Msisitizo: Ni kukusaidia wewe muombaji kujua namna ya kupanga kwanza vipaumbele vya Mungu kwenye ajenda zako za maombi kabla ya vipaumbele vyako.
Mara nyingi waombaji huwa tunapenda
kuombea sana mambo yanayotuhusu sisi wenyewe na kwa muda au kiasi kidogo sana
ndio tunakumbuka kuombea mambo ya nchi au mkoa au kanisa au familia n.k.
Muda mwingi muombaj anaoutumia
kuomba huwa anautumia kumueleza Mungu shida zake na haja zake lakini hatumii
muda mwingi kuombea makusudi na mipango ya ufalme wa Mungu mahali alipo.
Mstari unaotuongoza ni Ezekiel 22 : 29 – 31
“… nami nikatafuta mtu miongoni mwao atakayelitengeneza boma na kusimama
mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi nisije nikaiharibu, lakini
sikuona mtu. …”
Ukitazama kwa makini lile neno
“nami” sio mwanzo wa sentensi bali linaonyesha mwendelezo wa jambo lililokuwa linazungumziwa
hapo nyuma.
-
Kwenye huo mstari wa 29, Biblia inazungumzia habari za
dhuluma, uonevu na kutokutoa haki kwa maskini, hali ambazo zinatokea katika
nchi. Ndipo akasema “name nikatafuta mtu”.
Huu mstari hauwezi ukauelewa vizuri
kama hujaelewa kwanza nini maana ya ufalme wa Mungu na aina ya waombaji ambao
Mungu anawahitaji juu ya kuombea ajenda za ufalme wake.
MAMBO YA MUHIMU YA KUFAHAMU KUHUSU WAOMBAJI:
1.
Mungu ndiye
anayetufanya kuwa waombaji.
Ufunuo 5 : 9 – 10
-
Angalia lile neno “ukawafanya kuwa makuhani”
-
Kwa lugha nyepesi, kuhani ni muombaji.
-
Kuwa muombaji si jambo unalolitaka au unalolipata
mwanadamu kwa sababu umestahili hapana bali ni heshima au nafasi ambayo Mungu
anakupa kwa makusudi yake. Waebrania 5 :
1 – 4.
-
Tafsiri yake ni kwamba, unapopewa nafasi ya kuomba si
kwa sababu wamekosekana watu wa kuomba au kwa sababu wewe unasali kwenye kanisa
lenye ratiba nyingi za maombi, bali ni Mungu mwenyewe kakupa hiyo nafasi ili
uitumie kwa ajili ya makusudi yake. Na katika hayo makusudi yake ndipo
atakapokuteremshia ajenda zake za kuombea.
-
Ule mstari wa kwanza unasema “kuhani amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu”.
Maana yake ni kwamba ni lazima ndani yako Mungu ataachilia msukumo wa kuombea
mambo ambayo si mahitaji yako bali ni vipaumbele vya ufalme wake.
Biblia inasema, damu ya Yesu
ilimnunulia Mungu watu wa kila kabila, na lugha na jamaa na taifa, ikiwa
inamaanisha kwamba Mungu ameweka waombaji katika ngazi ya familia (jamaa), kwenye
kila lugha, kila kabila, na hata kila taifa.
-
Kote huko Mungu ameweka waombaji watakaoombea mambo ya
ufalme wa Mungu zaidi ya kuombea mahitaji yao binafsi.
-
Msukumo uliopo ndani ya waombaji wa aina hii ni
kuhakikisha wanaona ufalme wa Mungu unadhihirika mahali ambapo wamewekwa
kupaombea.
-
Kama mtu amewekwa kuombea familia yake, basi hatoomba
tu juu ya mafanikio yake binfsi bali ataomba juu ya familia yake imjue Mungu wa
kweli na iishi na kufanikiwa ndani ya huyo Mungu wanayemtumikia. Vivyo hivyo na
kwa waombaji wa kanisa au kabila au taifa, ajenda yao kubwa ni kwanza Mungu
ajulikane mahali walipo.
Kwa hiyo ni muhimu kujua kwamba
Mungu aliwatengeneza waombaji kwa makusudi yake. Na amewaweka mahali mahali ili
kuombea ufalme wa Mungu kujulikana mahali wanapopaombea, kama ni kanisani basi
ufalme wa Mungu udhihirike, au kama ni kwenye familia basi ufalme wa Mungu
udhihirike na kama ni kwenye taifa basi Mungu ajulikane kwenye hilo taifa.
2.
Misingi au
vipaumbele vya ufalme wa Mungu
Ufalme wa Mungu una misingi yake
ambayo ni muhimu kuifahamu.
Ukisoma kile kitabu cha Mathayo 6 : 33 Biblia inasema “Bali
utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake na hayo yote mtazidishiwa”
Mahali popote utakapo kuwepo ni
lazima utangulize ajenda ya ufalme wa Mungu kwanza kabla ya kutanguliza maslahi
yako binafsi.
-
Hebu fikiria pale unapokuwa unatafuta kazi (yoyote
ile), wazo la kwanza kukujia akilini mwako ni kiasi cha mshahara unachotaka
kulipwa. Lakini ukweli ni kwamba kabla ya kupata mshahara unatakiwa kutoa
huduma kwanza ndipo upewe mshahara wako.
-
Je ulishawahi kuifikiria hiyo huduma utakayokuwa
unaitoa ukishapata hiyo kazi kama inaendana na vipaumbele vya ufalme wa Mungu?
-
Hapo ndipo utakapojua kwamba si kila kazi
utakayotakiwa kuiomba au kuifanya hata kama watakulipa mshahara mzuri.
Mungu anachotaka kwanza si
kumueleza mahitaji yetu bali ni kuona tukiomba mapenzi yake yatimizwe kwanza.
Sisi tunayo mipango yetu juu ya maisha yetu lakini pia Mungu anayo mipango yake
juu ya hayo hayo maisha yetu. Kwa hiyo cha Mungu ndiyo kifanyike kwanza.
Na pia ukisoma Warumi 14 : 17 inasema:
“Maana ufalme wa Mungu si kula na
kunywa, bali ni haki, na amani, na furaha katika Roho
Mtakatifu”
Hii ndio
misingi ya ufalme wa Mungu (HAKI, AMANI, NA FURAHA)
v Haki
Ni kuyajua mapenzi ya Mungu kwako,
na mapenzi yako kwa Mungu.
Nini Mungu anataka atende kwako, na
nini unataka Mungu akutendee.
v Amani
Amani maana yake ni kutokuwa karibu
na hofu.
Yeremia 30 : 5 – Maana Bwana asema hivi, tumesikia sauti ya tetemeko
na ya hofu wala si ya amani.
Kinyume cha amani ni hofu. Amani
ikiondoka basi hofu inatawala.
Isaya 54 : 14 – Utathibitika katika haki, mbali na kuonewa, kwa
maana hutaogopa, na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia.
Kuwa na amani ni kuwa mbali na
maonezi.
Usipoijua haki yako, shetani bado
atakuonea tu na utabaki kuita ni mapito ya Bwana au ni majaribu ya kuniongezea
imani.
v Furaha
Jambo lolote ambalo halikuletei
furaha ndani ya moyo wako bali linakuletea huzuni ya kukudhoofisha au
kukukatisha tamaa basi msingi wa jambo hilo sio ufalme wa Mungu.
Kinyume cha furaha ni huzuni.
Wafilipi 4 : 4 – (7) Biblia inasema “Na amani ya Mungu ipitayo akili zote,
itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
-
Lile neno kuhifadhi maana yake ni kulinda. Kwa hiyo,
amani ya Mungu ina kazi moja wapo ya kuulinda moyo wako, isiingie huzuni
itakayoondoa tumaini uliloliweka juu ya Bwana katika mazingira unayopitia.
-
Hapo mwanzoni mwa hii mistari anaonyesha kuwa mtu
anaombea mambo yake na haja zake zinajulikana kwa Mungu, na inaonekana kabisa
mtu huyu pia anaombea ajenda za ufalme wa Mungu ndio maana Mungu anaituma amani
yake ili ihifadhi moyo wake na nia yake asije akakata tamaa kabla Mungu
hajamjibu maombi yake.
-
Ile amani inayotunza moyo wako ndiyo inayokupa kufurahi
katika Bwana siku zote kwa sababu unaendelea kumwamini na kumtegemea Mungu.
Kwa hiyo, hivyo ndiyo misingi au
viashiria vya ufalme wa Mungu mahali Fulani, na Mungu mwenyewe huwa
anavifuatilia.
Mpaka hapa sasa ndipo
utaelewa kwa urahisi kidogo ule mstari wa Ezekiel 22 : 29 – 31
-
Pale ambapo Mungu anatafuta mtu atakayeomba toba na
rehema juu ya mahali ambapo ufalme wake haupo.
-
Ule mstari
wa 29 unaelezea kuhusu mambo ya dhuluma na kutokutendeka kwa haki
juu ya nchi. Tafsiri yake ni kwamba misingi ya ufalme wa Mungu (haki, amani na
furaha) haipo katika hilo eneo ndio maana anatafuta mtu wa kuomba.
-
Muombaji wa namna hii huwa anaomba toba na rehema ili
Mungu arudishe ufalme wake ulioondoka kwa sababu ya dhambi.
-
Kumbuka: kinachoondoa ufalme wa Mungu mahali ni
dhambi. Kwa hiyo muombaji anaomba toba ili dhambi iondoke na isiwe na nguvu
tena bali ufalme wa Mungu ujengwe na uwe na nguvu mahali hapo.
Waombaji wa ajenda za ufalme wa
Mungu ndani yao watakuwa na msukumo wa kuombea juu ya haki kutendeka, kuwa na
amani na furaha.
-
Wewe ambaye umepewa mzigo wa kuombea taifa utashangaa
kila unapoona dhuluma kwenye nchi au maonezi yoyote yale utasikia msukumo wa
kuomba toba juu ya nchi na kuachilia tena ufalme wa Mungu kuja tena mahali
pale.
-
Na hata yule anayeombea familia au kanisa ni wazi
kwamba utakapoona haki hakuna, wala furaha na amani hakuna mahali ulipo, kuna
maonezi ya maskini na kunyimwa haki zao, basi utajua kuwa ni dhambi imeingia
ikaharibu mahali hapo na ndio maana ufalme wa Mungu umeondoka.
NB: Unachotakiwa kufanya ni kuomba toba na rehema juu ya mahali
hapo ili Mungu aachilie msamaha wake na asipaharibu.
Hivyo basi utakapoisoma tena hiyo Ezekieli 22 : 29 – 31 utaona mambo
yafuatayo:
i.
Mungu
anakumbuka rehema katikati ya ghadhabu
-
Anaposema “nami nikatafuta mtu …. Nisije nikaiharibu
nchi”. Hii inaonyesha wazi kuwa Mungu wetu kabla hajaadhibu mahali popote huwa
kwanza anakumbuka rehema juu ya watu wake hata kama wamekosa.
-
Mwanzo 18 :
23 – 26 – Kabla Mungu hajaangamiza miji ya Sodoma na Gomora
alitafuta mtu kwanza wa kuomba toba juu yao ili asiwaangamize. Japo muombaji
(Ibrahimu) hakufikia kiasi cha maombi kilichohitajika kuiponya ile miji.
ii.
Yapo mahusiano
katika ulimwengu wa kiroho kati ya Mungu na mahali Fulani (taifa, kabila,
familia, kanisa n.k)
-
Katika ulimwengu wa kiroho, familia yako, kabila lako,
taifa lako n.k ni baadhi ya maeneo ambayo Mungu anaweka uhusiano wake na hayo
maeneo kwa kuusimamisha ufalme wake mahali hapo.
-
Na kama ikitokea dhambi ikaingia mahali hapo basi
inaharibu mahusiano hayo ya Mungu na hilo eneo.
-
Kwa hiyo mahali hapo pakitawaliwa na dhambi basi
panaitwa “mahali palipobomoka”,
maana yake panahitaji matengenezo, laa sivyo, adhabu ya Mungu itashuka mahali
hapo.
-
Hivyo Mungu anaweza akaipiga familia au kabila, au
taifa kwa sababu mahusiano yameharibika na ufalme wake umeondoka kwa hiyo
hakuna tena watu wanaotenda haki, hofu na huzuni ndiyo vilivyotawala.
iii.
Mungu
anahitaji angalau mtu mmoja tu ili aiponye nchi
-
Nami nikatafuta mtu… hajasema kwamba akatafuta watu
bali akatafuta mtu.
-
Maana yake ni kwamba hata kama wote wametenda dhambi
kwenye familia au kwenye nchi na hasira ya Mungu ikawa juu ya eneo hilo basi
pakitokea tu mtu mmoja mwenye haki akasimama kwa ajili ya kuomba rehema kwa
Mungu ili Mungu asipaangamize mahali hapo, ujue kwamba Mungu hatopaangamiza
mahali hapo na ataparehemu kabisa kwa ajili ya huyo aliyeomba.
-
Yeremia 5 :
1 – muombaji mmoja mwenye haki anayo nafasi ya kuzuia ghadhabu ya Mungu
isiwake juu ya mahali au nchi au familia iliyomkosea Mungu.
-
Mithali 14
: 34 –“ haki huinua taifa bali dhambi ni aibu ya watu wowote”.
-
Mwenye haki mmoja anayo nafasi ya kuokoa taifa zima
kwa hiyo haki yake.
Hivyo mpendwa usijidharau ukajiona
huna thamani yoyote mbele za watu kwa kuwa mbele za Mungu wewe ni wa thamani
sana.
-
Mungu amekuweka kwenye hiyo familia kwa makusudi yake,
ndio maana inawezekana kwamba wewe ndio mtu pekee uliyeokoka kwenye ukoo mzima.
Wala kisikusumbue, kwa sababu kwa kupitia wewe Mungu anakwenda kuokoa ukoo
mzima au familia nzima.
-
Unapokuwa unaombea kwa mfano familia yako ni sawa na
kumwambia Mungu kwamba asiadhibu familia yako kutokana na dhambi zilizopo
kwenye hiyo familia, bali aiokoe kutoka kwenye maangamizi.
Mungu anatafuta angalau mtu mmoja
tu ili aiponye nchi, au kanisa, au familia n.k.
-
Wa kuiponya familia yako ni wewe muombaji.
-
Wa kuiponya nchi yako au kanisa lako ni wewe muombaji.
-
Madhara yoyote yanapotokea juu ya nchi au familia au
kabila au kanisa, wa kwanza kuulizwa ni wanamaombi waliowekwa kuyaombea hayo
maeneo.
Mungu haangalii wingi wa watu
wanoomba juu ya mahali fulani bali anaangalia watu wanoombea vipaombele vya
ufalme wake.
-
Kanisa linaweza likawa na waombaji wengi kwa idadi
lakini wakawa ni waombaji wasiokuwa na tija kwa taifa kwa sababu ya kutumia
muda wao mwingi katika kuombea shida zao binafsi badala ya kuombea ajenda za
ufalme wa Mungu.
-
Mungu amekuweka hapo ulipo kwa makusudi kabisa ili
kuujenga ufalme wake kwa kupitia maombi yako. Hivyo usijidharau hata kidogo.
No comments:
Post a Comment