KUJIKINGA NA MASHAMBULIZI YA ROHO ZA UDANGANYIFU ZINAZOTENDA KAZI KATIKA NYAKATI HIZI ZA MWISHO

 Mkazo wa somo: ni kukusaidia kutunza na kuimarisha imani yako kwa Yesu Kristo bila kufuata udanganyifu wa adui. Ni muhimu ukajua kuilinda imani yako uliyonayo kwa Mungu.

Yako mashambulizi yanayoletwa na hizi roho zidanganyazo juu ya wateule wa Yesu Kristo ili wasiendelee kumwamini na kumtegemea Mungu wao.

1 Timotheo 4 : 1

Biblia inaeleza wazi ya kwamba nyakati za mwisho watu watajitenga na imani wakisikiliza roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani.

-          Lile neno “kujitenga na imani” maana yake wataicha imani ya kweli na wataelekea imani potofu.

-          Maana yake ni kwamba kuna roho chafu ambazo zinatoka kwa shetani zinazoachiliwa katika kipindi hiki cha siku za mwisho kwa ajili ya kuwapoteza watu na kuwaondolea imani yao kwa Yesu Kristo.

-          Kikubwa zaidi kinacholengwa hapo ni watu kupoteza mahusiano kati yao na Mungu wao.

-          Kwa sababu imani inaleta mahusiano binafsi kati ya mtu na Mungu wake. Huwezi ukaenda mbele za Mungu kama humwamini; ni lazima kwanza uamini kama yupo – ndivyo kitabu cha Waebrania 11 : 6 inavyotuambia.

-          Hizi roho za udanganyifu zinakuja kipindi hiki kabla ya Yesu kurudi mara ya pili ili watu watetereke kiroho wasiwe imara. Unajua uongo kazi yake ni kukufanya utoke kwenye ukweli.

Hata pale katika bustani ya Edeni, roho ya udanganyifu ilikuwepo, ilitangulia kuja kabla ya Mungu hajashuka na kuwatembelea Adamu na Hawa siku ile wakati wa jua kupunga.

Mwanzo 3 : 1 – 8

-          Mungu aliposhuka aliwakuta tayari wamekwisha danganywa na nyoka kwamba wakila matunda walioambiwa wasiyale hawatakufa, wakati Mungu aliwaambia kuwa wakila hayo matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya watakufa. Na huo ndio ulikuwa ni uongo wa adui ili kuharibu uhusiano uliokuwepo kati ya mtu na Mungu.

Uongo huwa unafanana na ukweli lakini sio ukweli. Uongo utabaki kuwa ni uongo na ukweli utabaki kuwa ni ukweli. Hakuna namna yoyote ambayo uongo utageuka na kuwa ukweli. Hakuna!

 

Na hivi ndivyo itakavyokuwa katika nyakati hizi za mwisho ya kwamba roho ya udanganyifu inaachiliwa kwa ajili ya kuwaondolea watu imani yao kwa Yesu Kristo.

Swala sio kutokuwa na imani bali wanakuwa na imani juu ya vitu vingine au watu wengine lakini sio kwa Yesu.

Mathatyo 24 : 3 – 4

-          Hapa wakati Bwana Yesu ameulizwa na wanafunzi wake juu ya dalili za kuja kwake mara ya pili na ya mwisho wa dunia; Yesu aliwajibu kwa kuwataadharisha juu ya ujio wa roho za uongo ambazo zinaweza kuonekana zinafanya kazi sawa sawa na ukweli lakini sio za kweli.

-          Bila kuongozwa na Roho Mt. ndani yako ni vigumu sana kutenganisha uongo katikati ya ukweli.

-          Shetani ili ampate mtu huwa anamletea kitu kinachofanana na cha kweli lakini sio cha kweli.

Kwa mfano: kama unatembea njiani, roho ya udanganyifu haikuzuii kutembea bali itakuletea njia nyingine isiyo sahihi.

-          Roho ya udanganyifu haiwezi kukuzuia usisikile mahubiri au mafundisho bali itakuletea mafundisho yasiyo sahihi.

-          Hata kama katika mahubiri au mafundisho hayo wanataja jina la Yesu haimaanishi kuwa hayo ni mahubiri sahihi. Biblia inasema wengi watakuja kwa jina langu wakisema mimi ndiye nao watadanganya wengi.

-          Na ndio maana tunahitajika kujaa Roho Mt. wakati wote kwa sababu yeye ndiye kiongozi wetu kutujulisha mambo yaliyojificha hata mambo ya siri yeye anayajua. Ni hatari sana kwa wakristo wa nyakati hizi kutokujaa Roho Mt. ndani yao.

Mathayo 24 : 5, 24 – 25 – Yesu anawaonya na kuwapa angalizo juu ya ujio wa roho za udanganyifu ambazo zitatumia jina la Yesu au mafundisho yanayodhaniwa kuwa ni sahihi na kumbe sio sahihi. Na wengine watatoa hadi ishara na maajabu makubwa na kuwadanganya watu kuwa ni Yesu amefanya hiyo miujiza na kumbe sio kweli.

-          Lengo kubwa hapo ni kuwaondolea watu imani yao waliyonayo kwa Yesu.

-          Na ndio maana watu wengi kwa sasa wanakwenda ibadani au kanisani lakini hawana imani na Yesu wanayemwabudu. Wako tayari kuamini vitu kama keki au maji au mafuta ya upako lakini hawamwamini Yesu anayeweza kuwasaidia bila hivyo vitu. Na wengine wanakwenda mbali zaidi kwa kuwaamini watu na kuwategemea lakini mioyoni mwao wamemwacha Bwana.

Sasa angalia, kinachofanya watu wasiwe na imani kwa Yesu Kristo ni mafundisho yasiyo sahihi. Kisikutishe sana kwamba watu wanajazana katika nyumba za ibada zenye miujiza, wengi hawamfuati Yesu mtenda miujiza bali wanafuata miujiza yake. Na imani yao hawajaiweka kwa Yesu bali wameiweka kwenye vitu wanavyodhani kuwa ndio vimewapa miujiza.

-          Ndio maana Yesu akatuambia tuwe makini tusije tukadanganywa.

 

MOJAWAPO YA MBINU ZINAZOTUMIWA NA ROHO ZA UDANGANYIFU KUFANYA KAZI

v  Zipo mbinu nyingi ambazo zinatumiwa na roho ya Udanganyifu katika kutenda kazi kwake. Mojawapo ya mbinu hizo ni kuwafanya wakristo wasijue na kuthamini kazi za silaha za kiroho za Mungu tulizopewa kuzitumia (kuzijua kazi za silaha moja moja dhidi ya shetani)

Waefeso 6 : 11 - 17

Unajua tumepewa silaha za kumpinga shetani na kazi zake. Ziko silaha za kujilinda na silaha za kushambulia.

-          Na mara nyingi tumekuwa tukizitumia silaha za kushambulia zaidi na tukaacha zilaha za kujilinda.

-          Tunasahau ya kuwa shetani naye anazo silaha zake za kutushambulia hivyo ni lazima na sisi tuvae silaha zote ili tuweze kuizima mishale yote inayotoka kwa adui.

-          Biblia inatuagiza tuvae silaha zote na sio baadhi – (ule mstari wa 11)

Kwa hiyo, Roho ya udanganyifu inakufanya usione umuhimu wa kila silaha za kumpinga shetani.

-          Na kwa sababu hiyo ni vyema ukatambua kuwa mojawapo ya hila za shetani ni hiyo roho ya udanganyifu.

-          Ili uzipinge hila zote za shetani basi ni lazima uvae silaha zote za Mungu. Hiyo ndio kanuni ya Kimungu ilivyo.

NB: Kila silaha ina kazi yake na ina umuhimu wake, hivyo kama hutoivaa na hutojua namna ya kuitumia basi ujue kuwa kuna mahali tu utakwama kwa sababu shetani atakushambulia, na wewe hutoweza kumpinga.

 

 

 

Silaha mojawapo ambayo watu wengi huwa hatujui na pia hatupendi kuitumia sana ni Chapeo ya wokovu.

Chapeo maana yake ni kofia ngumu au kofia ya chuma, na huwa inavaliwa kichwani kwa ajili ya kulinda kichwa.

Isaya 59 : 17 na 1 Thesalonike 5 : 8

-          Kichwa ni eneo mojawapo katika mwili wa mtu ambalo ni la muhimu sana kulilinda. Kwa mfano uko vitani; adui yako anaweza akakulenga kichwani na akawa amekumaliza kabisa kabisa (hata ikapelekea kufa) lakini kama atakulenga sehemu nyingine za mwili wako kama miguuni au mkononi bado kuna uwezekano wa kuwa mzima na ukaendelea na mapambano. Kwa hiyo kichwani ni sehemu nyeti sana.

NB: Si watu wengi sana tunaojua kwamba wokovu ni silaha mojawapo tuliyopewa na Mungu ambayo ni silaha ya kujilinda.

Tuiangalie silaha inayoitwa chapeo ya wokovu

Hapa nataka tuangalie jambo hili kwa mtazamo huu ufuatao:

Yesu ni kichwa cha kanisa. Hivyo Yesu ndiye anayevalishwa kofia hiyo kwa sababu yeye ndiye kichwa chetu, (ili uelewe vizuri zaidi jambo hili, ni vyema ukatazama kwa mtazamo huu wa mtu, yaani Yesu ndiye kichwa, na kanisa ndio mwili; kwa hiyo chapeo ya wokovu inavaliwa kichwani yaani anavalishwa Yesu)

-          Sasa angalia, kwa nini Yesu ambaye ndiye kichwa chetu tumvalishe kofia ambayo ni wokovu? Tunalinda nini?

Jibu la swali hilo ni kama ifuatavyo: Ni lazima kwanza ujue Yesu anajifunua kama nani kwako.

Ø  Yohana 14 : 6 – Yesu kwetu anajifunua kama njia, na kweli na uzima

Kwa hiyo unamlinda Yesu kama unalinda njia, unalinda kweli, na unalinda uzima. Ni muhimu sana ukatambua jambo hili kwa sababu litakusaidia kuepuka mashambulizi ya roho ya udanganyifu.

a.      Njia- maana yake ni uhakika wa uelekeo wako. Wapi unaelekea?

-          Shetani akitaka kukudanganya hakunyang’anyi njia unayoiendea bali anakuonyesha njia nyingine isiyo sahihi. Anachokifanya shetani ni kukupoteza uelekeo wako. Hiyo ndio maana ya kukudanganya.

-          Mtu anapodanganywa maana yake amefuata jambo lisilo sahihi akidhani yakuwa ni sahihi. Kama ni njia, anakuwa amkwenda kwenye njia isiyo sahihi akidhani kuwa ni njia sahihi. Kwa hiyo maisha ya huyo mtu au mahusiano ya mtu huyo na Mungu wake ni lazima yaharibike au yapate shida kwa sababu uelekeo wake sio sahihi.

-          Hivyo shetani anakuwa amekupoteza kwenye uelekeo wako.

ü  Hapa wokovu unalinda njia au uelekeo wako. Wokovu unakusaidia kutokugeukia njia nyingine mbali na Yesu.

b.      Kweli

-          Hapa shetani anachokifanya ni kukuletea maneno yatakayofanana sana na kweli lakini ni ya uongo. Anaweza akatumia mafundisho au mahubiri yaliyopotoka kwa lengo la kukufanya usifahamu kweli ya Kristo.

-          Shetani anaweza akapindisha maagizo uliyopewa na Mungu kuhusu jambo fulani ili kukupoteza kwenye lengo alilolikusudia Mungu alipotoa hayo maagizo. Ni sawa na kile kipindi katika bustani ya Edeni, nyoka alimwambia mwanamke kuwa mkila matunda yale hamtakufa wakati Mungu alisema kuwa wakila hakika watakufa.

-          Ndio maana Biblia inamuita shetani ni baba wa uongo (Yohana 8 : 44). Pia mahali pengine Biblia inasema kuwa shetani anajigeuza kwa mfano wa malaika wa nuru (2 Korintho 11 : 14 - 15)

-          Maneno ya shetani ni feki bali maneno ya Kristo ni ya kweli, nuru ya shetani ni feki na nuru ya Kristo ni kweli.

ü  Hapa wokovu unakulinda usije ukaamini kila neno linalokuja kwako au unaloletewa kwa sababu shetani anaweza akaachilia maneno yake ya uongo na yakavuruga uhusiano wako na Mungu.

Hivyo unatakiwa kuwa makini hata na mafundisho unayoyasikiliza. Sio kila mafundisho ni ya kusikiliza kwa sababu yanaweza yakakuharibu kiroho chako. Unapaswa kutulia mahali pamoja bila kutangatanga hovyo.

c.       Uzima – maana yake ni maisha aliyoyakusudia Mungu tuishi.

Waefeso 2 : 10 – kuna aina fulani ya mfumo wa maisha ambayo Mungu ameyakusudia watoto wake tuishi.

-          Sasa shetani anachofanya ni kukuletea aina nyingine ya mfumo wa maisha ambayo sio sahihi kwa mtoto wa Mungu kuishi lakini aina hiyo ya maisha inafanana sana na ile aina ya maisha ya Kimungu. Shetani anakuletea mfumo feki.

-          Unaanza kuona watu wa Mungu badala ya kuanza kukemea dhambi ndio wanaanza kuisifia na kuiishi. Ukiangalia lugha zao, matendo yao kuwaza kwao hakuna tofauti na mataifa wanavyoishi.

-          Unakuta vijana wengi wa kikristo wanaishi maisha ya kwenda na wakati hata kama wanamkosea Mungu, wao hawajali bali wanachojali ni kwenda na wakati.

-          Na hiyo inapelekea hata mitindo mingi ya kimaisha ya duniani unaanza kuiona kanisani kwa sababu ya kuiga.

ü  Kwa hiyo wokovu ndani yako utakusaidia kulinda huo mfumo wa maisha ili uishi kama apendavyo Mungu wako na sio uishi kama dunia inavyotaka uishi.

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...