TAMBUA NAFASI YA BABA KIBIBLIA

 

Siku ya wababa duniani & kanisani

Lengo la somo: kukusaidia kufahamu umuhimu wa nafasi ya mwanaume kama baba na inavyotambulika kibiblia katika kutimiza kusudi la Mungu.

Mwanaume katika Biblia ana nafasi nyingi sana. Anaweza akatambulika kama mume, Baba, kiongozi n.k

-          Na kila nafasi ina wajibu wake na umuhimu wake kutokana na ilivyoumbwa.

-          Aliyeziumba hizi nafasi ni Mungu mwenyewe na ameziweka kwa makusudi yake mwenyewe.

-          Kwa hiyo, kabla ya kuitazama nafasi yoyote kimwili kwanza ni muhimu uitazame kiroho kwanza ili upate kujua kile kilichomsukuma Mungu kuiumba hiyo nafasi.

-          Usipojua kusudi la hiyo nafasi basi pia hutoona thamani ya hiyo nafasi.

-          Thamani ya kitu chochote inatokana na umuhimu wake; kama umuhimu haupo basi hata na thamani yake haitakuwepo.

Leo nataka tuone kwa undani kidogo juu ya nafasi ya mwanaume kama baba.

Biblia inapotujulisha nafasi ya baba kwa mwanaume inataka kwanza tujue nafasi ya Mungu kama Baba ikoje kwa sababu yeye ndiye Baba wa mababa, maana yake yeye ndiye asili na chanzo cha hiyo nafasi.

Unaweza ukajiuliza ni kivipi Biblia inaonyesha Mungu anavyojifunua kama Baba!

Waefeso 3 : 14 – 15 – “kwa hiyo, nampigia Baba magoti ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na duniani unaitwa…”

-          Lile neno ubaba wote maana yake familia yote

-          Ubaba wa Mungu ambao Biblia inaelezea hapa maana yake ni asili ya vitu vyote.

-          Biblia inaonyesha kuwa Mungu Baba ndiye asili ya mambo yote mbinguni na duniani.

Kwa hiyo, nafasi ya hii ya baba ambayo mwanaume anapewa asili yake ni kwa Mungu Baba

Yeye ndiye “role model” wetu wanaume, ya kwamba tukitaka kusimama vizuri inavyotupasa katika nafasi hii ya baba ni lazima tumfuate yeye (Mungu Baba).

Na nafasi hii inaoonyesha uhusiano wa ndani zaidi kama mahusiano ya kifamilia (baba na watoto).

-          Kuna namna hii nafasi inakuletea picha fulani ya ukaribu na wale ambao wewe umepewa kuwa baba kwao.

-          Ndani yako ukipewa hii nafasi utaona kama unahusika kwa karibu zaidi juu ya maisha ya wale uliopewa kuwahudumia kama watoto wako, kwa sababu wewe ndiye baba yao.

NB: Nafasi hii ni zaidi ya kuwa baba wa watoto kwa maana ya kwamba umewazaa wewe bali wanakuwa ni watoto wako kwa sababu Mungu ameweka ndani yako kitu cha kuwasaidia hao watu ili uwahudumie kwa ukaribu ule ule kama ambavyo ungewahudumia watoto wako. 

 

BAADHI YA TAFSIRI ZA KIBIBLIA ZINAZOONYESHA UMUHIMU NA MAANA YA NAFASI YA BABA

Sasa fahamu ya kwamba hii nafasi ya baba ndani yake imebeba tafsiri tofauti tofauti kulingana na Biblia inavyoeleza. Baadhi ya tafsiri hizo ni kama ifuatavyo:

1.     Nafasi ya baba kama mzazi wa kiume

Kwa lugha nyingine ni kwamba Yule mzazi wa kiume anaitwa baba.

-          Kwa hiyo, kila mwanaume mwenye uzao, kwa lugha nyepesi anapata kuwa na hii nafasi ya kuitwa baba.

-          Hii nafasi ni ya mwanaume pekee na sio ya mwanamke na baba ndiye aliyebeba nasaba za uzao wake.

Nasaba ni uhusiano wa kizazi baina ya watu kutoka katika ukoo mmoja au familia moja. Hiyo ndiyo inayoonyesha undugu, familia, ukoo, jamaa moja n.k

-          Na uhusiano huo ni lazima uwe uhusiano wa kizazi

-          Kumbuka kuwa, mtoto amebeba damu ya baba yake na sio damu ya mama yake.

Nehemia 7 : 5

Ezra 2 : 59

Mbari za baba zao maana yake ni nasaba (DNA – Deoxyribonucleic Acid)

Ndio maana hata kwenye historia ya ukoo wa Yesu inaonyesha jinsi ambavyo uhusiano wa vizazi ulivyokuwa tangu Ibrahimu hadi Yusufu baba mlezi wa kimwili wa Yesu.

-          Japokuwa Yesu hakuzaliwa kutokana na baba na mama bali kwa uweza wa Roho Mtakatifu, maana yake ni kwamba damu ya Yesu ilikuwa si damu ya kibinadamu iliyotoka kwa baba yake bali ilikuwa ni damu halisi ya Mungu Baba mwenyewe ndiyo maana ni damu bora zaidi kupita damu zote na ndiyo iliyoweza kutuosha dhambi zetu.

Baba ndiye mzalishaji, hivyo damu yake na ya mtoto ni sawa.

-          Mtoto hachukui damu ya mama bali damu ya baba yake.

-          Kitaalamu ni wazi kabisa kwamba kwenye tumbo la uzazi la mwanamke, mtoto anachopata kutoka kwa mama ni mfumo wa chakula bali mfumo wa damu anakuja nao kutoka kwenye mbegu za uzazi kutoka kwa baba.

NB: Katika ulimwengu wa roho kuna eneo la uzazi la mwanaume na eneo la uzazi la mwanamke

-          Eneo la uzazi la mwanaume linaitwa “viunoni”

Mwanzo 35 : 11

2 Samweli 7 : 12

Mwanzo 46 : 26

Kutoka 1 : 5

-          Na eneo la uzazi la mwanamke linaitwa “tumboni”

Mwanzo 25 : 22, 23, 24

Watoto wakashindana tumboni mwake…, Bwana akamwambia mataifa mawili yako tumboni mwako.

Rebeka aliona watoto wawili wako tumboni mwake bali Mungu aliona mataifa mawili yako tumboni mwake

Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba Rebeka aliliona tumbo lake la kawaida kimwili kwamba limebeba mapacha bali Mungu aliliona tumbo la Rebeka la kiroho kwamba limebeba mataifa mawili.

Yeremia 1 : 5

Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua- maana yake tumbo la kimwili la mama yake

Na kabla hujatoka tumboni nalikutakasa- maana yake kabla hajatoka katika tumbo la uzazi la kiroho la mama yake alitakaswa

Tumbo – ni kimwili, tumboni ni kiroho (jifunze kujua hilo)

Zaburi 58 : 3 – wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao, tangu tumboni wamepotea wakisema uongo

Wanaongeaje wakiwa kwenye tumbo? Hii inaonyesha ni kwenye tumbo la kiroho (panapoitwa tumboni)

Nimejaribu kukuonyesha kwa kiasi tu kuwa haya mambo ya uzazi yameanzia rohoni kwanza kabla hayajaja mwilini, hivyo ni muhimu kuyajua ili unapoombea uzao wako ujue namna ya kuomba.

 

2.     Nafasi ya baba kama tegemeo la msaada kwa ajili ya kutunza au kuhifadhi maisha ya watu.

Hii ni nafasi tofauti na ile ya baba kama mzazi wa kiume

Biblia pia imeonyesha nafasi ya baba ambayo mtu hupewa na Mungu kwa ajili ya watu ili kuhifadhi na kutunza maisha yao kwa sababu ya kile kitu kilichopo ndani ya huyo mtu.

Kumbuka kwamba Mungu alipokuumba aliweka kipawa au karam fulani ndani yako ambayo hutoitumia tu kwa ajili ya maslahi yako peke yako bali pia kwa ajili ya wale watu ambao Mungu atakuletea uwahudumie.

Kuna watu ambao kuishi kwao, kuendelea kwao, au kufanikiwa kwao kunategemea uwepo wa mtu fulani, kwa sababu huyo mtu ana kitu fulani ndani yake ambacho ni msaada kwa ajili yao.

-          Watu wa aina hii wapo kwenye jamii zinazotuzunguka.

-          Kuna wengine ni matajiri na wanawasaidia watu wenye uhitaji na wengine ni watu wa kawaida lakini wanaweza kuwasaidia watu kwa njia nyingine.

Mfano 1: Yusufu alikuwa kama baba kwa Farao

Mwanzo 45 : 7 – 8

Mungu alinipeleka mbele yenu kwa ajili ya kuwaokoa maisha yenu na ndio maana amenifanya kuwa kama baba kwa Farao

-          Biblia inatuonyesha jambo la ajabu sana hapa. Inaonyesha kwamba maisha ya Farao kama mfalme wa Misri yalitegemea sana uwepo wa Yusufu katika taifa lake, katika namna ambayo alimuona kama baba yake.

-          Na kitu hicho Yusufu alikijua. Yusufu alijua umuhimu aliokuwa nao mbele ya Farao, ndio maana akawaambia ndugu zake kwamba yeye amekuwa kama baba kwa Farao.

-          Na sio tu Farao aliyemuona Yusufu kama baba bali taifa zima la Misri na mataifa jirani pia, kwa sababu kitu alichobeba Yusufu ndani yake kiliwasaidia mataifa yote ya kipindi kile.

-          Hivyo tunaelewa kuwa ndoto alizoziota Yusufu akiwa mtoto hazikuwa ndoto kwa ajili yak wake binafsi  bali zilikuwa ni kwa ajili ya kuhifadhi maisha ya watu. Mungu akamfanya Yusufu kuwa kama baba kwako.

Mfano 2: Ayubu kama baba kwa maskini na wahitaji

Ayubu 29 : 12 – 16 – 17

Nalikuwa baba kwa mhitaji na daawa ya mtu nisiyemjua naliichunguza.

-          Maandiko yanaonyesha kwamba Ayubu pamoja na utajiri wake na kumcha Mungu kwake bado pia alikuwa ni msaada na tegemeo kwa watu maskini na wenye uhitaji.

-          Hao watu hawakuwa ndugu zake wala hakuwa anawafahamu lakini alihusika katika kuwasaidia mambo mbalimbali kwenye maisha yao.

-          Kulikuwa na watu kipindi cha Ayubu ambao walimtegemea Ayubu kwa kula, kuvaa, kuishi, na hata kupata mahitaji mbalimbali

-          Ayubu alipoanza kupita kwenye majaribu pia wale watu nao walipita kwenye hali ngumu kwa sababu msaada wao (yaani Ayubu) hakuweza kuendelea kuwasaidia tena.

Na mara nyingi huwa hatujui namna ya kuwaombea watu wa namna hii tulionao kwenye jamii zetu. Hivyo unakuta kama wakipata shida yeyote, sio tu kwamba wao wenyewe ndio watateseka bali na jamii kubwa ya watu wanaowategemea pia watapata shida.

 

3.     Nafasi ya baba kama mwanzilishi na kiongozi wa kabila au ukoo au familia

Mwanzo 25 : 22 – 23 – Bwana akamwambia mataifa mawili yako tumboni mwako, na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako.

-          Hawa watoto wawili ambao ni mapacha walikuwa ni waanzilishi wa mataifa mawili tofauti. Mmoja alikuja kuwa mwanzilishi wa taifa la Israel na mwingine taifa la Waedomu

Mwanzo 10 : 21- Shemu ambaye ni baba wa wana wote wa Eberi

Mwanzo 36 : 8 – 9 – Esau ndiye baba wa Edomu wote.

 

Biblia inaonyesha kuwa mataifa na makabila na jamaa na familia zimetoka kwa watu.

-          Kuna watu ambao Mungu aliwaweka kuwa waanzilishi na waasisi wa mataifa mbalimbali au makabila au ukoo.

-          Sasa hao waanzilishi wanaitwa baba. Unaweza kukuta wameelezea kwa mfano baba wa Edomu wote, au baba wa kabila la Yuda, au baba wa kabila la Manase

Hesabu 1 : 4

Mfano 1: Hesabu 17 : 1 – 3, 6

-          Hapa tunaona mfano huu kwamba kila fimbo moja ilikuwa inawakilisha nyumba ya kila baba ambaye ni katika wakuu wa makabila yao.

-          Sasa angalia, kama zingekuwa ni nyumba kwa maana ya familia basi zisingekuwa fimbo 12, zingekuwa fimbo nyingi sana. Bali wale wababa wa kila nyumba walikuwa ni viongozi wa makabila ya wana wa Israel (makabila kumi na mbili)

Makabila katika taifa la Israel yametokana na watoto wa Yakobo, hivyo kila mtoto mmoja alikuwa ni baba wa kabila lake

-          Yeye ndiye aliyelizaa hilo kabila

-          Yeye ndiye mwanzilishi wa hilo kabila

-          Na yeye ndiye aliyebeba baraka au laana za kabila zima

-          Kila aliyezaliwa katika kabila husika alikutana na mbaraka au laana hiyo iliyotokana na mwanzilishi wa kabila hilo – Mwanzo 49 : 1 – 28 & Hesabu 18 : 1 - 2

 

 

 

 

 

 

4.     Nafasi ya baba kama kichwa cha familia au mke

1 Wakorintho 11 : 3

Waefeso 5 : 23

-          Biblia inaonyesha namna ambavyo Mungu amemweka mwananume kuwa kichwa cha familia yaani kiongozi wa familia.

-          Na siku zote, kiongozi wa familia anawajibika katika hiyo familia

Hebu tuangalia kidogo baadhi ya wajiu na majukumu ya mwanaume mwenye nafasi hii ya baba kama kichwa cha familia.

a.      Kuitunza na kuilea familia yake

Waefeso 5 : 28 – 29 – ni wajibu wa kila baba kuilisha na kuitunza familia yake.

Maana yake ni kwamba baba anahusika na maendeleo ya kila mtu aliyeko katika familia anayoitunza.

-          Usiwe mmoja wapo wa wale wanaume wanaozikimbia familia zao kutokana na hali ngumu za kimaisha, bali unatakiwa uwe kielelezo na mfano kwa watu wa familia yako. Ndio maana ukaitwa kichwa cha familia.

-          Kuna familia ambazo mke anaweza akamuona mumewe ni kama baba yake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mume amesimama vizuri katika nafasi yake ya kuilea na kuijali familia yake pamoja na mke wake.

 

b.      Baba ni mwalimu katika familia

Kumb 6 : 6 – 7

Mithali 22 : 6

Ni wajibu wa kila mzazi na hasa baba wa familia kuwafundisha watoto wako njia iwapasayo kuiendea.

-          Baba huwezi ukafundisha watu waifuate njia iliyo sahihi wakati wewe mwenyewe hauendi katika njia sahihi. Hivyo ni lazima uchague kwanza njia sahihi ndipo utakapojua namna ya kuwafundisha watoto na familia yako yawapasayo kufanya. Yoshua 24 : 15

Pia baba anatakiwa ajue namna ya kuwaonya watoto wake anaowapenda

            Waebrania 12 : 6

            Mithali 3 : 11 – 12

 

 

 

 

c.       Baba hutakiwi kuwakatia tamaa watoto bali unatakiwa kuwavumilia na kuwapenda

Luka 15 : 11 – 32

Huo mfano unaonyesha namna Yule baba wa mwana mpotevu alivyokuwa na uvumilivu na upendo mkubwa kwa mwanaye aliyedai urithi wake mapema na kuondoka. Aliporudi alimuomba msamaha baba yake na akasamehewa.

Haijalishi mtoto wako amekukosea kiasi gani, hutakiwi kumkatia tamaa bali unatakiwa kumuonya na kuendelea kumpenda.

Moja ya sifa ya kuwa baba bora ni kujua namna ya kuwasamehe watoto wako waliokukusea pale wanaporudi kwako kukuomba msamaha.

 

d.      Baba una wajibu wa kuweka urithi kwa ajili ya uzao wako

Mithali 13 : 22- mtu mwema huwaachia wana wa wanaye urithi.

Mithali 19 : 14 – nyumba na mali ni urithi mtu apatao kwa babaye

Hivyo ni wajibu wa kila baba ambaye ni kichwa cha familia kutengeneza “future” ya watoto wake (yaani kutengeneza maisha ya baadae ya watoto wako).

-          Ni lazima ujifunze kuona mbele zaidi kule ambako familia yako inaelekea.

Baba hutakiwi kujifikiria wewe tu peke yako bali unatakiwa kufikiri juu ya familia yako inaishije na inauelekeo upi.

Kumbuka kuwa wako watoto wanaokutegemea wewe na pia wako wajukuu wanategemea waishi vizuri kutokana na urithi utakao waachia (ni haki yao kibiblia kupata urithi kutoka kwako).

Mjukuu kudai urithi kutoka kwa babu yake ni haki yake kibiblia.

Hivyo ufahamu na akili yako ewe baba vinatakiwa vifunguke ili uone jamii kubwa ya watu wanao kutegemea na kukufuata nyuma yako.

Ni lazima ujifunze kuishi kwa malengo ili uishi maisha yenye maana. Mitahli 29 : 18

Ni maombi yangu kuwa somo hili litafungua kwa sehemu ufahamu wako na kukusaidia kuanza kuishi kama vile apendavyo Mungu wako aliyekuokoa.

-          Kumbuka kuwaombea na wababa wengine ili watumie nafasi zao vizuri

-          Wanaume wengi hawajua majukumu yao kwa sababu hawajafundishwa na imepelekea kupata kizazi ambacho kinabaki kujiita tu mimi ni kichwa cha familia lakini hajui maana yake na wajibu wake ni nini kuwa kichwa cha familia.

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...