KUMSHUKURU MUNGU KUNAACHILIA NGUVU ZA MUNGU NDANI YAKO ZA KUKUSAIDIA KUANZA MSIMU MPYA

SEMINA YA MKESHA WA MWAKA MPYA 2023

Msisitizo wa somo: Ni kukujengea tabia ya kupenda kumshukuru Mungu kila wakati kwenye maisha yako.

1 Thesalonike 5 : 18

“shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo”

-          Huu mstari uzito wake upo kwenye hii sehemu ya pili inayosema “… maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu”

-          Watu wengi huwa hatuna habari na huo mstari tukidhani yakuwa hautuhusu lakini ukweli ni kwamba ndio uliobeba maana/uzito wa mstari mzima.

-          Tafsiri yake ni kwamba anachokitaka Mungu kwetu sisi ni tuwe na shukrani mbele zake katika mazingira yote hata kama ni magumu. Mungu huwa anapenda kushukuriwa. Anapenda kuona watoto wake wakiwa wanamshukuru Yeye katika hali zote wanazopitia.

Ukisoma kwenye Biblia ya Kiswahili unaweza usione huo uzito lakini baadhi ya tasfiri za Biblia za kiingereza zinaonyesha wazi jambo hilo.

Kwa mfano:

American Standard Version-ASV

“In everything give thanks: for this is the will of God in Christ Jesus to you-ward.”

Amplified Bible-AMP

“In every situation [no matter what the circumstances] be thankful and continually give thanks to God; for this is the will of God for you in Christ Jesus.”

Complete Jewish Bible-CJB

“In everything give thanks, for this is what God wants from you who are united with the Messiah Yeshua.”

Contemporary English Version-CEV

“Whatever happens, keep thanking God because of Jesus Christ. This is what God wants you to do.”

-          Hapo tunaona kwamba kutokana na hizo tafsiri mbalimbali za Biblia, Kumshukuru Mungu ni jambo ambalo Mungu anategemea watoto wake watakuwa wanalifanya mara kwa mara kwake.

-          Ndani mwako itaanza kutengenezeka tabia ya kumshukuru Mungu sit u kwenye matukio maalum bali hata kwenye mambo ambayo unadhani ni ya kawaida kwako lakini Mungu anahitaji shukrani zako.

-          Wengine wanamshukuru Mungu baada ya kuwavusha kwenye magumu na wengine wanamshukuru Mungu baada ya kuwapatia mahitaji yao. Hayo yote ni mema, lakini tambua kwamba kumshukuru Mungu ni kwenye mambo yote.

Jambo la muhimu la kufahamu ni kwamba huwezi ukamshukuru Mungu wakati unapita kwenye hali ngu kama humuoni Kristo kwenye hiyo hali.

-          Wengi tunaona kushindwa, kukata tamaa, kuvunjwa moyo, kudharauliwa, n.k

-          Lakini ukijifunza kumuona Kristo kwenye hiyo taabu unayopitia, basi kitakachoinuka ndani ya moyo wako ni kumshukuru Mungu.

-          Kumshukuru Mungu hakuji hivi hivi; ni lazima ujifunze kwanza kumuona Yesu Kristo kwenye hiyo hali unayopitia ndipo utamshukuru Mungu.

-          Unajua kuna wakati mwingine unaweza ukapitia hali ambayo ni vigumu sana kusema kwamba utamshukuru Mungu, kwa sababu moyo unakataa kabisa kutokana na ugumu wa mazingira unayopitia. Si kwamba hujui kuwa unatakiwa kumshukuru Mungu bali moyo unakataa kabisa. Hapo unatakiwa umuombe Mungu akusaidie.

 

MAANA YA KUMSHUKURU MUNGU

Kumshukuru Mungu ni ile hali ya kuonyesha kuwa unatambua na unathamini kazi anayoifanya Mungu kwenye maisha yako.

-          Kumbuka kuwa huwezi kuhesabu mambo ambayo Mungu anakutendea kwenye maisha yako. Wema wa Mungu umekuzunguka muda wote na pande zote ndio maana leo hii uko hai bila kujalisha mazingira unayopitia.

-          Sasa kule kujua kuwa wema wa Mungu umekuzunguka pande zote na kwamba hajakuacha, yuko pamoja nawe katika hali zote, kunakupa hali ya kuendelea kumtegemea na kumwamini, ndipo swala la kumshukuru linapokuja hapo.

Unaweza ukamshukuru Mungu kwa njia mbalimbali kama vile:-

-          Maombi ya shukrani

-          Sadaka ya shukrani

-          Nyimbo za shukrani n.k

 

NINI KINATOKEA UNAPOMSHUKURU MUNGU

1.      Mungu anakufungulia msimu mpya mbele yako ambao ameachilia nguvu zake zikusaidie kwenye huo msimu.

Mwanzo 8 : 15 – 22

Mungu alirejesha majira yaliyokuwa yameharibiwa na gharika baada ya kusikia harufu nzuri ya sadaka iliyotolewa na Nuhu. Tunaamini yakuwa ilikuwa ni sadaka ya shukrani kwa sababu tunaona Mungu akirejesha kwa upya majira yaliyopotea.

Tunapoingia msimu mpya hasa huu mwaka mpya wa 2023 ni muhimu kuwa na baraka za Bwana ambazo zitatufanikisha katika njia tunazopitia.

Kwa wengine mwaka mpya unaweza ukawa ni mambadiliko tu ya tarehe lakini kwenye yao hakuna chochote kinachobadilika. Lakini kwetu sisi tunaomjua Mungu, mwaka mpya ni msimu mpya. Maana yake ni lazima tuone baraka na uweza wa Bwana ukiwa juu yetu kwa viwango vingine ili kutufanikisha na kutusaidia.

-          Kama ni utumishi, basi tunamuona Mungu akiinua viwango vyetu vya kutumika mbele zake kwa utukufu na na kibali kikubwa.

-          Kama ni hali ya kiuchumi kwenye familia, basi tunamuona Mungu akihusika kuinua uchumi wetu kwa viwango vya juu zaidi.

 

2.      Unampa Mungu nafasi ya kushughulika na adui zako.

2 Nyakati 20 : 15 – 17, 21 – 22

Hawa wana wa Israel walimshukuru Mungu kabla ya vita wakiamini kwamba Mungu atawapigania, na ndivyo ilivyokuwa kwani Mungu aliwashindia vita bila wao kupigana.

-          Unapomshukuru Mungu katikati ya magumu unayopitia inaonyesha ni kwa jinsi gani unamtegemea Mungu akusaidie kukuvusha katika hiyo hali.

-          Wana wa Israel waliona vita ni vikubwa na adui zao ni wengi kuliko wao, kwa namna yoyote ile ilikuwa ni vigumu sana kuishinda ile vita bila msaada wa Mungu. Lakini walipotambua siri iliyopo katika shukrani basi walishinda vita kwa kumshukuru Mungu.

Kuna wakati unaweza ukawa unapitia hali Fulani ambayo si nyepesi kwenye maisha yako lakini ghafla ndani ya moyo wako unakuja wimbo au nyimbo za kumshukuru na kumsifu Mungu, ujue kuwa Roho Mt anakujulisha ni nini unachotakiwa kukifanya kwa wakati huo. Maana yake Mungu anataka umshukuru Yeye ili Yeye ashughulikie tatizo lako.

 

3.      Utukufu wa Mungu unashuka

2 Nyakati 5 : 1 – 13 – 14

Baada ya wana wa Israel kuijenga nyumba ya Bwana, ile siku ya ufunguzi wakati wanaliingiza sanduku la agano ndani ya hekalu, ndipo walipomsifu na kumshukuru Mungu mpaka utukufu wa Mungu kama moshi ulishuka ukalijaza hekalu lote hata watu walishindwa kuonana.

-          Mungu alijidhihirisha kwa namna ya pekee sana ambapo ule utukufu ulilifunika hekalu lote.

-          Kumbe, tunapomsifu na kumshukuru Mungu basi utukufu wake unashuka kwenye maisha yetu.

-          Na utukufu wa Mungu ukikushukia hutabaki jinsi ulivyokuwa. Ni lazima Mungu akutane na haja za moyo wako, ni lazima maisha yako yabadilishwe, ni lazima Mungu aondoe aibu ya kudharauliwa na kuonewa katika maisha yako.

Matendo 16 : 23 – 26

Wafilipi 4 : 6

 

4.      Kunampa Mungu nafasi ya kufanya zaidi ya vile ulivyo muomba.

Luka 17 : 12 – 19

Hii ni habari ya wale wenye ukoma kumi waliomwende Yesu wakiomba awaponye, yesu aliwaponya lakini ni mmoja wao tu ndiye aliyekuja kushukuru kwa Yesu.

-          Bwana Yesu alishangaa kuona ni mtu mmoja tu ndiye aliyekuja kumshukuru wakati wote waliponywa. Yesu alitegemea awaone wote wakija kumshukuru.

-          Mungu yuko serious na swala la kushukuru.

-          Kushukuru si swala dogo mbele za Mungu, lina uzito wake.

-          Wewe unaweza ukaona ni jambo dogo tena la kawaida lakini mbele za Mungu ni jambo kubwa sana na Mungu huwa analifuatilia.

-          Si watu wengi wanajua kuwa Mungu akikupa kitu huwa anafuatilia kuona kama utamshukuru.

-          Yule aliyerudi kushukuru alipewa kitu kingine ambacho hao wenzake hawakupewa. Alipewa wokovu, maana aliambiwa imani yako imekuponya. Wote mwanzoni waliomba kuponywa lakini aliye shukuru alipewa ziada, (imani yake ilimwokoa).

Tunaposhindwa kumshukuru Mungu kwa mambo tunayomuomba basi huwa tunakosa kupata hata vile ambavyo tungevipata kama tungeshukuru.

Kuna mambo kweye maisha yako ambayo utayapata tu endapo utamshukuru Mungu.

-          Kuna wakati Mungu atakupa upendeleo ambao huo huwezi kuupata usipokuwa mtu wa shukrani mbele za Mungu.

No comments:

Post a Comment

Katika maisha yako usisikilize watu wanasema nini bali msikilize Mungu anasema nini, kwa sababu watu hawajui ni nini ambacho Mungu amekupang...