ili uweze kupambana nayo ni lazima na wewe uwe kwenye
level au ngazi ya juu zaidi kuliko wao ndipo utaweza kuwashinda.
-
Ndio maana Biblia inasema tumeketishwa juu sana kuliko falme na
mamlaka na nguvu, ikiwa inamaana ya kuwa tuko juu ya kila aina ya upinzani wowote
katika ulimwengu wa roho.
-
Utumishi wowote ni vita, na ndio maana ni muhimu sana kwa mtumishi
yeyote wa Mungu ajifunze kutumia nafasi yake ya kimamlaka aliyonayo rohoni ili
kushinda vita katika ulimwengu wa roho.
-
Na kwa sababu hiyo unao uwezo ndani yako wa kutamka jambo nalo
likatokea.
Kwa hiyo hata kama watu hawatambui thamani
yako, jua ya kwamba wewe ni mtu mkuu sana na mwenye kuheshimiwa sana. Na hata
mbingu zinakujua
Na pia ni muhimu sana kwa watumishi wa Mungu
kujijua wao wana nafasi gani mbele za Mungu (sisi ni watoto wa Mungu aliye hai)
Nafasi tulizonazo katika ulimwengu wa roho ni
heshima tunayoipata baada ya Yesu Kristo kuingia mioyoni mwetu
NB: Nafasi
yoyote ile (kifalme na kikuhani) huwa ina mambo makubwa mawili
i.
Mamlaka
-
Mamlaka ni nguvu ya kiutawala juu ya mipaka ya eneo fulani
-
Eneo letu la kiutawala ni katika ulimwengu wa roho na wa mwili pia. Lakini eneo letu la vita ni
katika ulimwengu wa roho peke yake.
2 Korintho
10 : 3 – 5
Efeso 6 : 12
ii.
Majukumu /
wajibu
-
Majukumu ni kazi tunazotakiwa kuzifanya kutokana na nafasi
tulizonazo (nafasi ya kifalme na ya kikuhani)
-
Yeremia 1 :
4 – 10
– Yeremia anapewa kazi ya kufanya kutokana na nafasi ya kinabii aliyopewa.
-
Kila nafasi ina majukumu yake. Huwezi ukapewa nafsi isiyokuwa na
majukumu.
3.
Mungu
anakupa nafasi ya kufanya kazi pamoja naye
Yohana 15 :
14 – 15
– siwaiti tena watumwa kwa sababu mtumwa hajui atendalo bwana wake bali ninyi
mmekuwa rafiki zangu.
Warumi 8 :
28 – nasi
twajua ya kuwa Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia
mema.
Ni heshima kubwa sana kufanya kazi pamoja na
Mungu.
-
Si rahisi sana wakati mwingine kuelewa sentensi hiyo lakini hebu
fikiria kwamba kuna wakati Mungu hatofanya jambo lolote duniani bila
kukushirikisha kwanza. Hivi unajisikiaje unapopata nafasi hiyo? Amosi 3 : 7
-
Na Mungu anakushirikisha kwa sababu anajua akikuagiza uombe ni
kweli utaomba au uende ukafanye jambo fulani ni kweli unakwenda kufanya.
Mungu
anapokupa nafasi ya kufanya kazi pamoja naye, mambo haya yatatokea:
i.
Yeye anapata nafasi ya kukujulisha nini cha kufanya, mahali gani,
muda upi na kwa nani.
Yeremia 1 :
7 - 8
Zaburi 32 :
8
ii.
Wewe pia unapata nafasi ya kushauriana naye nini cha kufanya (unahojiana naye)
Isaya 43 :
26
Mathayo 16 :
19
Kama
kufunga au kufungua kunaanzia duniani kwanza basi maana yake ni kuwa Mungu
anakusikiliza wewe ni nini utakachoamua kukifanya naye ndipo afanye.
Mfano: Musa
alikataa kuwaongoza wana wa Israel bila kuwa na Uso wa Mungu pamoja naye.
Kutoka 33 :
15
-
Musa alikuwa anajua tofauti ya kuongozwa na malaika wa Mungu, na
Mungu mwenyewe.
-
Kuongozwa na Mungu sio sawa na kuongozwa na malaika. Hadhi au
heshima hazifanani.
-
Iweje aanze na Mungu kisha amalize na malaika?
4.
Unapata
kujulikana na kuaminika katika ufalme wa mbinguni.
Luka 10 : 17
– 20 – msifurahi
kwa sababu pepo wanawatii bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa
mbinguni.
Daniel 10 :
11 – Daniel
mtu upendwaye sana.
Huku kujulikana na ufalme wa mbinguni
kunatokana na uaminifu ulionao juu ya kuifanya kazi ya Mungu unayopewa. Kuna
watu wanapewa kazi na Mungu za kufanya lakini wanazifanya kwa ulegevu na sio
kwa uaminifu.
-
Mbingu zinarekodi kwamba mtu huyu ni mwaminifu au sio mwaminifu
-
Ni kitu kimoja wewe kumwamini Mungu lakini ni kitu kingine Mungu
kukuamini wewe.
-
Hebu fikiria Mungu anakuagiza muda fulani uende ukaombe lakini
wewe hauombi kwa muda ule aliokuagiza Bwana bali unakwenda kuomba kwa muda wako
uliojipangia. Mbele za Mungu unaonekana sio mwaminifu.
Mwanzo 18 :
17 – 19
– Je, nimfiche Ibrahimu jambo nitakalo kulifanya… kwa maana nimemjua ya kuwa
atawafundisha wazao wake juu ya njia ya Bwana.
Hesabu 12 :
1 – 7 – 8
– Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote.
Ayubu 1 : 1 – Mtu huyo
alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu na kuepukana na uovu.
Ni sawa na mfano wa mtu aliyeajiriwa
serikalini.
-
Ile kwamba ameajiriwa na serikali inamaanisha kuwa serikali inamuamini
ndio maana imempa ajira hiyo.
MSISITIZO AMBAO MUNGU ANAKUWA NAO
PALE ANAPOKUPA KAZI UIFANYE (ANAPOACHILIA WITO NDANI YAKO)
Msisitizo wa Mungu katika utumishi au huduma
anayokupa uifanye haupo katika umuhimu wa hiyo kazi aliyokupa bali upo katika
kusikiliza na kufuata maagizo na maelekezo anayokupa.
-
Kazi au utumishi wowote ulionao ni rahisi sana kwa mtu yeyote Yule
mwingine kuifanya lakini tofauti ni maelekezo.
-
Ni rahisi sana kwa watu wengi kusikiliza huduma zao zinasema nini
lakini hawataki kusikiliza Mungu anasema nao nini.
-
Mfano, swala sio kuwa na kipaji cha kuimba au kuhubiri bali ni
maelekezo na maagizo gani uliyopewa yanayohusu huduma yako ya kuimba au
kuhubiri.
Unaweza ukahubiri kitu ambacho Mungu
hajakutuma kwenda kuhubiri, Na huo ndio ugomvi mkubwa uliopo kati ya Mungu na
wahubiri wengi kwa sababu wengi wanahubiri vile ambavyo Mungu hajawatuma
kuhubiri. Wanahubiri wanayoyajua wao wenyewe na sio kile ambacho Mungu kawatuma
kuhubiri.
Yeremia 23:
16 – 18, 22, 25 – 28 – Lakini kama wangalisimama katika baraza yangu,
wangaliwasikizisha watu wangu maneno yangu.
-
Katika ulimwengu wa roho kuna eneo linaitwa baraza ya Mungu. Hapo
ni mahali ambapo Mungu anakutana na watumishi wake na kuwapa maneno yake kwa
ajili ya kuwapelekea watu.
-
Kwa mfano mhubiri yeyote ni lazima ujifunze kusimama barazani pa
Mungu ili upokee neno kutoka kwa Bwana kwa ajili ya watu unaokwenda
kuwahubiria.
NB: Usihubiri kwa sababu una kipawa cha kuhubiri bali hubiri kwa
sababu Mungu amekupa neno la kuhubiri.
-
Mungu anajua kuna uhusiano uliopo kati ya Neno linalohubiriwa na
hali za mioyo ya watu wanaosikia neno hilo.
-
Na ndio maana kuna watakaopokea neno hilo kama chakula cha
kushibisha nafsi zao, pia kuna watakopokea neno hilo kama uponyaji wa majeraha
katika miyo yao, na wapo pia watakopokea kama nguvu mpya ya kuimarisha roho
zao.
-
Kwa hiyo ni muhimu kusikia kutoka kwa Bwana kwa sababu Yeye ndiye
atakayekupa chakula sahihi kwa kuwa anajua watu wake wanahitaji nini na kwa
muda gani.
Kwa hiyo ni
vyema ukajua kuwa kuna watu wanaweza wakapona kwa neno unalokwenda kuwahubiria
au wanaweza wakapotea kwa neno hilo hilo unalokwenda kuwahubiria.
Yeremia 23 : 1 – 2, 16 – 17
-
Hebu angalia, hilo ni neno linalotoka madhabahuni lakini
linawaharibu watu badala ya kuwajenga na kuwasaidia.
-
Unaweza ukaenda mahali inawezekana ikawa ni kwenye mkutano fulani
au kanisa fulani na ukasikiliza mahubiri lakini baada ya yale mahubiri
kumalizika unaanza kujisikia huzuni au unahisi kukosa amani moyoni mwako. Roho
mtakatifu ndani mwako anapiga kelele kukuambia kuwa kuna chakula kimeingia
moyoni mwako lakini si kizuri kwa afya ya roho yako.
-
Ni sawa na gari inayotumia mafuta ya petrol halafu wewe ukaenda
kuweka mafuta ya diesel. Haitawaka bali itapata shida.
Hivyo ni hatari sana kuitii huduma uliyonayo
kuliko kumtii Mungu aliyekupa hiyo huduma.
-
Unapoweka huduma moyoni basi utaisikiliza zaidi huduma uliyonayo
badala ya kumsikiliza Mungu . ni rahisi sana kufuata akili zako badala ya
kufuata maelekezo unayopewa na Mungu.
-
Yesu ndiye anayekaa moyoni na sio huduma.
-
Ukimweka Yesu moyoni, utamsikiliza yeye zaidi. Lakini ukiweka
huduma moyoni basi utaisikiliza zaidi huduma
Ufunuo 3 : 20 – Yesu anakaa moyoni
Yohana 14 : 23 - Yesu na Baba watakuja kufanya makao ndani ya
mtu
Zaburi 119 : 11 – moyoni nimeliweka neno ambaye ni Yesu
Yohana 1 : 1 - Yesu ni Neno ambalo linatakiwa likae moyoni
Yesu
anapokuja kukaa ndani yako, haji peke yake bali anakuja pamoja na Baba kwa
sababu Yesu yu ndani ya Baba na Baba yu ndani ya Yesu.
Baadhi ya
mifano ya watu walioweka huduma na utumishiwao moyoni badala ya kumweka Mungu
moyoni mwao; na kwa sababu hiyo wakasikiliza sana huduma zao badala ya
kusikiliza maelekezo ya Mungu.
a. Utoaji wa sadaka wa Kaini
Kutoa sadaka ni utumishi. Unaweza ukaielekeza
sadaka yako madhabahuni au mahali pale ambapo Bwana atakutuma uipeleke
Mwanzo 4 : 3
– 5
Waebrania 11
: 4
-
Biblia inaeleza wazi kuwa hawa ndugu wawili walikuja kutoa sadaka
mbele za Bwana.
-
Huku kwenye kitabu cha Mwanzo hatuonyeshwi wazo la kutoa sadaka
lilitoka wapi lakini kitabu cha Waebrania kinatuambia “kwa imani” – maana yake wazo hilo lilitoka kwa Mungu kwa
kuwasemesha mioyoni mwao.
Kufuatana na Warumi 10 : 17 – Biblia inasema “basi imani chanzo chake ni
kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo”
-
Kwa hiyo lile neno “kwa
imani” maana yake ni kwamba Kaini na Habili wote walisikia neno la Bwana
juu ya agizo la kwenda kutoa sadaka.
NB: Agizo lilikuwa moja lakini maelekezo yalikuwa ni
tofauti.
-
Wote Kaini na Habili walifuata agizo la kutoa sadaka bali kilicho
watofautisha ni utekelezaji wa maelekezo binafsi waliyopewa.
-
Shida haipo kwenye agizo bali shida ipo kwenye kufuata maelekezo
-
Unaweza ukapatia kufuata agizo la kwenda kuhubiri lakini ukakosea
kwenye maelekezo ya nini cha kuhubiri na wapi pa kuhubiri na kwa nani unatakiwa
ukamhubirie.
-
Mfano: mtume Petro na Paulo hawa wote ni mitume na wameitwa kuwa
mitume wa Yesu Kristo bali tofauti yao ni kwamba Petro kapewa injili ya waliotahiriwa (kwa Wayahudi)
na Paulo amepewa injili ya wasiotahiriwa
(kwa wamataifa.)
-
Hapo ndipo pia utakapojua kuwa Kaini hakukataliwa kwa sababu ya
kutofuata agizo bali kwa kutofuata maelekezo.
b. Mfalme Sauli alipotoa sadaka ikakataliwa.
1 Samweli 15
: 1 – 3, 9, 10 – 11, 14 – 15 – 23
Habari hii inaeleza namna ambavyo mfalme
Sauli alipewa agizo na maelekezo ya kulipa kisasi cha Bwana juu ya Waamaleki.
-
Agizo lilikuwa ni kwenda kuwapiga Waamaleki, na maelekezo yalikuwa
ni kuwaangamiza kabisa bila kuacha hai chochote binadamu wala mnyama.
-
Lakini cha ajabu Sauli alichopatia ni kufanya agizo aliloambiwa
lakini akakosea kwenye maelekezo aliyopewa. Kwani aliacha hai baadhi ya mifugo
akinia kwamba aje kumtolea Mungu sadaka.
-
Mungu akamkasirikia kwa sababu ya kutofuata maelekezo aliyompa
japokuwa alitimiza agizo la kwenda kuwapiga Waamaleki.
NB: Kwenye kila
utumishi ambao Mungu amewapa watu wake kuna kuwa na agizo na maelekezo
-
Agizo linaweza likawa ni la pamoja lakini maelekzo yakawa ni
kibinafsi
-
Wote mnaweza mkawa ni wahubiri wa injili mmepewa agizo la kuhubiri
lakini maelekezo ya kuhubiri yakwa ni tofauti, kama vili ilivyokuwa kwa Mtume
Petro yeye alipewa injili ya waliotahiriwa na Paulo alipewa injili ya
wasiotahiriwa japo wote wawili walikuwa ni mitume.
-
Kwa hiyo usijaribu kuiga huduma ya mwenzako anatumiaje.
Hapo ndipo utakapoelewa vizuri nini maana
yake alipowaambia wale watu kuwa sikuwajua ninyi. (Mathatyo 7 : 21)
JINA LA YESU
Jina la Yesu ni jina la Mungu Baba mwenyewe
Tuanze kuangalia pale Yesu alipokuwa
anazaliwa.
Luka 1 : 31
– 33
“Tazama utachukua mimba na kuzaa motto mwanamume,
na jina lake utamwita Yesu”
Mathayo 1 :
20 – 21
“Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama
malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto akisema, Yusufu mwana wa Daudi, usihofu
kumchukua Mariam mkeo, maana mimba yake ni kwa uwezo wa Roho Mt, naye atazaa mwana
nawe utamwita jina lake Yesu”
Je, umeshawahi kujiuliza kwa nini Yusufu na
Mariam waliambiwa ya kuwa mtoto huyo atakayezaliwa jina lake wamwite Yesu? Je,
hili jina lilitokea wapi? Kungetokea nini kama mtoto huyo asingepewa jina Yesu?
Hebu tafakari juu ya haya maswali yatakusaidia kuchochea kiu ya kutaka kujua
siri iliyopo katika jina hili la ajabu
Sababu kubwa mbili za Yesu kupewa jina hili
ni hizi zifuatazo:
1. Ni mrithi
Waebrania 1
: 1 – 4
“Mungu, ambaye
alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia
nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa
mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu, Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa
utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake,
akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;
amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu
kuliko lao.”
-
Yesu ni mrithi wa vitu vyote kutoka kwa Baba. Mojawapo ya vitu
alivyovirithi ni jina la Baba yake ambalo ni Yesu.
-
Kumbuka kuwa huwezi ukarithi kitu ambacho ni cha kwako unarithi
kitu kisichokuwa cha kwako, na pia huwezi ukarithi jina lako bali unarithi jina
lisilo la kwako.
-
Kwa hiyo Biblia inaposema “kwa kadiri jina alilolirithi” maana
yake jina hilo halikuwa la kwake bali la Yule aliyemrithisha ambaye ni Mungu
Baba.
-
Na kwa sababu Mwana wa Mungu alikuwa ni mrithi wa yote basi
ilibidi pia arithi na jina pia.
-
Hivyo Biblia inapotuambia kuwa Baba alimpa Mwana jina lake maana
yake ni kwamba jina hili hapo awali lilikuwa ni jina la kwake Baba mpaka pale
alipoamua kumpa Mwana jina hilo kama sehemu ya urithi kwa kuwa Mwana alikuwa ni
mrithi wa yote.
Yohana 5 :
43 – “Mimi nimekuja
kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake
mwenyewe, mtampokea huyo.”
-
Yesu mwenyewe anasema kwa sababu amekuja kwa jina la Baba yake
ndio maana hatumpokei bali angekuja kwa jina lake mwenyewe tungempokea.
Hapo ndipo utakapolewa kwa nini anasema jina
hili ni bora kuliko majina yote mbinguni, duniani, na chini ya nchi- kuzimu (Ebrania 1 : 4 & Wafilipi 2 : 9 – 10)
Kwa hiyo Mungu Baba amempa Mwana jina hilo
ili ajulikane kwa hilo. Hapa utaelewa pale Yesu alipokua akituombea kwa Baba
yake katika kitabu cha Yohana 17 : 6,
11, 12, 26 - “….Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu…Wala
mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba
mtakatifu, Kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi
tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, Mimi naliwalinda Kwa jina lako ulilonipa,
nikawatunza….Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo….”
-
Kwa hiyo Mungu katika agano jipya anajifunua katika jina la Yesu.
2. Ni mtii
Wafilipi 2 :
9 – 10
“Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno,
akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti
lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila
ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba”.
Hii sentensi inayosema, “Kwa hiyo tena Mungu
alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina”; inatuonyesha ya kuwa ‘Kwa hiyo tena Mungu’ aliamua
kumpa mtoto wake jina lipitalo kila jina; jina la Yesu kwa kuwa mtoto wake
alifanya jambo Fulani lililompendeza.
-
Jambo hili ni
lipi? Ni UTII –
alikuwa mtii hata mauti; naam, mauti ya msalaba
Imeandikwa hivi katika Wafilipi 2:5-8
“Iweni na nia
iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye
mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa
ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna
ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama
mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba”
-
Yesu alikuwa ni mtii kwa kila alichokuwa anaagizwa kufanya na Baba
yake
-
Na ndio maana Yesu alikuwa anaujasiri wa kusema “mimi siyatafuti
mapenzi yangu mwenyewe bali mapenzi ya Yule aliyenipeleka” Yohana 5 : 30
Na kwa sababu pia alikuwa anayafanya yale
yampendezayo Baba yake, basin a Baba pia alikuwa pamoja na Mwana kila mahali
kwa sababu ya jina lake.
-
Yohana 8 : 28 – 29 “…na yakuwa sifanyi neno lolote kwa nafsi yangu,
ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo. Naye aiyenipeleka yu pamoja nami,
hakuniacha peke yangu kwa sababu nafanya siku zote yale yampendezayo”
-
Kwa hiyo Mungu Baba yupo pamoja na Bwana Yesu kwa sababu ya jina
lake.
NB: Jina la
Yesu limebeba uwepo wa Yesu. Hivyo jina la Yesu lina mamlaka kuliko majina yote
ya mbinguni, duniani na chini ya ardhi-kuzimu.
Na sisi pia
tumepewa jina la Yesu Kristo
Warumi 8 : 16
– 17 “Roho
mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na
kama tu watoto basi tu warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam
tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye”
-
Kufuatana na Yohana 1 : 12
– sisi tunafanyika kuwa wana wa Mungu pale tunapompokea Yesu Kristo maishani
mwetu. Na kwa sababu hiyo na sisi pia ni warithi sawa na Yesu Kristo tukirithi
yote kwa Baba yetu aliye mbinguni.
-
Na kitu kimoja wapo tunachorithi ni jina la Yesu ambalo ni jina la
Mungu Baba.
-
Kwa hiyo uwepo wa Mungu unakuwa ndani yetu kwa sababu ya jina la
Yesu.
MUNGU
ANAJULIKANA MAHALI KWA KUPITIA JINA LAKE
Mungu anaweza akajitambulisha kwa watu au
akajifunua kwa watu kutokana na Jina lake. Kuna watu ambao walimfahamu Mungu na
akajifunua kwao kwa namna ya tofauti na wengine walimvyomfahamu.
Mathayo 6 :
9 “Baba yetu
uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje”
-
Angalia yale maneno yanayosema “Jina lako litukuzwe” maana yake jina lako lijulikane au lifahamike
au litambulike.
-
Mungu akitaka ajulikane mahali huwa anajifunua katika jina lake
kwa sababu jina lake limebeba uwepo wake na pia jina lake limebeba kazi yake.
Yohana 17 :
6 “Jina lako
nimewadhihirishia” maana yake wamelijua jina lako, wamelifahamu
Mungu anapenda kutukuzwa.
-
Sasa
anatukuzwaje?
-
Kwa kupitia
jina lake.
Jina lake linapotukuzwa yeye ndiye anatukuzwa. Kwa sababu jina lake
linamaanisha uwepo wake.
Angalia kile kipindi ambacho Mungu alimtuma
Musa kuwatoa wana wa Israel katika nchi ya utumwa:
Kutoka 3 : 13 : 13 – 14 – Musa
aliuliza, je, nikienda niwaambie huyo Mungu aliyekutuma kwetu anaitwa nani?
Mungu akamjibu
-
Unaweza ukajiuliza kama mimi nilivyojiuliza, kwamba kwa nini
Waisrael walitaka kujua jina la Mungu aliyemtuma Musa wakati alishawaambia kuwa
Yeye ni Mungu wa baba zao Ibrahimu, Isaka na Yakobo?
-
Wana wa Israel walikuwa wanajua kwamba Mungu anaposhuka mahali na
akajidhihirisha kwao basi jina lake linatambulisha kazi yake, hivyo walijua
kweli ni Mungu wa baba zao na alijifunua kwao lakini baba zao hao hawakuwa
utumwani kama wao walivyokuwa utumwani kwa hiyo alivyojifunua kwa baba zao ni
tofauti atakavyojifunua kwao. Ndio maana walitaka kumjua jina lake kwa sababu
walikuwa wanajua jina lake litawajulisha Mungu anayewasaidia atajifunua kwao
kwa namna gani.
Pia ukisoma Kutoka 6 : 2 – 3 – Biblia inaeleza
kwamba Mungu hakujulikana kwa akina Ibrahimu, Isaka na Yakobo kwa Jina la
YEHOVA bali alijulikana kwa jina la Mungu Mwenyezi.
-
Hivyo hiyo inatuonyesha wazi kabisa kwamba Mungu alivyojifunua kwa
wana wa Israel ambao walikuwa utumwani ni tofauti na alivyojifunua kwa
Ibrahimu, Isaka na Yakobo, ndio maana akasema kwao sikujulikana kwa jina la
Yehova bali kwa jina la Mungu Mwenyezi.
Mwanzo 17 :
1 Ibrahimu anamfahamu Mungu Mwenyezi
Mwanzo 28 :
1 – 3 Isaka anamfahamu Mungu Mwenyezi
Mwanzo 35 :
11 Yakobo anamfahamu Mungu Mwenyezi
NB: Mungu
anataka ajulikane duniani ndio maana anataka jina lake lijulikane na litukuzwe
kwa sababu jina lake ndio jina kuu kuliko majina yote na ndio limebeba uwepo
wake.
Mahali ambapo kuna jina lake basi ndio penye
uwepo wake:
Kumb 12 : 10
– 11 – 14
Biblia inasema kuwa mahali atakapopachagua
Bwana ili aliketishe jina lake hapo ndipo mtakapomtolea Mungu sadaka zenu na
ndipo ambapo mtakapoabudu. Kwa hiyo ni wazi kabisa kwamba mahali penye jina la
Yesu basi pana uwepo wa Yesu.
Wakati mwingine tutapata neema ya kujifunza
zaidi kuhusu Jina la Yesu.
MAMLAKA NA
UWEZA WA JINA LA YESU
Kwa kupitia jina la Yesu;
ü Matendo 4 : 12 – tunaokolewa
ü Marko 16 : 17 – 18 – tunatoa pepo (mfano: Matendo 16 : 16- 18), tunasema kwa lugha mpya, tunaweka mikono yetu
juu ya wagonjwa nao watapata afya na hata tukinywa vitu vya kufisha
havitatudhuru.
Kwa hiyo ukitaka kulitumia jina la Yesu
Kristo kihalali na uweze kuona uwezo na mamlaka yake ni muhimu kwanza, uwe
mwana wa Mungu kwa kumpokea Kristo moyonimwakokama Bwana na mwokozi wako; pili,
uwe mtii ukifuata maagizo ya neno la Mungu katika Roho Mtakatifu.
Sasa unaweza
ukajiuliza swali hili;
Kama mtu anayemwamini Mungu ndiye anayeweza
kulitumia jina la Yesu kwa usahihi, kwa nini basi kuna watu watalitumia jina
hili la Yesu kutoa unabii, kutoa pepo n.k angali sio watumishi wa Mungu?
Jibu:
Jibu la swali hili lipo katika mfano huu:
Serikali ina utaratibu wa kusajili madaktari wanaotibu magonjwa ya binadamu
(medical doctors), sasa kuna watu ambao wako huku mitaani na inawezekana
wamefungua maduka ya dawa na wanatibu watu bila ya kuwa na leseni
zinazowaruhusu wao kutibu. Lakini kiukweli ukienda pale kupata msada wa
kitabibu utaupata hata kama hana leseni ya udaktari.
-
Sasa hapa elewa kwamba hata kama daktari hana leseni ya kutibu
lakini akakupatia dawa sahihi ya kuponya ugonjwa wako ni wazi kuwa utapona, kwa
sababu kinachokuponyesha ni dawa na sio leseni yake. Hivyo ndivyo na watu
wanaotumia jina la Yesu lakini wao wenyewe hawajulikani na huyo Yesu mwenyewe.
Ni maombi yangu kuwa Mungu akakujulishe
tumaini la wito wako katika Kristo Yesu kama ulivyo ili umtumikie kwa furaha
huku ukumtukuza Yesu moyoni mwako.
No comments:
Post a Comment